HATI YA KUKAMATWA MKE WA GBAGBO YAFUNGULIWA,WANAMGAMBO WA DRC KUPATA HUKUMU SIKU TOFAUTI
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) imeamua kuachia huru
hati ya kukamatwa kwa mke wa aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Simone
Gbagbo huku mahakama hiyo pia ikitanganza kwamba itatoa hukumu siku
mbili tofauti katika kesi zinazowakabili wanamgambo wa zamani wa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
ICC
Hati ya kukamatwa mke wa Gbagbo yafunguliwa: Majaji wa Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) Alhamisi waliamua kuifungua hati ya
kukamatwa mke wa Rais wa zamani wa Ivory Coast, Simone Gbagbo
anayekabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Hati hiyo ya
kukamatwa kwa mwanamke huyo ambayo awali ilitolewa Februari 29, mwaka
huu, inadai kuwa mwanamke huyo anahusika kwa mashitaka ya uhalifu dhidi
ya binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji na aina nyingine za
unyanyasaji wa kijinsia ilifanywa kati ya Desemba 16, 2010 na Aprili 12,
2012. Ghasia hizo zimekuja kufuatia mume wake, Laurent Gbagbo na Rais
wa sasa wa nchi hiyo Allasane Ouattara kila mmoja kujitangaza kuwa Rais
baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. Wakati Gbagbo mwenyewe hivi sasa
anashikiliwa jela ICC akiwa anakabiliwa pia na mashitaka ya uhalifu
dhidi ya binadamu, mkewe, Simone anashikiliwa kizuizini, Kaskazini mwa
Ivory Coast na watawala wapya wa nchi hiyo.
Viongozi wa wanamgambo wa zamani DRC kuhukumiwa siku tofauti:
Mahakama ya Kimataiafa ya Makosa ya Jinai (ICC) Jumatano iliamua kutoa
hukumu katika kesi inayowakabili viongozi wa wanamgambo wa zamani wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mathieu Ngudjolo na Germain
Katanga katika siku tafauti. Wakati hukumu ya Ngudjolo imepangwa
kutolewa Desemba 18,mwaka huu, ile ya Katanga itatolewa hukumu si kabla
ya mapema mwakani. Viongozi hao wawili wanakabiliwa na mashitaka ya
uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa na wanamgambo waliokuwa chini yao
eneo la Bogoro, Ituri, Mashariki mwa DRC Februari 24, 2003.
Wanachama wa ICC wahitimisha mkutano wao: Nchi wanachama waliotia
saini kuanzishwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC),
wamehitimisha mkutano wao Jumatano wiki hii. Katika maazimio
yaliyopitishwa na mkutano huo ni pamoja na bajeti ya Euro milioni 112
ikiwa ni chini ya kiwango kilichoombwa na mahakama hiyo ambacho ni Euro
milioni 118.
Mwendesha mashitaka ICC achunguzi waasi wa M23: Mwendesha Mashitaka
wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Fatou Bensouda
alisema Jumatano wiki hii kwamba Mahakama yake itachunguza uhalifu
unaodaiwa kufanywa na kundi la waasi la M23, Mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC). Alionya kwamba matukio ya hivi karibuni
yanaashiria kutokea kwa ghasia zaidi katika kanda hiyo. Kundi la M23
linaoongozwa na waasi wa jeshi la DRC wakiwemo Bosco Ntaganda na
Sylvetstre Mudacumura ambao hati za kukamatwa kwao zimeshatolewa na
mahakama hiyo.
RWANDA
Kesi ya Mugesera kuanza kusikilizwa Desemba 17: Mahakama moja nchini
Rwanda Jumatatu iliahirisha tena kuanza kusikilizwa kwa kesi ya mauaji
ya kimbari dhidi ya mwanasiasa mkongwe nchini humo, Leon Mugesera,
aliyerejeshwa kutoka Canada karibu mwaka mmoja uliopita.Majaji wamepanga
tarehe mpya ya Desemba 17, mwaka huu kuanza kusikiliza kesi hiyo.Kesi
hiyo imeahirishwa kutoa muda zaidi kwa wakili wa mshitakiwa huyo kutoka
Kenya iweze kuajiandaa.
WIKI IJAYO
Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya utetezi
inayomkabili kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC), Jean Pierre Bemba anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na
uhalifu wa kivita itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Novemba 26.
Uhalifu huo unadaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri
ya Afrika ya Kati.
0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia