JAMII nchini imeaswa kutumia ipasavyo fursa
zilizopo na zinazotolewa na Serikali au mashirika mengine ya ndani na nje ya
nchi hususani shirika la kazi duniani (ILO) kwa kuwa wabunifu na kujituma ili
waweze kujiendeleza kimaisha.
Hayo yameelezwa juzi mjini Kateshi wilayani
Hanang’ mkoani Manyara na Ofisa Maendeleo ya mifugo na uvuvi wa wilaya hiyo Dk
Tom Maeda,kwenye uzinduzi wa mpango wa ukuzaji wa ujasiriamali kwa vijana wenye
kauli mbiu moto wa nyika.
Katika uzinduzi huo ulioandaliwa na asasi ya
Disabled and Orphans Hope Centre (Dohoce) ya wilayani Hanang’ kupitia shirika
la kazi duniani (ILO) Dk Maeda alisema huu ni wakati wa wajasiriamali nchini
kuchangamikia fursa zilizopo.
Alisema wilaya hiyo ni sehemu ya jumuiya ya
watanzania wenye kuwajibika kutekeleza malengo ya milennia na dira ya Taifa ya
mwaka 2025 na mkakati wa kukuza uchumi na kuondoa umasikini (Mkukuta) namba
mbili.
“Haya yote yanategemea kwa kiwango kikubwa
utashi wa jamii hasa vijana kujituma,kuwa wabunifu na kupenda kujiajiri wenyewe
kwa kutumia fursa zilizopo na zinazotolewa na Serikali na asasi za kijamii,”
alisema Dk Maeda.
Naye,Mratibu wa Dohoce,Kianga Mdundo alisema
takwimu zilizotolewa na Waziri wa kazi na ajira Dk Makongoro
Mahanga,zinaonyesha kuwa watanzania walioajiriwa kwenye sekta rasmi ni asilimia
30,ajira Serikali asilimia tano,sekta zisizo rasmi asilimia 35 na wasio na
ajira asilimia 30.
Mdundo alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya mahesabu ya mashirika ya umma,Zitto Kabwe alisema wahitimu wa vyuo vyote
nchini kwa mwaka ni 650,000 na wanaopata ajira ni 40,000 na 610,000 waliobaki
wanakosa ajira.
“Kwa hiyo soko la ajira isiyo rasmi ndiyo
inayotegemewa kuwa mkombozi wa vijana katika kujiletea maisha bora kwa kila
mtanzania hivyo Dohoce imeamua kuwajengea uwezo jamii iliyopo wilayani Hanang’,”
alisema Mdundo.
Kwa upande wake,mwezeshaji wa mafunzo hayo
Julius Slaa alisema kada zilizopatiwa mafunzo hayo na kupatiwa cheti ni mafundi
wa ushonaji,seremala, magari,pikipiki,waashi,mamalishe,wakulima,wafugaji na
wasindikaji vyakula.
Slaa aliwataja wengine ni wakuzaji miche ya
miti,wadau wa sokoni,wana harakati wa mazingira,wafugaji wa nyuki,taasisi za
fedha,wasimamizi na waandaji wa mipango,wakuzaji miche ya miti,wana michezo na
wana habari.