HALI si shwari ndani ya Kanisa la Kiinjilili la
Kilutheri(KKKT) Dayosisi mkoani Arusha mara baada ya waumini wa kanisa hilo usharika
wa Ngateu kuwazomea na kisha kuwafungia madhabauni baadhi ya viongozi wa kanisa
hilo huku wakitishia kujitenga wakipinga kitendo cha kuvuliwa madaraka
mchungaji kiongozi wa usharika huo,Phillemon Mollel.
Tukio hilo lilijitokeza
jana majira ya saa 5;30 asubuhi ambapo baadhi ya waumini wa usharika huo
walijawa na jazba na kisha kuanza kumzomea msaidizi wa askofu mkuu wa dayosisi
mkoani hapa,Solomon Masangya aliyekuwa ameambatana na askofu mstaafu wa kanisa
hilo,Gabriel Kimereki kanisani hapo.
Hivi
karibuni kanisa hilo lilimvua madaraka mchungaji kiongozi wa usharika
huo,Mollel kwa kile kinachodaiwa ni kuwashawishi waumini wa kanisa hilo
wasichangie fedha za kulipa deni la hoteli inayomilikiwa na kanisa hilo ya
Corridor Springs ambayo iko hatarani kupigwa mnada na benki mojawapo hapa
nchini .
Hoteli hiyo
inadaiwa mkopo na benki hiyo kiasi cha jumla ya $ 4 milioni sawa na sh,11
bilioni kiasi kilichopelekea kanisa hilo kuwachangisha waumini wake ili waweze
kuokoa deni hilo ili isiweze kupigwa mnada wakati wowote kuanzia sasa.
Baadhi ya
waumini wa usharika wa Ngateu jana walijikusanya katika viunga vya kanisa hilo
katika kikao cha kupinga kuvuliwa madaraka mchungaji wao ambapo hatahivyo kikao
hicho hakikufanikiwa kumalizika kwa amani.
Awali akiongea
katika kikao hicho,msaidizi wa askofu wa dayosisi mkoani hapa,Masangya
aliwaambia waumini hao ya kuwa amefika kanisani hapo kusikiliza kero yao na
kuwataka watulize jazba kitendo ambacho kilipingwa vikali.
Hatahivyo,mara baada ya mvua kunyesha kwa wingi aliwashauri waumini hao waingia
ndani ya kanisa lao ili waweze kufanya kikao hicho kwa utulivu kitendo
kilichopokelewa na kisha waumini hao kuingia ndani ya kanisa hilo.
Akiwa ndani
ya kanisa hilo msaidizi huyo aliibua gumzo mara baada ya kuwaambia ya kwamba
anaomba akutane na baraza la wazee wa usharika huo na kisha baadaye atawapa
taarifa ya kile kilichojadiliwa.
Hatahivyo,waumini
hao walipinga wazo hilo kwa madai kwamba hakuna usiri wowote katika jambo hilo
na kitendo cha kutaka kukutana na baraza hilo ni kutaka kuficha baadhi ya mambo
ambayo wamekuwa na wasiwasi nayo.
“Jamani
ndugu waumini nawaomba mtoke nje ili nikutane na baraza la wazee wa usharika
wenu alafu tukimaliza kuongea nao tutawapa taarifa kamili”Masangya alisikika akiwaambia
waumini
Mara baada
ya vuta ni kuvute hiyo ndipo katika hali isiyo ya kawaida askofu mstaafu wa
kanisa hilo mkoani Arusha,Kimerei aliamua kuamka na kutangaza ya kwamba
kikao hicho kimehairishwa hali ambayo ilichafua hali ya hewa kanisani hapo.
Hatahivyo,baadhi
ya waumini waliokuwepo ndani ya kanisa hilo walianza kuwazomea viongozi hao wa
kiroho na wengine wakionekana wakifunga milango ya kanisa hilo ili wasitoke nje
hali iliyopelekea viongozi hao kukimbizwa katika moja ya ofisi zilizopo ndani ya kanisa hilo kwa
muda lakini baadaye walitoka nje na kisha kutokomea.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti baadhi ya waumini wa kanisa hilo walisema ya kwamba endapo
mchungaji wao asiporudishwa kuongoza kanisa hilo patachimbika huku wakimtaka
askofu mkuu wa kanisa hilo dayosisi mkoani hapa,Thomas Laiser sanjari na
katibu mkuu,Israel Ole Karyongi wote waachie ngazi.
Waumini
hao
walidai kwamba wako tayari kujitenga na kuanzisha dhehebu lao huku
wakitangaza msimamo wa kutopeleka sadaka zao mbele ya dayosisi hiyo kwa
madai kwamba kuna
wamenusa harufu ya ufisadi.
"Kuanzia
leo hatupeleki sadaka yoyote dayosisi na tunataka mchungaji wetu
atuongoze kwenye sadaka ya mwaka mpya hatumtaki mchungaji yoyote
wakitulazimisha patachiumbika hapa ni bora tujitenge"walisema kwa
nyakati tofauti
Alipotafutwa
Ole Karyongi hakuweza kupatikana lakini alipotafutwa Laiser alijibu kwa kifupi
kwamba kwa sasa hayuko tayari kuongea chochote kwa kuwa yuko hospitalini na
anapata matibabu
.