ALIYEKAMATWA NA PEMBE ZA NDOVU NI ASKARI WA JWTZ


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema kwamba mwanajeshi aliyekamatwa juzi katika tukio la ujangili mkoani Arusha ni askari wake.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe jana alimtaja askari huyo kuwa ni mwenye namba MT 59509 Sajenti, Azizi Athuman Yusufu ambaye alisema ni askari wa jeshi hilo na alikuwa dereva wa mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe anayefundisha hapa nchini.

Hata hivyo Kanali Mgawe alisema mkufunzi huyo wa kijeshi, hakuwapo wakati wa tukio hilo. “Kweli huyo ni askari wetu. Alikuwa anamwendesha mkufunzi wa kijeshi kutoka Zimbabwe. Siku hiyo alimrudisha nyumbani kwake saa saba mchana na kwenda kupaki gari. Lakini baadaye saa moja usiku, alikwenda kulichukua gari hilo na kutokomea nalo kusikojulikana hadi alipokutwa katika tukio hilo,” alisema Kanali Mgawe.

Wakati JWTZ likitoa taarifa hiyo, Polisi mkoani Arusha jana lilieleza jinsi askari huyo alivyokamatwa. Hata hivyo namba ya askari huyo ilitofautiana na namba ya askari ikimtaja kuwa ni mwenye namba MT 59503.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema askari huyo alikamatwa saa 5:00 usiku wa Januari 20 mwaka huu. Alikutwa na pembe mbili za ndovu na bunduki moja aina ya Riffle yenye namba 458.

“Tunaamini bunduki hiyo ndiyo iliyotumika kwenye uwindaji huo haramu,” alisema.
Kamanda Sabas alidai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na wenzake zaidi ya wawili ambao walikimbia wakati mwenzao huyo anakamatwa eneo la Manyara Kibaoni Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

“Gari lililohusika kwenye uhalifu huu limethibitika kuwa ni mali ya JWTZ na uchunguzi unaendelea kujua namna gani wahusika walifanikiwa kuondoka nalo kambini na kwenda kulitumia kwenye uhalifu huo,” alisema Sabas.

Awali, habari kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa gari hilo lilikuwa na zaidi ya abiria watatu ambao mara baada ya matairi mawili kupasuka, moja la mbele kulia na jingine la nyuma kushoto watu wawili waliteremka na kutokomea porini na mizigo isiyojulikana.

Ilidaiwa kuwa baada ya wananchi kufika kwa nia ya kutoa msaada kwa majeruhi, mtuhumiwa aliyekutwa akiwa amevaa jaketi la JWTZ na suruali ya jinsi pamoja na bunduki, aliwahakikishia wananchi waliotaka kuwakimbiza watu hao wakidhani wamemwibia wasishughulike nao kwa kuwa hajaibiwa chochote.

Baada ya wananchi na askari wa jeshi la polisi waliofika kumtilia shaka mtuhumiwa, msako ulifanyika kuelekea walikokimbilia abiria hao garini na mizigo, lakini hawakuonekana.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post