Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa
MWENYEKITI wa Kamati Kudumu ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowasa, ameeleza kushtushwa na
wingi wa vijana gerezani na mahabusu na kusema kuwa hiyo ni hatari kwa
uchumi wa nchi.
Lowasa alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati kamati
yake ilipokutana na viongozi wa Jeshi la Polisi, magereza na Wizara ya
Mambo ya Ndani kwa ujumla kwa ajili ya kujadili udhaifu ulioko kwenye
magereza.
Alisema katika ziara ya kamati yake hivi karibuni ya kutembelea
magereza mbalimbali nchini alibaini kwamba asilimia 90 ya vijana ndiyo
waliojazana katika magereza kama wafungwa na mahabusu na kusema tatizo
linachangiwa na ukosefu wa ajira.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema wajumbe wa
kamati yake katika ziara hiyo walibaini udhaifu mkubwa katika utendaji
kazi kati ya idara ya upelelezi, magereza na jeshi la polisi na kutaka
viongozi wa juu kulishuighulikia suala hilo.
Alisema katika gereza la Segerea walibaini kuwa lilikuwa na
mahabusu zaidi ya uwezo wake kwa asilimia 23, kwani lina wafungwa 98 na
mahabusu 2,400.
“Hali hii inaitia aibu nchi yetu katika vyombo vya kimataifa
vinavyotetea haki za binadamu, kwa sababu makosa mengi yanayosababisha
mlundikano huo wa mahabusu ndani ya magereza ni makosa ya kijinga
kabisa kama vile kuiba kuku, baiskeli, kuzurura au kupiga kelele,”
alisema.
Aliongeza kuwa wamebaini kuwapo uonevu kwa wanawake, alitoa mfano
kwa mahabusu mwanamke aliyewaeleza alikamatwa kwa kosa la kuzurura
wakati alikuwa ametumwa dukani na mumewe kununua dawa na kwamba wakati
anakamatwa alijitetea na mumewe lakini polisi waliomkata
walimng’ang’ania na kumtaka alipe faini ya sh 200,000.
Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Umma (POAC)
imeurejesha ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili
urekebishe hesabu za taasisi hiyo kwa miaka minne ya fedha tangu 2008
hadi mwaka 20011 pamoja na makosa mengine zaidi ya 25.
Pamoja na UDSM, pia wamemtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kufanyia ukaguzi sh milioni 317 za Taasisi ya Mimea Nchini (TPRI)
za mwaka wa fedha 2011/2012 ambazo zinadaiwa kupelekwa katika Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.