SEMINA na kikao
cha wahariri na waandishi wa habari waandamizi wa michezo na burudani
nchini, vinatarajiwa kufanyika April 12 na 13 mwaka huu, katika
jiji la Arusha.
Semina hiyo, pia
itakwenda sambamba na kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward
Moringe Sokoine ambapo wanahabari hao watatembelea familia na Kaburi la
Sokoine wilayani Monduli ili kutoa pole.
Maamuzi ya
kufanyika semina hiyo na kikao cha wahariri jijini hapa, yalifikiwa juzi katika
kikao baina ya Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari zamichezo
nchini(TASWA), Juma Pinto na viongozi wa TASWA Arusha katika hoteli ya palace
mjini hapa.
Akizungumza
katika kikao hicho, Pinto alisema TASWA inatarajia kuitisha kikao hicho, Arusha
ikiwa ni sehemu ya mipango yake,kukifanya chama hicho kuwa cha kitaifa
zaidi na pia kuongeza uelewa wa masuala ya michezo kwa wanahabari.
“kamati ya
utendaji ya TASWA taifa hivi karibuni ilikutana ambapo pamoja na mambo mengine
iliamua kuifanya kikao na semina ya wahariri mkoani Arusha hivyo nimekuja
hapa ili tushauriane kuwezesha semina na kikao hiki”alisema Pinto.
Pinto
alisema ili kufanikisha semina hiyo, TASWA taifa na Taswa Arusha,
wanapaswa kushirikiana katika maandalizi ya kutafuta wadhamini, ambapo
pia watashirikishwa wanahabari toka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga na Manyara.
Wakizungumza
katika kikao hicho, Katibu wa TASWA Arusha, Mussa Juma na Katibu
msaidizi Hamza Kalmera walieleza TASWA Arusha kuwa tayari kuandaa semina
hiyo, ambayo itafanyika siku ya kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri mkuu, Edward
Moringe Sokoine pia kutafanyika tamasha maalum la michezo mbali
mbali.
Juma
alisema TASWA Arusha itajipanga kuhakikisha wakati wa semina hiyo,
wahariri na waandishi wa habari waandamizi watapata fursa ya kutembelea kaburi
la Sokoine wilayani Monduli kama
ishara ya kumuenzi.
"tutajipanga
wanahabari waende Monduli juu kutoa pole kwa familia ya Sokoine na pia
siku ya April 13 kufanyike mchezo kati ya TASWA Arusha na TASWA Dar es salaam"alisema
Juma.
Katika semina
hiyo, pia wanahabari hao, wanatarajiwa kupata taarifa ya awali ya marekebisho
ya katiba ya TASWA na pia taarifa ya uanzishwaji wa chama cha kuweka na
kukopa TASWA SACCOs.