MKUU wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara,Christina
Mndeme amepiga marufuku ukataji miti hovyo kwenye wilaya yake kwa ajili ya
matumizi ya uchomaji wa mkaa na uharibifu wa mazingira.
Mndema alitoa agizo hilo juzi,kwenye kijiji
cha Getanuwas wakati akizindua matumizi ya mkaa mbadala uliotengenezwa na
kikundi cha wanawake 27 wa kikundi cha Umoja cha kata ya Getanuwas wilayani
humo.
Mndeme alisema atawachukuliwa hatua kali
watakao kata miti hovyo kwani jamii ya wa mkoa huo inatakiwa kutumia mkaa huo
mbadala kuliko kukata miti hovyo kwani wanaharibu mazingira ya wilaya hiyo.
“Huu mkaa mbadala ni mzuri na unatengenezwa
hapa kwetu Hanang’ hivyo tunatakiwa tuwaunge mkono wote walioubuni kwa kuutumia
kwani hata mimi nautumia mkaa huo ambao kipande kimoja kinauzwa sh200,” alisema
Mndeme.
Pia mkuu huyo wa wilaya alijitolea sh300,000
ili kukiwezesha kikundi hicho mashine ya kutengeneza mkaa huo mbadala kwani
mashine wanayotumia hivi sasa ni mali ya Dayosisi ya Mbulu,inayotumiwa kwa
mafunzo sehemu nyingine.
Naye,Mratibu wa mradi wa kuondoa umaskini na
kukuza uchumi mkoani Manyara,Goma Gwaltu alisema mradi huo umewezeshwa na
shirika la misaada ya makanisa ya Kinorway (NCA) kupitia kanisa la KKKT
Dayosisi ya Mbulu.
Gwaltu alisema kuwa mradi huo wa kutengeneza
mkaa mbadala (Briquettes) utawanufaisha wanawake hao kiuchumi na pia utamaliza
tatizo la uharibifu wa mazingira kwenye wilaya hiyo.
Alisema matarajio yao ni kuutangaza mradi huo
mkoa mzima na teknolojia hiyo ikienea sehemu tofauti itanufaisha kikundi hicho
kwa kutumia nishati mbadala inayotokana na nyasi,karatasi na majani
yaliyoanguka toka mitini.
Kwa upande wake,Askofu wa Dayosisi ya Mbulu
iliyodhamini mafunzo ya mradi huo,Zebedayo Daudi alisema jamii ya eneo hilo
inapaswa kubadilika ili kutunza mazingira kwa kutumia mkaa huo mbadala na
kuachana na ukataji miti.
“Kijiji kiliitwa Getanuwas na jamii ya
wabarbeig kwa kiswahili ni mti mfupi hivyo badilikeni kwa kutunza mazingira na
soko la mkaa huu mbadala litakuwepo tu kwani hata Dar es salaam wanahitaji
huduma hii,” alisema Askofu Daudi.