WANANCHI wa
kijiji cha Sukuro wilayani Simanjiro mkoani Manyara wamemwomba Rais Jakaya
Kikwete aingilie kati sakata la mpaka kati ya kijiji chao na Kitiengare huku
wakisema kuwa wamechoka kunyanyaswa kwa kukamatwa mara kwa mara na kisha
kubambikiwa kesi mbalimbali kana kwamba wao si watanzania.
Pia,wamesikitishwa
na kitendo cha mbunge wa jimbo hilo,Christopher Ole Sendeka kushindwa
kuwasaidia kuutatua mgogoro hadi sasa huku wakidai kusikitishwa na kauli zake kwamba mgogoro huo umeshamalizika.
Wakizungumza
katika mkutnao ulioitishwa na uongozi wa serikali ya kijiji hicho kujadili
tukio la kukamatwa kwa viongozi wa serikali ya kijiji hicho pamoja na chama
juzi wananchi hao kwa sauti ya pamoja walionyesha hali yao ya wasiwasi kwa viongozi wa serikali
mkoani humo.
Akizungumza
katika mkutano huo,mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho,Kaayai Murero alisema kwamba hivi karibuni baadhi ya
viongozi wa serikali ya kijiji hicho pamoja na chama cha Mapinduzi(CCM)
walikamatwa na jeshi la polisi na kasha kuachiwa katika mazingira ya
kutatanisha.
Alisema kuwa
kumekuwa na hali ya wasiwasi kijijini kwao kwa kuwa baadhi ya familia zinaishi
kwa hofu kutokana na mgogoro wa ardhi baina ya kijiji chao na Kitiengare kwa
kuwa wamekuwa wakikamatwa hovyo na jeshi la polisi wilayani humo na kisha
kubambikiwa kesi.
Mwenyekiti
huyo kwa unyonge alimtaka Rais Kikwete kuingilia kati mgogoro huo huku akidai
kuwa umedumu kwa muda mrefu na uongozi wa serikali na chama cha CCM mkoani
Manyara hauonyeshi jitihada za dhati kuutatua mgogoro huo.
Naye,mwenyekiti
wa kitongoji cha Molawak,Lengai Ole Makoo alisema kuwa baadhi ya wananchi
waekuwa wakikamatwa hovyo na jeshi la polisi kwa madai ya kuchangia fedha za
kuendesha kesi iliyopo mahakamani kwa lengo la kudhoofishwa.
Alisema
kuwa wananchi hao wamekuwa wakipigwa na
kutishiwa kunyang”anywa kadi za CCM kwa madai kwamba waachane na kesi ya kudai ardhi waliyoifungua mahakamani wilayani Babati na
kumtaka Rais Kikwete aingilie kati.
Nao baadhi
ya wakazi wa kijiji hicho,Abraham Koringo,Olais Soyai na Magdalena Daniel
walimwomba Rais Kikwete kuwasaidia katika unyanyasaji huo huku wakidai kwamba
wamekuwa wakihangaishwa kana kwamba sio watanzania.
Kwa nyakati
tofauti walisisitiza kwamba baadhi ya wanasiasa pamoja na viongozi wa serikali
hawana nia njema ya kuutatua mgogoro huo uliodumu kwa takribani miaka mitano
kwa kuwa wanaufaika kwa kupokea chochote.
“Tunaitaka
serikali ifanye maamuzi magumu tunamwomba mheshimiwa Rais aingilie kati kwa
kuwa vijiji vya Kitiengare na Sukuro vilitenganishwa kisheria sasa hii leo
tunataka kunyang”anywa ardhi yetu”walisema kwa unyonge wananchi hao
Katika
mkutano huo baadhi ya wazee wa mila maarufu kama Malaigwanani walihudhuria
mkutano huo ambapo kwa sauti ya pamoja walitoa tamko la kuendelea kuchangishana
fedha za kugharamia kesi waliyoifungua mahakamani kudai ardhi ndani ya kijiji
chao.