SAKATA la baadhi ya
wananchi pamoja na wanasiasa kupinga usafirishwaji wa bomba la gesi
kutoka mkoani Mtwara kwenda jijini Dar es salaam limezidi kuchukua sura mpya
baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana wa
CCM(Uvccm) mkoani Arusha,James Ole Milya kutamka ya kwamba serikali ina lengo
la kuufanya mkoa wa Mtwara ubaki kuwa katika lindi la umaskini wa
kutupwa.
Hatahivyo,Milya ambaye kwa
sasa amehamia Chadema amemtaka Rais Jakaya Kikwete pamoja na baraza lake la
mawaziri kuwaonea huruma wakazi wa Mtwara huku akisisitiza ya kuwa wakumbuke
maisha ya miaka 50 ijayo kuanzia sasa na si kujijali peke yao wakati wakiwa madarakani.
“Kitendo cha serikali kutaka
kujenga kiwanda cha gesi Bagamoyo ni kutaka kuumaliza mkoa wa Mtwara ubaki kuwa
maskini wa kutupwa hilo
halikubaliki”alisema Ole Milya
Akihojiwa na gazeti hili jana
jijini hapa,Ole Milya alisema kuwa Mungu hakukosea kubariki rasilimali
mbalimbali katika maeno mengi hapa nchini na ndiyo maana hata Mtwara
kumevumbuliwa rasilimali kama gesi.
Alisema kuwa serikali ina
uwezo wa kujenga kiwanda cha gesi mkoani humo na kasha kuweka utaratibu mzuri
wa kusafirisha gesi hiyo hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kuwa kuna faida
nyingi kwa kiwanda hicho kujengwa mkoani humo kama
huduma za afya kuboreshwa,elimu pamoja na miundombinu hivyo alisisitiza umuhimu
wa kujengwa kiwanda mkoani Mtwara.
Alisisitiza kuwa waziri wa
nishati na madini,Sospether Muhongo hapaswi kuwa na fikra mgando kutoa kauli za
kejeli kwa wakazi wa Mtwara huku akimtaka afikirie maisha ya watanzania katika
kipindi cha miaka 50 ijayo wakati atakapokuwa hayuko madarakani.
Alisema kuwa tatizo kuu la
msingi linaloikabili serikali ya Rais Kikwete ni baadhi ya watumishi wake
kupenda asilimia kumi katika kila mradi huku akidai tabia hiyo ndiyo inaua
nchi.
Hatahivyo,alionya na kutoa
ushauri kwa wakazi wa Mtwara kuwa wanapaswa kutambua ya kwamba rasilimali ya
gesi iliyopo ndani ya mkoa wa wao inapaswa kuwanufaisha watanzania wote.
“Wananchi wa Mtwara ni lazima
watambue ya kuwa rasilimali ya gesi iliyopo pale ni rasilimali ya taifa lote
watu wote wanapaswa kunufaika nayo ila kipaumbele kiwekwe Mtwara”alisisitzia
Ole Milya