PAMOJA na mambo mengine Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga kuzitumia sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa
kwake, kufanya tathmini ya uchaguzi wake mkuu wa viongozi mbalimbali
uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana.
Lengo la tathmini hiyo ni
kujifunza au kukumbushana kwa kina changamoto zilizojitokeza, hivyo
kuitumia fursa hiyo kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya uchaguzi mkuu
mwingine wa ndani ya Chama mwaka 2017.
Hayo yalisemwa na Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
alipozungumza na waandishi wa habari leo, Januari 21, 2013, katika Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.
Nape alisema, sherehe za miaka
36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zitafikia kilele chake
Februari 3, 2013, na zitafanyika Kitaifa kwenye Uwanja wa Lake
Tanganyika mjini Kigoma.
Alisema, mgeni rasmi katika
sherehe hizo ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na zitahudhuriwa
pia na Makamu Wenyeviti wa CCM (Zanzibar) Rais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na
Wajumbe wote wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa wakiongozwa na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.
“Baadhi ya viongozi hasa
sekretarieti na maofisa wa Chama tutaenda Kigoma kwa kreni, na Chama
kimeamua kutumia usafiri huu kama sehemu ya kupongeza juhudi
zinazofanywa na serikali katika kuboresha huduma za usafiri huo”,
alisema Nape
Nape alisema, uamuzi wa
kufanya kilele cha sherehe hizo kuwafanyika Februari 3, 2013 ni kutokana
na tarehe yenyewe ya kuzaliwa kwa CCM, ambayo ni Februari 5, 2013 kuwa
siku ya kazi, hivyo kutoweza kutoa fursa kwa wanachama kushiriki kwa
ufanisi katika sherehe hizo muhimu kwao.
“Sherehe hizi za miaka 36 ya
kuzaliwa kwa CCM zinafanyika ikiwa ni takriban miezi miwili tu tokea
kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama na jumuiya zake zote
ukamilike Novemba 13, 2012, Kwa hiyo ni sherehe muafaka kujipongeza na
vilevile kuwashukuru wanachama wake kwa kukamilisha kwa ufanisi uchaguzi
huo”, alisema Nape.
Alisema ili kuwashirikisha
wanachama katika ngazi zote, uzinduzi wa sherehe hizo utafanyika kwenye
matawi yote, Jumatano Januari 30, 2013, kwa kufanya mikutano ya
wanachama wote, nafasi ambayo itatumika kufanya tathmini ya uchaguzi
mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 katika ngazi hizo.
Nape alisema Alhamisi Januari
31, 2013 itakuwa ni siku ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ambapo wanachama wa
jumuiya hiyo watashiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ambazo
alisema ni pamoja na usafi wa mazingira na upandaji wa miti.
“Kazi nyingine zitakazofanywa
na vijana ni kujadili mafanikio ya UVCCM katika kipindi cha miaka 36
tokea kuzaliwa kwa CCM na Shughuli nyingine itakuwa ni kufanya tathmini
ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012, na mwisho ni
kufanyika kwa matamasha mbalimbali ya michezo yatakayowahusisha vijana
wote”. alisema Nape.
Alisema Februari Mosi, 2013,
itakuwa Siku ya Umoja wa Wazazi. Hao watashiriki katika shughuli za
kijamii ikiwa ni pamoja na kupanda miti, kushiriki katika ujenzi wa
miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa madarasa, zahanati, nyumba za
walimu na kadhalika.
Shughuli nyingine
itakayofanywa na Wazazi ni kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na
jumuiya zake wa mwaka 2012, na pia watajadili mafanikio ya jumuiya hiyo
yenyewe kwa miaka 36 iliyopita. Jumamosi Februari 2, 2013 itakuwa siku
ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Nape aliendelea kueleza kwamba
shughuli zitakazofanywa na wanachama hao wa UWT ni kufanya usafi,
kupanda miti, kutembelea na kufariji wagonjwa katika hospitali na vituo
vya afya, kutembelea vikundi vya uzalishaji mali vya kina mama, kufanya
tathmini ya uchaguzi mkuu wa CCM na jumuiya zake wa mwaka 2012 na mwisho
ni kujadili mafanikio ya UWT kwa miaka 36 iliyopita.
Siku ya kilele cha sherehe
hizo ambazo alisema kaulimbiu yake ni Umoja ni Ushindi kutafanyika
Matembezi ya Mshikamano na kwamba wanachama wa CCM na jumuiya zake zote
nchini kote ambazo ni UVCCM, Wazazi na UWT watafanya Matembezi ya
Mshikamano katika kila tawi kwa muda ambao kila tawi litaona unafaa kwa
kuzingatia hali halisi ya mazingira ya eneo husika.
Vilevile itafanyika mikutano
ya wanachama wote kwenye matawi, kata, wilaya na mikoa ambayo itatumika
kupokea na kujadili maazimio ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika tarehe
11 – 13 Novemba, 2012 na utekelezaji wa Mradi wa Awamu ya Tatu wa
Kuimarisha Chama