Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,Gilles Muroto
akiongea na wananchi wa Mtaa wa Sanawari (hawapo pichani) uliopo kata ya
Sekei halmashauri ya jiji la Arusha juu ya uanzishaji wa vikundi vya
ulinzi shirikishi
Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,Gilles Muroto (wa
tatu kulia) akimtambulisha Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa
Arusha,Mrakibu wa Polisi (SP),Mary Lugola pamoja na askari wengine wa
kitengo hicho mkoani Arusha.
Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto
amewaambia wakazi wa Mtaa wa Sanawari waliopo Kata ya Sekei iliyopo
halmashauri ya jiji la Arusha waunganishe nguvu zao pamoja ili waweze
kuushinda uhalifu.
Hayo
aliyasema jana katika mkutano kati jeshi la Polisi na wananchi hao
uliofanyika katika uwanja wa wazi uliopo mtaani hapo ikiwa ni muendelezo
wa mkakati wa jeshi hilo juu ya utoaji wa elimu ya polisi jamii kuanzia
ngazi ya mtaa na vitongoji vya Mkoa huu wa Arusha.
Mkuu huyo
wa Polisi wilaya alisema kitendo cha watu wachache kujitokeza
kuhudhuria katika mkutano huo ambao ulikuwa unajadili mambo mbalimbali
ya maendeleo ya mtaa pamoja na masuala ya ulinzi ni dalili tosha kwamba
baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawana umoja.
“Hii
inashangaza yaani mkutano ambao umetangazwa karibu kila nyumba na una
lengo la kujadili maendeleo ya mtaa ambao umehudhuriwa na viongozi wa
mtaa pamoja na Diwani wa kata lakini watu wachache, hii ni hatari na
hamtaweza kusonga mbele.” Alionya Mkuu huyo wa Polisi wilaya.
Alisema
hali hiyo ya utengano ndio inayotoa mwanya kwa wahalifu kufanya uhalifu
kwani mpaka hivi sasa mtaa huo hauna vikundi vya ulinzi shirikishi kwa
kuwa wananchi hawahudhurii katika mikutano ili waweze kushirikiana na
jeshi la Polisi kujadili suala hilo.
Mrakibu
huyo Mwandamizi wa Polisi alisema kwamba, suala la ulinzi si la
kiitikadi za kisiasa bali watu wa vyama vyote wanatakiwa washiriki kwani
mhalifu anapovamia sehemu hamuulizi mwenye mali kama ni kiongozi,
mwanachama au shabiki wa chama gani bali anaangalia kile
anachokiihitaji.
Aliwataka
wananchi wa Mtaa huo kuanza kuchukua hatua za kupambana na wahalifu kwa
kuanzisha kikundi cha ulinzi shirikishi ambacho kitaendeshwa kwa
michango ya kila mkazi ambaye atapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya
kuwalipa posho walinzi pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile tochi, sare
na kadhalika.
Aliongeza
kwa kusema ili kikundi kikamilike inatakiwa wawe na silaha ya moto
ambayo itawasaidia katika shughuli za doria badala ya kutumia marungu
pekee. Alisema kikundi hicho kitakuwa kinafanya kazi hiyo kwa
kushirikiana na jeshi la polisi ambapo pale wanapoona kuna matatizo
watakuwa wanawasiliana na yeye au viongozi wengine wa jeshi hilo moja
kwa moja ili waongezewe nguvu.
Mkutano
huo uliohudhuriwa na Diwani wa Kata ya Sekei Mh. Chrispin Tarimo,
Mwenyekiti wa mtaa huo Godfrey Mollel, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii
Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi Mary Lugola, Polisi Tarafa ya Themi
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Zuhura na askari wengine toka kitengo hicho
ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mkuu huyo wa Polisi wilaya kwa
wenyeviti wa mitaa ya halmashauri ya jiji Arusha ya kufanya mikutano na
wananchi ili kuimarisha ulinzi ndani ya wilaya ya Arusha.