NJAA KALI YAWAKUMBA WAHADIZABE

Watu wa jamii ya  Wahadzabe wanaoishi porini kwa kula mizizi, asali na kuwinda wanyama wadogo  katika eneo la Eyasi Wilayani Karatu Mkoani Arusha wanakabiliwa na njaa kali inayotishia maisha yao .
Waandishi wa habari waliotembelea eneo  hilo  mwishoni mwa wiki walishuhudia makundi ya Wahadzabe  wakipita katika vijiji vya  jirani na maeneo yao huku wakiomba chakula .
Wakizungumza na waandishi wa habari ,watu wa jamii hiyo walisema kuwa ongezeko la wafugaji  na mifugo na wakulima limesababisha mizizi ,matunda na asali  kupotea kabisa.
 

“Kuna maelfu ya ngombe wamemaliza msitu hakuna kitu tena hatuoni tumbili wala digidigi  ,pia   kuna machimbo ya madini yameanzishwa ,wafanyabiashara wanakata miti na kuchoma mkaa hali  hii inatishia uhai wetu, ”alisema  Kankono Mkanga kwa niaba ya wenzake.
Aliongeza kuwa maeneo yao hivi sasa vimeanzishwa vitalu vya uchimbaji madini  huku wengine wakijenga kambi za kitalii hali ambayo inatishia uhai wao kuliko nyakati mbaya zilizowahi kuwapata katika historia yao nchini.
Walisema kwa sasa hali ni  mbaya kiasi cha kuwafanya kukosa mlo kati ya siku moja hadi mbili huku waathirika wakiwa ni watoto na wazee wao.“Tunakabiliwa na njaa kali ,huwa tunapata chakula kutoka katika makanisa yaliyopo Mangola  na watalii lakini hadi sasa hatujapata chochote mwaka huu”alisema Kankono.
Kwa mujibu wa Ngake Mtawona  Mtawona,  ardhi yao imepokwa na wakulima na wafugaji na kuwaacha  bila kitu na kuwa omba omba wa kudumu.
"Tunaomba chakula , wanyama wametoweka  na sisi tunategemea zaidi nyama kama njia yetu ya asili ya kuishi ."  alisema mzee  mmoja wa kihadzabe  akiwa anatengeneza   mishale  kupitia kwa mkalimani .
Alisema tukipita katika vijiji kuomba tunapewa vitunguu na tunakula kama chakula na wakati mwingine tunaumwa tumbo lakini hatuna la kufanya kwani ni suala la kifo na maisha
WAHITAJI CHAKULA HARAKA
Afisa Tarafa ya Eyasi , Laanyun Ole Supuk , amethibitisha jamii hiyo kuwa katika tishio la kupotea kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokuwa  na chakula na kuiomba serikali kupeleka chakula cha msaada haraka.
Ole Supuk aliongeza kuwa tatizo kubwa ni mfumo wa maisha ya  jamii hiyo  ya kutokuweka chakula cha akiba.
 “Nafikiri ikiwa watu hawa ambao wako 400 katika eneo hili wakipata tani za mahindi 80 itawasaidia hadi msimu mkubwa wa utalii utakapoanza
kwani watalii watakuwa wengi na watapata fedha za kununua chakula wenyewe, “ alisema.
 Wahadzabe jamii ambayo huishi kwa makundi madogomadogo wanakadiriwa kuwa 1,500 nchini. Maisha yao yamekuwa yakifanana na watu wa mwituni kutoka Klahari nchini Botswana.
 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post