SERIKALI
imeipa kazi ya kuandaa mpango kabambe (Master Plan) wa mipango miji
kampuni ya kimataifa ya Surbana International Pty Ltd ya nchini
Singapore kwa ajili ya majiji ya Arusha na Mwanza.
Kampuni hiyo inatakiwa kukamilisha shughuli hiyo ndani ya miezi 13 tangu kusainiwa kwa mkataba huo.
Mkataba huo ulisainiwa wiki iliyopita jijini hapa na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata na Ofisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Kong Wu Mun.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Waziri wa Nchi wa Mambo ya
Nje na Mambo ya Ndani wa Singapore, Masagos Zulkiflg walikuwepo
kushuhudia tukio hilo la utiaji saini.
Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Kidata alisema tukio
hilo ni mwendelezo wa mchakato uliokuwa umeanza kufuatia mkataba wa
makubaliano ambao Wizara ya Ardhi ilisainiana na Singapore Desemba 2013
kwa niaba ya Tanzania.
Alisema lengo la kuanzisha mradi huo ni kuwezesha miji iliyopangiliwa
vizuri na yenye maendeleo na kuondokana na msongamano wa magari pamoja
na nyumba zisizokuwa na mpangilio jijini Arusha.
“Kuwepo kwa mpango huu kutawezesha kwa kiasi kikubwa sana kuishi
katika mpangilio unaohitajika na kuchangia nchi kupata maendeleo kwa
kuwa na miundombinu ya kutosha katika maeneo yenye mpangilio,” alisema
Kidata.
Alisema kuwa wanatarajia kusaini mkataba na kampuni ya China kwa
ajili ya kuandaa mpango kabambe kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara
ambayo inatazamiwa kukua kwa kasi kubwa kutokana na kugunduliwa kwa
nishati ya gesi.
Zulkiflg alisema kuwa nchi yake imejikita katika kusaidia mataifa
yanayoendelea, hasa kwa kuwasaidia kuandaa uwepo wa mipango miji jambo
alilodai kuwa litaharakisha maendeleo kwa kuhamasisha uwekezaji toka
mataifa mbalimbali