Baadhi ya washiriki wa mashindano ya resi za Ngalawa wakijiandaa tayari kwa kuanza mashindano hayo katika shamra shamra za tamasha la 17 la ZIFF 2014 linaloendelea visiwani Zanzibar.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar
NGALAWA zote 11 zilizoingia majini kukamilisha mzunguko wa saa mbili wa resi za ngalawa mjini Zanzibar zilimarisha mashamshamu hayo bila najali na timu tatu zilipewa zawadi za ushindi.
Resi za Ngalawa kama zinavyojulikana ni utamaduni halisi wa visiwa vya pemba na Unguja na ni sehemu ya tamasha kubwa la filamu la kimataifa la Zanzibar ambalo linaendelea visiwani hapa.
Kwa wale waliozaliwa maeneo ya bara, resi hizi zilikuwa kivutio kikubwa kwao kutokana na maandalizi yanayofanywa kabla ya kuingia majini na dau kunyanuliwa.
Wakati dau limenyanyuliwa, maji yamekuwa yakichotwa ama ndani ya Ngalawa au nje katika bahari kumwagia tanga katika hali inayoelezwa kuliimarisha katika ukinzani wa upepo.
“mbio za Ngalawa ni kipimo kikubwa cha Uzanzibari wetu na kila mwaka ZIFF huhitimisha utashi wake wa kuwa na tamasha la nchi za jahazi kwa kuwa na mbio za ngalawa” alisema mshehereshaji Muslim Nassoro Abdalla katika shamrashamra zilizofanyika ufukweni kandoani mwa hoteli ya Tembo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (mwenye t-shirt ya njano) akupiliza Kipenga kuashiria kuanza kwa mashindano hayo yaliyofanyika kwenye fukwe za Hoteli ya Tembo visiwani Zanzibar.
Muslim ambaye alisema kwamba mwaka huu walitaka kuwa na mbio za timu 20 (ngalawa) walishindwa kuhitimisha ndoto hiyo kutokana na masuala nje ya uwezo wa ZIFF.
Ili kukamilisha vyema mbio hizo kunatakiwa kuwa na boti za kutosha za uokozi kama kutatokea ajali.
Mwaka juzi kulitokea ajali ambayo hata boti ilipofanya uokozi nayo ikazidiwa na kulazimisha watu kukwama mpaka jioni walipopata boti nyingine kutoka Bandarini.
Wakati wa mbio za resi ambazo washindi wa kwanza ni timu iliyokuwa ikiongozwa na Hatibu Suleiman waliokuwa ndani ya ngalawa Ipo Siku, ngoma mbalimbali za asili zilipigwa ufukoni kama hamasa huku watu wakisubiri marejeo ya ngalawa hizo.
Baadhi ya Ngalawa zinazoshiriki mashindano hayo zikianza kukata mawimbi.
Mbio hizo ambazo zilianzishwa na mbunge wa Kiembesamaki na Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mahmoud Thabiti Kombo mshindi wake wa pili alikuwa ni timu ya haji Hassan (kama nadhodha) ndani ya ngalawa Kipanga. Aidha Hassan Simai na wenzake waliokuwa katika ngalawa iliyoitwa peace of Love walikuwa washindi wa tatu.
Timu ya ngalawa ambayo inahitaji ujuzi katika utekaji tanga , kulirekebisha na kubalansi ngalawa inahitaji watu wapatao watano na si chini ya watatu.
Tamasha la filamu linaendelea mjini hapa kwa shughuli mbalimbali zikiwemo za mafunzo ya utunzi, utengenezaji wa filamu na uhakiki wake.
Pichani juu na chini ni Sehemu ya wakazi wa Zanzibar wakishuhudia mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mahmoud Thabit Kombo ( wa pili kulia) akiwa meza kuu na mmoja wa wadhamini wa mashindano hayo Mohammed
Burudani ya Ngoma kutoka Nungwi ikitumbuiza wakati wa mashindano hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akionyesha moja ya zawadi t-shirt kwa watoa burudani waliokuwa wakishindana kucheza ngoma za asili.
Mkazi wa Nungwi na Stone town (mwenye kaptura) wakishindana kutoa burudani ya ngoma za asili za visiwani humo wakati wa mashindano hayo.
Mshehereshaji wa tamasha la ZIFF 2014, Muslim Nassor akimuonyesha moja ya zawadi (haipo pichani) mkazi wa Stone town aliyekuwa akisherehesha wakati wa mashindano ya Ngalawa kwenye fukwe za hoteli ya Tembo visiwani Zanzibar.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akikabidhi zawadi kwa mshindi wa tatu nahodha wa resi za Ngalawa iliyopewa jina la " Peace of life" M, Bw. Hassan Simai.
Mshindi wa tatu nahodha wa resi za Ngalawa, "Peace of life" Bw. Hassan Simai katika picha ya pamoja na mdhamini wa Ngalawa yao iliyopewa jina la " Peace of life" Mkurugenzi mtendaji wa Zanlink, Bw. Sanjay Raja.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akikabidhi zawadi kwa mshindi wa pili nahodha wa resi za Ngalawa iliyopewa jina la "Kipanga" Haji Hassan. Katikati ni mdhamini wa Ngalawa ya Kipanga, Bi. Latifa Mohamed Omar kutoka Zan Air.
Mwenyekiti wa Bodi ya ZIFF, Mh. Mahmoud Thabit Kombo akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza wa nahodha mashindano ya resi za Ngalawa, Bw. Khatib Suleiman katika shamra shamra za tamasha la 17 la ZIFF linaloendelea kutimua vumbi visiwani Zanzibar.
mshindi wa kwanza wa mashindano ya resi za Ngalawa, Bw. Khatib Suleiman (kushoto) akipongezwa na mdhamini wake mwakilishi wa Com-Net Zanzibar Bw. Mohammed (katikati). Kulia ni Mwenyekiti wa bodi ya ZIFF, Mh. Mahmoud Thabit Kombo.