Peter Muthirika anayeongoza chama cha DPP ndiye raisi mpya wa Malawi
Rais
mpya wa Malawi Peter Mutharika ameapishwa rasmi baaada ya
kucheleweshwa kwa matokeo ya uchaguzi kufuatia madai ya udanganyifu na
wizi wa kura. Mutharika aliibuka mshindi wa uchaguzi huo baada ya
kujipatia zaidi ya asilimia 36 ya kura zilizopigwa. Rais anayeondoka
mamlakani Joyce Banda alikuwa katika nafasi ya tatu.
Banda amewataka wafuasi wake kuheshimu matokeo hayo.
Mahakama kuu ilipinga ombi la kura kuhesabiwa
upya baada ya Banda kudai kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa katika
shughuli hiyo.
Peter Mutharika aliwahi kuhudumu kama waziri wa
maswala ya kigeni na ndugu ya aliyekuwa rais wa taifa hilo marehemu
Bingu wa Mutharika aliyefariki mwaka 2012 akiwa afisini.
Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza amesema kutoka
mjini Blantyre kuwa Profesa Peter Mutharika ameshinda uchaguzi huo kwa
kupata asilimia 36.4 ya kura zote akifuatiwa na Dr Lazarus Chakwera
mwenye asilimia 27.8 huku Rais anayemaliza muda wake Dr Joyce Banda
akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 20.2 na Atupele Muluzi amekuwa wa
nne na asilimia 13.7
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Mackson
Mbendera amesema uchaguzi huo ulikumbwa na changamoto nyingi lakini
mwishowe nchi ikalazimika kupata kiongozi wake na akawaomba wananchi
kuwa na utulivu .