Mhe. Mama Salma Kikwete, Mlezi wa MEWATA;
Mhe. Kebwe Steven Kebwe (Mb.), Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Mhe Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
Wakuu wa Wilaya – Tabora, Nzega na Urambo;
Wabunge Wote wa Mkoa wa Tabora Mliopo;
Dkt. Serafina Mkuwa, Mwenyekiti wa MEWATA;
Wawakilishi wa Washirika Wetu wa Maendeleo;
Dkt. Joseph Komwihangiro, Mwakilishi wa Marie Stopes;
Madaktari Wote wa MEWATA na Watumishi wa Sekta ya Afya;
Mwakilishi wa Shirika la Marie Stopes na Wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Waliopo;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani na Pongezi
Niruhusuni nianze kwa kuwashukuru Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid (aliyewakilishwa hapa leo na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Stephen Kebwe) na Mwenyekiti wa Chama cha Madakatari Wanawake Tanzania (MEWATA), Dkt. Sarafina Mkuwa kwa kunialika kuja kuzindua huduma za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti Mkoani Tabora. Nawapongeza nyote kwa maandalizi mazuri kwani ni ukweli usiopingika kuwa shughuli hii imefana sana. Aidha, nawashukuru wenyeji wetu wa Mkoa wa Tabora wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Fatma Mwasa, kwa mapokezi mazuri mliyonipatia mimi, mke wangu na wageni wenzetu. Sikutegemea kupata mapokezi tofauti na haya hapa Tabora, kwani upendo wenu kwangu na ukarimu wenu tunaujua na unasifika na wengi.
Madhumuni ya Ziara
Ndugu Wananchi;
Nimekubali kuja kujumuika nanyi katika uzinduzi huu, siku ya leo, ili kuongeza sauti yangu na uzito kuhusu shughuli hii muhimu na adhimu inayofanywa na Madaktari Wanawake hapa nchini. Ni ukweli ulio wazi kuwa MEWATA imesaidia kuokoa maisha ya akinamama wengi nchini ambao, vinginevyo, wangepoteza uhai kwa saratani hizi mbili zinazowapata wanawake. Hatuna budi kuvunja ukimya na kuungana na Madaktari Wanawake kuzungumzia maradhi haya na kuelimishana ili wananchi, wadau na Serikali kwa umoja wetu au mmoja mmoja, tuchukue hatua stahiki za kukabiliana na maradhi haya.
Aidha, ni nafasi nzuri ya kutoa pongezi zangu kwa wanachama wa MEWATA kwa kazi kubwa na nzuri waifanyayo na mafanikio yaliyopatikana. Sijui hali ya maradhi haya ingekuwaje hapa nchini kama Madaktari Wanawake wasingeamua kufanya kazi hii njema wanayoifanya. Kwa niaba ya wanawake na wanaume wote wa Tanzania tafadhali pokeeni pongezi zetu za dhati. Endeleeni kufanya kazi hii njema na Mwenyezi Mungu atawalipa kwa wema wenu na mioyo yenu ya huruma. Nawaahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa hali na mali na kwa kadri ya uwezo utakavyoniruhusu.
Nimefurahi sana kwamba ndugu zetu wa MEWATA wameweza kufika hapa Tabora siku ya leo. Mtakumbuka kuwa nilipokuja kwenye Sherehe za Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi, 2010, niliahidi kwamba nitawaomba MEWATA waje kufanya uchunguzi wa saratani za mlango wa kizazi na matiti kwa akinamama. Hayawi hayawi leo yamekuwa. Nawashukuru sana viongozi na wanachama wa MEWATA kwa kuja kwenu. Mmenitoa kimasomaso. Wahenga walisema: “Ada ya Mja kunena, muungwana na vitendo”. Ndugu zangu wa Tabora ahadi imetimia, kazi kwenu. Jitokezeni kwa wingi kupima muokoe maisha yenu.
Hali ya Magonjwa ya Saratani ya Wanawake Nchini
Ndugu Wananchi,
Tanzania inatambulika kuwa ni moja ya nchi zenye kiwango kikubwa cha maradhi ya saratani ya mlango wa kizazi hapa Afrika ya Mashariki. Inakadiriwa kuwa takriban wanawake 56 katika kila wanawake 100,000 hupata saratani hii. Inakadiriwa pia kuwa zaidi ya watu 35,000 wanapata saratani hii kila mwaka na zaidi ya watu 27,000 hupoteza maisha. Mwaka 2010 peke yake, wanawake wapatao 6,000 waligundulika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi na wanawake 4,000 kati yao walifariki dunia.
Wataalamu wanatuambia kuwa, saratani hii huwapata wanawake wa umri wa miaka 30 na 50. Aidha, wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI wako katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huo kwa asilimia 50. Pamoja na tatizo hili, bado tunayo changamoto ya saratani ya matiti ambayo ni ya pili kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi nchini. Hivyo basi, hapa nchini wanawake wako kwenye hatari kubwa ya kufa kwa saratani kuliko wanaume kwa sababu saratani nyinginezo, hazibagui ukiacha ile ya tezidume inayowapata wanaume pekee.
Hatua za Tahadhari za Kuzingatiwa
Bahati nzuri, saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zinaweza kutibika ikiwa zitagunduliwa mapema. Njia pekee ya kuweza kugundua mapema ni kupima mara kwa mara. Wataalamu wanashauri kuwa ni vyema wanawake wenye umri wa kati ya miaka 30 na 50 wakachunguza afya zao walau mara moja katika kila miaka mitatu. Na, kwa wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanashauriwa kuchunguzwa walau mara moja kwa mwaka.
Bahati mbaya sana, uzoefu umeonyesha kuwa wanawake wengi hufika hospitali wakati ambapo ugonjwa umeshapea na kuenea sehemu nyingine za mwili. Wanakwenda hospitali wakati maradhi yamefikia hatua isiyoweza kutibika na hivyo kupoteza maisha. Hivyo basi, kupima na kugundulika mapema kwa saratani ni hatua muhimu sana ya kuepusha vifo vinavyotokana na maradhi hayo. Bahati nzuri hivi karibuni kumekuwepo na mwamko na mwitikio mzuri wa kujitokeza kwa wanawake wengi kupima saratani ya matiti. Haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na MEWATA. Juhudi hizi zinapaswa kuendelezwa. Zinastahili kuungwa mkono.
Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
Ndugu Wananchi;
Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na saratani ya mlango wa kizazi. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha Programu inayoshughulikia masuala ya Saratani za Uzazi katika Kitengo cha Afya ya Uzazi na Mtoto mwaka 2008. Kupitia programu hii tuna Mpango Mkakati wa Kukinga na Kudhibiti Saratani ya Mlango wa Kizazi (2011-2016). Mwongozo wa kutoa huduma umeandaliwa pamoja na miongozo ya mafunzo kwa watoa huduma na ujumbe wa kuelimisha jamii kupitia njia mbalimbali. Kupitia programu hii tumeweza kuanzisha vituo zaidi ya 130 vinavyotoa huduma ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi katika Mikoa 17 hapa nchini. Ukilinganisha na mwaka 2008 tulipokuwa na vituo vinne tu vilivyokuwa vinatoa huduma hii ya uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na tiba ya mabadiliko ya awali, haya ni maendeleo makubwa.
Ndugu Wananchi,
Kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo MEWATA, Marie Stopes, WAMA na wengineo kutekeleza mpango wa “Utepe wa Pinki na Utepe Mwekundu” yaani “Pink Ribbon Red Ribbon”. Kupitia program hiyo, kampeni ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti ilizinduliwa katika mkoa wa Mwanza mwezi Machi mwaka huu katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Kupitia mpango huo, tumekabidhi mashine 16 za kutolea huduma za matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya mlango wa kizazi (Cryotherapy machine) kwa mikoa ya Mwanza, Mara, Iringa, Njombe na Mbeya. Mipango inaendelea kwa mikoa iliyosalia pamoja na Tabora kupatiwa mashine hizo kuendeleza juhudi za Serikali kupanua upatikanaji wa huduma hizi katika mikoa yote nchini.
Lengo letu katika kufanya hivyo ni kutaka kupunguza mzigo mkubwa unaoielemea Hospitali yetu ya kuu kansa ya Ocean Road. Pia, tunataka kuwapunguzia wanawake adha na gharama ya kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi. Tunatambua umuhimu wa huduma hizi kuwa karibu zaidi na walipo watu ili ziwafikie wanawake wote bila kujali hali zao za kipato.
Ndugu Wananchi;
Katika jitihada za kutokomeza maradhi haya, Serikali, kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo, imeanza kutoa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa Kizazi ya “Human Papilloma Virus (HPV)”. Chanjo hii hutolewa kwa watoto wa kike wenye umri wa miaka 9. Chanjo hii hukinga wasipate maambukizi ya virusi ambavyo husababisha Saratani ya Mlango wa Kizazi. Wizara ya Afya tayari imezindua mpango huo wa utoaji wa chanjo ya HPV kwa wasichana tarehe 29 Aprili, 2014 wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Duniani na mama Salma Kikwete. Mpango huo ulizinduliwa kwa Halmashauri tano za Hai, Siha, Moshi Vijijini, Moshi Mjini na Rombo za Mkoa wa Kilimanjaro, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa azma ya kutoa chanjo hii nchi nzima ifikapo mwaka 2016.
Shukrani kwa Wadau
Ndugu Wananchi;
Napenda kutoa pongezi na shukrani za pekee kwa MEWATA kwa kazi nzuri na kubwa ya kukuza uelewa wa jamii na kuhamasisha uchunguzi wa saratani zinazowapata wanawake. Ni dhahiri kwamba ili jambo hili lifanikiwe lazima liwe na mshika bango wake. Bahati nzuri ndugu zetu wa MEWATA wamejitoa kimasomaso na wamefanya kazi ya Serikali kuwa rahisi. MEWATA imekuwa inafanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya Saratani ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi. Kama nilivyokwisha kusema awali, juhudi hizo zimewafikia wanawake wengi nchini na kuokoa maisha yao.
Aidha, napenda kuchukua fursa hii kutambua na kutoa shukrani maalum kwa Shirika la Marie Stopes na wadau wote ambao wanashirikiana na Serikali katika kupambana na tatizo hili kubwa la Saratani ya Mlango wa Kizazi. Vilevile, tunawashukuru wale wote wanaotoa huduma ya afya ya uzazi na mtoto nchini. Napenda kwa mara nyingine tena kuwahakikishia ushirikiano wa Serikali ya CCM ninayoiongoza kwenu. Ni, dhamira yetu kupunguza na ikiwezekana hata kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na Saratani ya Mlango wa Uzazi na Saratani ya Matiti ambazo kwa kweli zinaweza kuzuilika.
Wito kwa Wananchi
Ndugu Wananchi;
Natoa wito kwa wanawake wa Tabora kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi wa saratani hizi na wataalamu walioko hapa. Napenda kuwatoa hofu kuwa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti siyo magonjwa ya aibu au ya mkosi au uchawi au laana na wala siyo magonjwa yasiyotibika. Magonjwa haya huweza kumpata mwanamke ye yote, awe ameolewa au hajaolewa, awe amezaa au hajazaa, awe tajiri au maskini. Madhali ni mwanamke anaweza kupata. Sharti lake la kupona ni kugundulika mapema na kuanza tiba mapema. Kuchelewa kugundulika na kuchelewa kuanza matibabu ndiko kunakosababisha vifo kutokana na maradhi haya. Waswahili wana msemo usemao, mficha maradhi kifo humuumbua. Hivyo ndugu zangu kina mama nashauri mfanye uchunguzi mapema, ili kama kuna tatizo muanze tiba mapema.
Napenda kutumia fursa hii, kuwaasa akina baba na walezi nao kusaidia katika juhudi za kuzuia na kutibu magonjwa haya ya saratani ya wanawake. Mwanamke anayepata magonjwa haya anahitaji matunzo na upendo siyo masimango na unyanyapaa. Masimango na unyanyapaa huwafanya wanawake waogope kujitokeza kuchunguza afya zao na kupatiwa tiba kwa kuogopa kubaguliwa au kuachwa. Magonjwa haya yanatibika. Si kila mwanamke anayepata saratani hufariki dunia. Kinachotakiwa ni baba na mama kushirikiana kumpeleka mama kufanyiwa uchunguzi na kupata tiba iwapo atagundulika kuwa na maradhi. Saratani siyo ugonjwa wa zinaa, hivyo, msiwanyanyapae akina mama bali muwalee na kuwatunza ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida. Akina baba muwe ndiyo nguzo ya mafanikio katika mapambano dhidi ya saratani.
Na, kwa wanaume wenzangu, tujenge mazoea ya kupima afya zetu hususan kuhusu saratani ya tezidume (prostate). Hii ni saratani inayoua wanaume wengi duniani na hapa nchini. Lakini nayo kama zilivyo saratani za matiti na mlango wa kizazi zinatibika kama zitagundulika mapema. Kila mkienda kupima afya pimeni afya ya tezidume mjue mustakabali wenu.
Ndugu Wananchi;
Sote tukiungana pamoja tunaweza kutokomeza saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti. Nia ya kutokomeza maradhi haya tunayo, sababu ya kutokomeza tunayo na uwezo wa kuyatokomeza tunao. Kinachotakiwa ni kuunganisha nguvu zetu pamoja. Mimi na mke wangu Mama Salma Kikwete tuko nanyi na tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega katika vita hii sasa na hata baada ya kuacha Urais mwakani. Inawezekana, timiza wajibu wako!
Ndugu Wananchi;
Kwa vile niko Tabora ni vyema nikatumia nafasi hii pia, kuyazungumzia baadhi ya mambo niliyoyazungumzia au kuahidi kufanya safari zilizopita. Kwa upande wa barabara, napenda kuwahakikishia kuwa barabara kuu zinazoendelea kujengwa hapa Mkoani Tabora tutazimaliza. Subira yavuta heri. Barabara ya Urambo –Kaliua ujenzi utaanza mwaka huu wa fedha na Chaya – Nyahua, mchakato wa kutafuta fedha unaendelea ili nayo ujenzi wake uweze kuanza kabla ya mimi kumaliza kipindi changu cha uongozi. Kuhusu kupata maji ya Ziwa Victoria, kwa Igunga, Nzega, Tabora, Urambo na Sikonge hatua za awali zimeanza na kinachofuatia ni kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huo mkubwa. Tunakusudia kuiomba Serikali ya India ambayo ndiyo iliyogharamia matayarisho ya mradi. Tuna matumaini ya kufanikiwa. Sote tuzidi kuomba iwe hivyo.
Kwa upande wa tatizo la wakulima wa tumbaku kutokulipwa stahili zao na vyama vya ushirika nimeelezwa na kulielewa. Kuna tuhuma za wizi na ubadhilifu. Nimemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi atume watu wake wa upelelezi wa makosa ya Jinai waje wafanye uchunguzi ili wahusika wakamatwe na kufikishwa Mahakamani na kupewa adhabu zinazostahili. Ameniahidi kuwa keshokutwa Jumatatu watu hao watakuja. Wapeni ushirikiano unaostahili ili tukomeshe uhalifu na dhuluma zinazofanywa na Maofisa wa Vyama vya Ushirika na taasisi za fedha kwa muda mrefu sasa.
Baada ya kusema hayo, naomba nitangaze sasa zoezi hili la uchunguzi wa Saratani ya Mlango wa Kizazi na ya Matiti limefunguliwa rasmi.
Nawashukuruni sana.