POLISI
mkoani Kilimanjaro imefanikiwa kunasa dawa za kulevya zinazodaiwa kuwa
ni Cocaine zenye uzito wa zaidi ya kilo nne, huku mhusika wa dawa hizo
akiwatoroka polisi wa Kitengo cha Dawa za Kulevya Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) katika mazingira tatanishi.
Tukio hilo linatokea wakati dunia leo inaadhimisha siku ya kupiga
vita matumizi ya dawa za kulevya ambayo huadhimishwa Juni 26 kila mwaka
ambapo kitaifa yanafanyika jijini Mbeya yakibeba kaulimbiu ya “Uteja wa
dawa za kulevya unauzulika na kutibika, chukua hatua”.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani hapa,
dawa hizo zikiwa zimefichwa kwa ustadi mkubwa ndani ya mikoba
inayotumiwa na wanawake pamoja na mifuko ya kutunzia faili, zilikamatwa
Juni 23, saa 10 alfajiri, katika Uwanja wa KIA.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa
kwa dawa hizo huku akisema hadi sasa bado hazijafahamika ni aina gani
ingawa uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa ni Cocaine.
“Dawa hizi zilikuwa zimefichwa kwenye mabegi mawili makubwa ambayo
ndani yake kulikuwa na pochi zinazotumiwa na wanawake, mhusika
alionekana kana kwamba anafanya biashara ya mikoba kumbe katikati ya
pochi hizo ndiko alikuwa ameficha,” alisema Boaz.
Alisema mzigo huo ulikamatwa uwanjani hapo ukidaiwa kuwa ni wa abiria
aliyesafiri na ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopian
Airline) iliyokuwa ikitokea Brazil na kupitia katika Uwanja wa Ndege wa
Addis Ababa, Ethiopia, kisha Mombasa na hatimaye kutua KIA.
Alisema abiria huyo ambaye majina yake yamefahamika pamoja na picha
zake, anadaiwa kutelekeza mizigo yake uwanjani hapo na kukimbia mikono
ya polisi huku akiomba kutozungumzia kutoweka kwake pamoja na kutotaja
majina ya mhusika kutokana na sababu za kiupelelezi.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia