Wazazi na walezi wa Wilaya
ya Mbulu Mkoani Manyara, wameupongeza uongozi wa shule ya sekondari Chief
Sarwatt, kwa kufaulisha vizuri wanafunzi 37 wa kidato cha tano, ambao kati yao 33
wamefaulu somo la sayansi.
Wakizungumza na waandishi wa
habari LEO, wazazi hao walidai kuwa uongozi wa shule hiyo chini ya mkuu wao
Tareto Mirisho Ayo, unapaswa kupongezwa kutokana na ufaulu wa kutisha wa
wanafunzi wa shule hiyo.
Pia, walitoa pongezi kwa halmashauri
ya wilaya hiyo kupitia ofisa elimu ya sekondari, Michael Hadu, uongozi wa kata
ya Endagikot na bodi ya shule kwa kusimama kidete hadi kusababisha shule hiyo kufaulisha
kwa kiwango hicho.
Mkazi wa Endagikot John Tluway
alisema kitendo cha wanafunzi hao 37 kufaulu kidato cha tano, kinatakiwa kuigwa
na shule nyingine kwani kimeonyesha kuwa, wasichana wanaweza pindi wakipatiwa
miundominu mizuri kwenye shule zao.
“Huu ni ufaulu unaotisha kwani
wasichana 33 wamefaulu masomo ya sayansi ambayo wanadaiwa kuwa ni magumu kwao
lakini pia tunawapongeza hao wengine wanne walifaulu kwenye masomo ya sanaa,”
alisema Tluway.
Hata hivyo, Richard Salawo
aliutaka uongozi na wanafunzi wa shule hiyo kutobweteka na matokeo hayo bali
waongeze juhudi ili kipindi kijacho wapate matokeo mazuri zaidi kuliko haya
ambayo yametokea kwa mwaka huu.
“Tumeziona juhudi za uongozi wa
shule, walimu, bodi ya shule na wanafunzi kwa kufanikisha ufaulu huu ila
wasivimbe kichwa, mikakati ya ufaulu iongezwe ili shule hiyo izidi kuwa kituo kizuri
cha taaluma,” alisema Salawo.
Alisema miundombinu bora
iliyowekwa shuleni hapo imesaidia hali hiyo ya ufaulu, kwani baada ya mabweni
kujengwa kumesababisha wasichana kulala shuleni na kusoma kwenye mazingira
mazuri, tofauti na awali.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia