NAIBU Meya wa Arusha, Prosper Msofe, amewasilisha mahakamani barua
ya kusaini mkataba kati ya Tanzania na Singapore juu ya uandaaji wa
mpango wa majiji ya Arusha na Mwanza ili kushawishi apate dhamana.
Hayo yalitokea jijini hapa jana mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya
ya Arumeru, Jackson Ndaweka, aliyesikiliza shauri la shambulio la
kudhuru mwili linalomkabili Msofe baada ya wakili wa serikali, Diaz
Makule kutaka mshitakiwa huyo asipewe dhamana.
Msofe aliileza mahakama hiyo kuwa shitaka linalomkabili lina dhamana,
hivyo anaomba apate haki hiyo ili ahudhurie mkutano wa kutiliana saini
kati ya nchi hizo kwa mustakabali wa wakazi wa Arusha.
Aliikabidhi barua hiyo kwa hakimu kama uthibitisho, huku akisisitiza
kwamba mkutano huo utafanyika kwenye ofisi yake na ujumbe wa watu
kutoka Singapore umefika, hivyo asipohudhuria fedha za umma zitapotea.
Wakili Makule alitaka Msofe huyo asipewe dhamana kwa madai kwamba
aliendelea kupiga watu hata baada ya kuwa nje kwa dhamana kwenye kesi
nyingine iliyokuwa mahakamani hapo wiki iliyopita.
Hakimu Ndaweka aliahirisha kwa saa mbili shauri hilo kisha aliamua
kumwachia kwa dhamana Msofe baada ya kuridhika kwamba mashitaka
yanayomkabili yana dhamana.
Msofe anatuhumiwa kumpiga mgambo, Wiliam Molel Aprili 16, 2014 na
siku hiyo hiyo akiwa Ngarenaro, alimpiga tena mgambo Mary Samwel na
kumchania nguo yake.
Shauri limeahirishwa hadi Julai 14, mwaka huu litakapotajwa tena mahakamani hapo.