Kamati ya maendeleo ya
Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeazimia kuanzisha mfuko wa
kusaidia polisi jamii wa kata hiyo kwa lengo la kuwawezesha ili wafanye kazi
zao ipasavyo katika ulinzi shirikishi.
Diwani wa kata ya Mirerani,
Justin Nyari akizungumza mbele ya Mkuu wa kituo cha polisi Mirerani, ASP
Lwitiko Kibanda, alisema wanatarajia kuomba kibali kwa Mkuu wa wilaya hiyo ili
kuchangisha fedha za kutunisha mfuko huo.
“Tunatarajia kuanzisha mfuko huu
baada ya OSC wa Mirerani kuleta wazo hili na sisi tuthamini kazi za polisi
jamii katika kata yetu, kwani wamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi katika
kupambana na uhalifu,” alisema Nyari.
Alisema mfuko wa polisi jamii na
ulinzi shirikishi utawasaidia kuwapa morali ya kufanya kazi kwa juhudi zaidi
tofauti na hivi sasa ambapo hawapati kifuta jasho ili hali wanafanya kazi nzuri
za kusaidia wananchi kwenye suala la ulinzi.
Naye, Mkuu wa kituo cha polisi
Mirerani, Mrakibu Msaidizi wa polisi, Lwitiko Kibanda alitoa shukurani kwa
uongozi wa kata hiyo kujali na kuthamini jitihada za polisi jamii wa eneo hilo,
ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa polisi.
“Tumekuwa tukiwapa mafunzo polisi
jamii zaidi ya 30 hapa kituoni na wamekuwa wakitusaidia katika shughuli za
ulinzi na usalama hapa Mirerani, ila tatizo ni namna ya kuwawezesha kwani sisi
hatuna fungu hilo,” alisema Kibanda.
Alisema dhana ya ulinzi
shirikishi na polisi jamii ilianzishwa na jeshi la polisi baada ya kuona kuwa
watakuwa msaada kwa askari kutokana na idadi ndogo ya polisi waliopo nchini
hivyo watashirikiana nao kuhakikisha usalama unakuwepo