mkurugenzi wa Roling Stone Ally Mtumwa |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limejitosa kuokoa mashindano ya
vijana ukanda wa maziwa makuu ambayo yalikuwa katika hatihati ya
kufanyika na sasa waratibu Rollingstone Sports Academy ya mjini hapa
chini ya mwamvuli wa mtandao wa taasisi za soka la vijana Afrika
Mashariki na Kati (ECAYFA) watayaendesha kwa kushirikiana na shirikisho
hilo.
Mashindano hayo ya wazi, hufanyika kila mwaka mkoani Arusha na mwaka
huu yatafanyika jijini Dar es Salaam mwezi ujao na kushirikisha timu za
vijana chini ya miaka 20 na 14 kutoka Burundi, Rwanda, Kenya, Zanzibar
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza na libeneke la kaskazini blog, Mkurugenzi wa Rollingstone
Football Academy, Ally Mtumwa, alisema mashindano hayo yalikuwa katika
hatihati ya kufanyika, baada ya TFF kuchelewa kutoa kibali cha
kuendesha, kwani taasisi hiyo iliandika barua ya kuomba tangu Februari,
lakini hawakupatiwa kwa wakati.
Mtumwa alisema kutokana na kuchelewa kwa kibali hicho, walishindwa
kufanya maandalizi ikiwa ni pamoja na kutafuta wafadhili na kualika
timu, hususani zile zinazotoka nje ya nchi, hali iliyosababisha
kufikiria kuyasogeza mbele au kutofanyika kabisa.
Aliongeza kuwa baada ya kufuatilia, TFF walikiri kupokea barua hiyo
na kusema sababu zilizochangia kutofanyiwa kazi ni pilikapilika za
kuhama ofisi kupisha ujenzi wa ofisi za Karume.
Alisema lakini kwa kujua umuhimu na ukubwa wa mashindano hayo,
waliamua yafanyike kwa ushirikiano wa pamoja kwa sharti la kufanyika
jijini Dar es Salaam ili waweze kushuhudia.
Hii itakuwa mara ya pili kwa mashindano hayo ya 14 kufanyika nje ya
Arusha, kwani mwaka 2012 yalifanyika nchini Burundi na utakuwa mwanzo
wa kuzunguka katika mikoa na nchi mbalimbali ambazo zitakuwa tayari
kuandaa na kukidhi vigezo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia