Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amesema anaamini kuwa rais ajaye wa
Tanzania, atakuwa ni kijana na kusema kwamba kila zama zina kitabu
chake.
Akizungumza hivi karibuni,
waziri huyo alisema kuwa itakuwa ni kosa iwapo Rais Jakaya Kikwete
atakabidhi kijiti kwa mtu mwenye umri unaofanana naye.
Nyalandu alibainisha kwamba wakati ukifika, atatangaza iwapo atagombea
urais au kuendelea kugombea ubunge katika jimbo lake la Singida
Kaskazini.
“Ukifika wakati ni lazima kubadilishana vijiti. Ni lazima kizazi
kinachomaliza muda wake, kikabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Ni
wazi mtu mwenye umri unaofanana na kiongozi anayeondoka madarakani hana
nafasi,” alisema Nyalandu akiongeza:
“Kijiti hiki anachokiacha Jakaya Kikwete, aliachiwa na kaka yake Rais
Benjamin Mkapa na Mkapa naye aliachiwa kijiti na kaka yake Mzee Ali
Hassan Mwinyi ambaye ndiye alisema kila zama na kitabu chake.”
Alieleza kuwa huo ni uhalisia wa maisha na kwamba ni lazima kila mtu kukubali hivyo.
“Sasa tunahangaika kuandika hitimisho la zama za Rais Kikwete, ndiyo
sisi tunapambana kuhakikisha tunakomesha ujangili na wengine wanafanya
kazi nyingine. Haya yakikamilika ni zama zake (Rais Kikwete),
zimekamilika,” alisema Nyalandu.
Alifafanua: “Rais Kikwete atakabidhi kitabu kwa zama nyingine na sharti
akabidhi kijiti kwa kizazi kinachofuata. Haitawezekana ikiwa atakabidhi
kijiti kwa kizazi chake hichohicho. Ni kosa kurudia zama zilizopita.”
Nyalandu alisema kuwa ni vyema mtu yeyote mwenye umri unaofanana na
kiongozi anayeondoka madarakani akasahau kupewa kijiti kwani historia na
hata maandiko ya Mungu vipo tofauti.
Makundi ya urais
Akizungumzia taarifa za kutakiwa na makundi ya waliojitangaza kugombea
urais ili awaunge mkono na yeye asubiri kupewa uwaziri mkuu, Nyalandu
alisema taarifa hizo siyo sahihi.
“Hakuna kiongozi anayechaguliwa na mtu mmoja. Sisi sote ni viongozi na
hakika hakuna anayependa tuwe viongozi, bali ni Mwenyezi Mungu tu. Kwa
mfano, mimi najiona mwenye bahati tu, kwani kabla ya kuwa waziri,
nilikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na kulitokea matatizo,
wenzangu waliondoka. Baadaye, nilikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, pia wenzangu kama saba waliondoka na nikapanda hadi nilipo sasa.
Haya ni mapenzi ya Mungu…”
Hata hivyo, Nyalandu ambaye amekuwa akitajwa kuwa na nia ya kugombea
urais alisema bado wakati mwafaka haujafika kutangaza nia yake.
“Mimi kama kiongozi wa kitaifa, kama waziri na mjumbe wa Halmashauri Kuu
ya CCM, naweza kukuhakikishia kama nitagombea lakini hili ni jambo
linalokwenda na wakati. Wakati ukifika nitafanya uamuzi mgumu kuwa
nitagombea au la. Kugombea ni uamuzi mgumu na kutogombea ni uamuzi mgumu
pia,” alisema.
Alisema kwamba mtu anayetangaza kugombea urais au anayekaa kimya, ajue
kuwa Watanzania huwapima watu kwa matendo yao wanayofanya.
“Kupimwa tunapimwa, mtu ambaye hajatangaza nia siyo kama hapimwi, watu
wanatupima tu. Tunaishi vipi na watu, je, familia yako ipo vipi, je
jimboni wanakuonaje, umesaidia maisha ya watu au unapandisha mabega
baada ya uwaziri au unashirikiana na wananchi vizuri? Kiongozi anapimwa
na vitu vingi,” alisema na kuongeza:
“Mwanasiasa akiwa ametangaza nia au hajatangaza ajue yupo katika vipimo.
Kinachopimwa siyo maneno ni kazi tunazofanya. Kama kiongozi, sote
tutapimwa hata kama ulitangaza nia tangu mwaka 2010.”
Rais ajaye atatoka CCM lakini…
Kuhusu nafasi ya CCM kutoa rais ajaye, Waziri Nyalandu alisema: Kama taa
ikikuangazia na Watanzania wakasema sisi tunakutaka wewe kupitia chama
chao, basi utakuwa kiongozi wao.”
Nyalandu alisema kuwa anaamini rais ajaye atatoka CCM, lakini
akatahadharisha kwamba lazima chama hicho kihakikishe kinatimiza wajibu
wake kwa kumpitisha mgombea wake kikizingatia misingi ya uwazi na
ushirikishwaji.
“CCM inapaswa kuhakikisha rais ajaye atatokana na mapenzi ya wanachama walio wengi ili iwe rahisi kumnadi,” alisema.
Alifafanua kuwa ni muhimu ijulikane kwamba hakuna mtu yeyote aliye na
hatimiliki ya siasa za Tanzania na hakuna mtu ambaye familia yake ina
hakimiliki ndani ya CCM.
“Ijulikane, Mtanzania yeyote ana haki ya kuchukua fomu na kugombea kama
lengo lake ni kuwasaidia Watanzania. Mtu ambaye ana nia ya kuendeleza
kazi anayomalizia Rais Kikwete. Lazima apokee mtu ambaye atajenga kwenda
juu na siyo kubomoa,”alisema.
Kuhusu tuhuma juu yake
Akizungumzia tuhuma zinazoelekezwa kwake, Nyalandu alisema ni za
kupangwa na za uongo, huku akitolea mfano wa tuhuma za kudaiwa kutaka
kuuza Hifadhi ya Katavi na kuruhusu wanyama 700 kuwindwa bure.
“Huu ni uongo, hivi kama ni waziri anataka kuuza Hifadhi ya Taifa, kweli
angemaliza hata saa mbili bila ya kufukuzwa na rais?” anahoji Nyalandu .
Alisema tuhuma nyingi dhidi yake zinatokana na msimamo wake katika vita
dhidi ya ujangili nchini na kwamba kuna watu ndani ya Serikali na idara
mbalimbali walikuwa wakihusika na matukio ya ujangili na sasa
wanajitahidi kumchafua.
“Na hapa ieleweke kuwa tunawafahamu watu wote waliopo katika mtandao
huu, ujumbe wanaotumiana na simu wanazopigiana, wakati ukifika
tutawakamata mmoja baada ya mwingine, kwani tayari maofisa wengi
wizarani tumewaondoa na wengine kuwabadilisha idara,” anasema.
Mgogoro kati yake na Katibu Mkuu
Kwa muda mrefu, Waziri Nyalandu, anatajwa kuwa na uhusiano mbaya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, Nyalandu alisema kuwa taarifa nyingi zinazoelezwa siyo
sahihi na kwamba yeye ni kiongozi wa wizara na kila mtu ana wajibu wake.
“Mengi yanasemwa sisi hatuelewani, lakini ukweli ni kuwa kila mtu
anafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria na hatuna msuguano
wowote,” alisema.
Akizungumzia uamuzi wa kuhamishwa watendaji kadhaa katika wizara hiyo,
Nyalandu alisema suala hilo halimaanishi kuna mgogoro, kwani
waliohamishwa wapo ambao tayari wameripoti vituo vyao vya kazi.
“Kama nilivyosema awali kuna mambo mengi yanaendelea pale wizarani na
kuna watu wanatoa taarifa potofu kwenye vyombo vya habari, kwa kuchomoa
madokezo tu ya mambo na kufanya yametendeka, lakini tutahakikisha
tunakomesha mambo haya,” alisema.
Safari za nje na kufanya kazi nje ya ofisi
Akizungumzia tuhuma za kufanya safari nyingi za nje ya nchi na kuhamisha
ofisi yake kutoka wizarani na kuipeleka hotelini, Nyalandu alisema
tuhuma hizo hazina ukweli.
“Mimi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, ofisi yake ni mapori yote ya
akiba yenye ukubwa wa kilomita za mraba 200,000. Ofisi yangu ni kutafuta
watalii na kufikia Machi mwakani utalii ndiyo unatarajiwa kuongoza
katika kuchangia pato la taifa, sasa unaposema sikai ofisini sijui ofisi
ipi?” anahoji.
Hata hivyo, alisema kuwa uamuzi wa kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori,
aliutangaza akiwa wizarani na hilo ni kati ya mambo makubwa aliyofanya
ili kunusuru rasilimali za taifa kuendelea kupotea.
“Katika mpango huu wafanyakazi wengi ajira zao zitakoma na watakuwa
chini ya mamlaka yenye bodi yake ambayo inaongozwa na wananchi na hapo
tutaweza kuratibu vyema mapori ya akiba na maeneo mengine ya hifadhi za
wanyama,” alisema.
Ujangili umenisababishia vita
Kuhusu ujangili, Waziri Nyalandu alisema mapambano dhidi ya ujangili nchini yamemsababishia vita kubwa.
Alisema wizara hiyo ina rasilimali nyingi na kwamba kuna watu walizoea njia za mikato.
Matatizo ya wanyamapori yaani tembo na faru kuuawa yanatokana na uchu wa
watu wachache na hasa wenye mamlaka ambao walitumia nafasi zao kwa
namna moja ama nyingine.
Anafafanua kuwa watu hao walifanya vitendo hivyo kwa kutofanya kazi
ipasavyo ama kufumbia macho vitendo hivyo ama kushirikiana na majangili.
“Vitendo hivi vilifanya ujangili kufikia mahali ambapo haiwezekani tena
kudhibitiwa. Hadi kufikia mwaka 2013 tembo walikuwa wanakwisha kabisa
kutokana na ujangili,” alisema,
“Ukipita katika kila pori unakutana na mizoga ya tembo ambayo meno yao
yamechukuliwa. Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la
Cites tembo wapatao 10,000 walikuwa wanauawa kwa mwaka. Idadi hii
ilifikia mahali ambapo imekuwa ni janga kuu la kitaifa,” alisema na
kuongeza:
“Nilipoteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii mwezi Februari mwaka
huu, moja ya maagizo ambayo Rais alinipa ni kuhakikisha kuwa hali hiyo
tunaisimamisha mara moja.”
Alisema walianzisha Operesheni Tokomeza kwa ajili ya kukomesha matatizo
hayo lakini kwa bahati mbaya operesheni hiyo haikwenda vizuri kutokana
na shutuma mbalimbali za uvunjifu wa haki za binadamu.
“Kama mnakumbuka Rais pia aliunda tume kuchunguza nani alihusika, nani
alifanya nini, ili kuhakikisha kuwa tunaposimamia haki, ni muhimu
kuonekana inatendeka. Kwa kuwa hatuwezi kusimamia sheria za nchi
tukavunja haki za msingi za wananchi,” alisema.
Hatua zilizochukuliwa
Nyalandu alisema majangili yalitawala kutokana na askari wanyamapori kutokuwa na fedha, silaha na pia kutokana na kuwa wachache.
Alisema maaskari wanyamapori walikuwa na magobori wakati majangili walikuwa na silaha kali.
“Lakini kulikuwa na silaha aina ya AK-47 zipatazo 500, kulikuwa na
ubishi kati ya wizara na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na kwa muda wa
miaka miwili ambayo silaha zilikuwa bandarini, majangili yalikuwa
yakitandika wanyama porini kila asubuhi na usiku,”alisema.
“Katika saa 24 tu tangu nilipoteuliwa niliamua kutoa Sh250 milioni kulipia hizo silaha na zikaingia katika mapori,” alisema.
Alisema hadi kufikia Julai mwaka huu alikuwa ameajiri wafanyakazi
wengine wa wanyamapori 430 ambao wengi wamepelekwa katika maeneo ya
Selous.
Pia alisema wameongeza idadi ya vijana wanaojitolea ambao wamemaliza mafunzo lakini hawajapata ajira.
“Na hawa tumewapeleka kwa mamia katika mapori tumewapa silaha na magari,” alisema.
Nyalandu alisema lazima ijulikane kuwa kiini cha ujangili kipo katika namna gani unawapa motisha wafanyakazi.
“Fedha zile zilikuwa hadi zifike kwa katibu mkuu, waziri, ndiyo ziende
kunakohusika, nikasema ninataka fedha ziidhinishwe moja kwa moja na
wakuu wa idara kwa hiyo nikakata ukiritimba na urasimu. Vijana hawa
wakaanza kupata fedha hata kama wanapata kidogo lakini wanapata kwa
wakati.”
Alisema hatua hizo ziliongeza morali kwa wafanyakazi.
Meno ya tembo yalindwa na UN
“Nilijiuliza kwa nini meno ya tembo ambayo tuliyakamata yalikuwa ni ya
zamani? Kwa nini siyo mapya? Ukiambiwa tani za meno ya tembo zimekamatwa
Zanzibar, Dar es Salaam zote zilikuwa ni za zamani.”
Aligundua kuwa kuna mchezo ulikuwa ukichezwa ndani ya ghala la meno ya tembo.
“Na hiyo ilikuwa inachangia ujangili kwa sababu watafanya watu wao
waende wakafanye ujangili wa meno ya tembo ili walijalizie (ghala).
Niliagiza kuwa kuanzia sasa meno ya tembo tutayalinda kwa pamoja
nikawaita Umoja wa Mataifa, serikali za Uingereza na Tanzania ili
tujadili kwa pamoja jinsi tutakavyoyalinda,”alisema.
Aliagiza kuwa kila jino la tembo lifanyiwe DNA ili ijulikane linatokana na tembo wa mwaka gani, alikufa wapi.
Alisema hatua hizo zimemletea upinzani mkubwa.
Hata hivyo, alisema baada ya kubadilisha watu waliokuwa wakilinda ghala
na kulinda kwa ushirikiano, meno ya tembo yameongezeka kutoka tani
100,000 hadi 130,0000.
“Ni hatua ambayo imeniletea vita vikubwa sana lakini ni hatua ambayo
imeponya tembo wengi sana. Ni hatua ambayo imewabania ulaji watu wengi
sana. Lakini ukiwa kama Waziri wa Maliasili na Utalii, inakupunguzia
sana marafiki,” alisema Nyalandu.
Idadi ya vibali yapunguzwa
Alisema ukichukua DVD ambayo iliwasilishwa na Mbunge wa Iringa Mjini,
Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ilikuwa ikionyesha idadi kubwa ya
wanyama wakiuawa.
“Niliwaondelea vibali na hatua hii ilisaidia sana kuleta woga kwa makampuni ya uwindaji,”alisema.
Alisema pia waliwafundisha kanuni za uwindaji ili wawe wawindaji mahiri.
Alisema pia wamepunguza vibali vya uwindaji kwa mwaka kutoka 200 hadi 100.
“Nimepiga marufuku uwindaji wa tembo vijana na watoto sasa ni tembo wazee tu wanaweza kuwindwa,” alisema.
Akizungumzia hali ya ujangili nchini, Waziri Nyalandu alisema wizara
yake kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali na wananchi wema,
wanaendelea kudhibiti ujangili, kwani idadi ya tembo inaongezeka na
watuhumiwa wanakamatwa.
Pia alisema hivi sasa wananchi wamekuwa wakishirikiana na serikali kutoa
taarifa za ujangili na wizara imeongeza motisha kwa askari wa
wanyamapori.
Aidha Waziri Nyalandu aliwasifu wanahabari kuwa wamefanyakazi kubwa
kuzungumzia ujangili na sasa jambo hili linapigwa vita kila kona,”
anasema.
Alisema katika kuhakikisha ulinzi unaimarishwa, askari zaidi ya 400
wamepewa kazi ya ulinzi wa wanyamapori katika mapori mbalimbali na
wengine bado wanaendelea na mafunzo.
Tume ya oporesheni tokomeza
Akizungumzia Tume ya Rais ya kuchunguza athari za Operesheni Tokomeza,
Nyalandu alisema inaendelea na kazi na wote ambao watatajwa na tume hiyo
bila kujali nafasi zao watashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na
taratibu.
“Tutahakikisha haturudii makosa yaliyofanyika katika operesheni
iliyofanyika na tumekubaliana kufuata kanuni na taratibu katika utendaji
wetu,” alisema.
Kuna watendaji serikalini wanahusika na ujangili
Akizungumzia tuhuma za baadhi ya watendaji ndani ya serikali na vyama
vya siasa kuhusika na ujangili, alisema tuhuma hizo zinafanyiwa kazi na
baadhi wamechukuliwa hatua.
Waziri Nyalandu alisema ni kweli kuwa sehemu kubwa ya meno ya tembo
yaliyokuwa yanakamatwa nje yalikuwa ni ya muda mrefu, hivyo kulikuwa na
uwezekano wa kuibiwa kutoka katika ghala maalum la kuhifadhi memo hayo.
“Tanzania inaongoza kwa kuwa na meno ya tembo mengi katika ghala la
taifa na sasa yapo tani 130,000 ambapo thamani yake ni zaidi ya dola
milioni 60,” alisema.
Kadhalika Waziri Nyalandu alisema: “Kuna watu walinipinga ndani ya
serikali, lakini sasa tumekubaliana kuwa askari wetu watashirikiana na
vyombo vingine kulinda meno haya ili kuhakikisha yanakuwa salama na
dunia inajua yapo salama,” anasema.
Mamlaka ya wanyamapori suluhu ya ujangili
Waziri Nyalandu alisema kuanzisha mamlaka ya wanyamapori anaamini ndiyo
suluhu ya vitendo vya ujangili kwani, chombo hicho kitakuwa na uwezo
mkubwa wa kulinda wanyamapori hapa nchini.
“Tutahamisha wafanyakazi wengi kwenda katika mamlaka hii, ambayo makao
makuu yatakuwa Morogoro na tutaongeza usimamizi wa mapori ya akiba,
askari wengi wataajiriwa wakiwa na silaha za kisasa,” alisema.
Alisema mamlaka hiyo, pia inaungwa mkono na wahisani mbalimbali, ambao
wamekubali kuisaidia serikali ya Tanzania katika vita dhidi ya ujangili.
“Tutakuwa na helikopta za kutosha, ndege na vifaa vingine pia kuna fedha
nyingi tumepata katika kuiwezesha mamlaka hii kukabiliana na ujangili.”
Nimejifunza mengi kwa walionitangulia
Waziri Nyalandu, ambaye ameshika wizara hiyo, ambayo imekuwa kaa la moto
kwa mawaziri wengi waliomtangulia kutokana na kuondolewa alisema kuwa,
kuna mambo mengi mazuri yaliyofanywa na mawaziri waliomtangulia.
“Serikalini tunafanyakazi kwa pamoja, hivyo maamuzi ya mawaziri waliotangulia huwezi kupingana nayo yote.”
Hata hivyo, alisema kuna changamoto zilizosababisha wao kuondolewa
katika wizara naye amekuwa akikabiliana nazo na Mungu anamsaidia
anaendelea kuzishinda.
Kuhusu Jimbo lake
Waziri huyo alisema jimbo lake kwa sasa ndiyo wazalishaji wakubwa wa
chakula katika Mkoa wa Singida kutokana na kuzalisha chakula kingi cha
ziada na mazao mengi ya biashara ikiwamo vitunguu vinavyouzwa ndani na
nje ya nchi.
Waziri Nyalandu amekuwa mbunge wa jimbo la Singida Kaskazini kwa miaka 14 sasa.
Mwananchi