Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Kungulu Kasongi (aliyevaa shati jeupe) akiwaelezea wachimbaji wadogo namna uchorongaji wa miamba.
WADAU wa
ununuzi wa madini ya kati (TASGEDO), na wale wa vyama vya wachimbaji
nchini (REMAS) wamepinga hatua ya serikali kupandisha mara dufu gharama
ya leseni za utafiti na uchimbaji na leseni za ununuzi wa madini ya Vito
na Almasi nchini.
Wakizungumza
jana na waandishi wa habari mjini Arusha , wadau hao wamesema ongezeko
hilo la ada litaleta athari kiuchumi, kwani wanunuzi wakubwa na wadogo
wa madini watashindwa kumudu gharama hizo, hasa ikizingatiwa wengi wao
hawana mitaji mikubwa ya biashara.
Wamesema
hatua ya Serikali kupandisha maradufu viwango vya gharama za leseni
mbalimbali haukuzingatia au kufikiria kwamba, wachimbaji na
wafanyabiashara wa vito na almasi hawana uwezo wa kuchangia pato la
taifa, kwani hawana mitaji mikubwa.
Mwenyekiti
wa TASGEDO nchini, Khamis Rioba, amesema hatua hiyo ya serikali
kutowashirikisha wadau inalenga kuweka mazingira magumu na kufanya
washindwe kuendelea na shughuli zao za uchimbaji na ununuzi wa madini na
kwamba kwa namna moja ama nyingine imewafuta wazawa kwenye sekta hiyo.
Amesema
madini ni rasilimali na hazina ya Taifa inayopaswa kuheshimiwa, hivyo
ameishauri serikali kupunguza ama kurekebisha viwango hivyo na kuweka
viwango stahiki vitakavyowezesha wazawa kumudu pasipo shaka.
Naye Katibu
wa Chama cha wachimbaji madini Arusha “AREMA” Isaya Letema ameishauri
serikali kuwa wiwango vya leseni za viwanja viwe kwa makampuni makubwa
ya wawekezaji toka nje ya uchimbaji na uzalishaji wa madini kwani wana
mitaji mikubwa ya uchimbaji na uzalishaji madini hapa nchini.
Amesema hivi
karibuni serikali ilipandisha leseni ya utafiti wa madini kwa kila
kiwanja kutoka shilingi 80,000 na shilingi 160,000 hadi kufikia shilingi
320,000 na shilingi 800,000 gharama za leseni ya wanunuzi wakubwa wa
madini ya vito kutoka shilingi 250,000 hadi shilingi milioni 1.6 kwa
mwaka.
Aidha maombi
ya ada ya leseni hiyo ilikuwa ikitozwa shilingi 50,000 nayo imepanda na
kufikia shilingi 320,000 kwa madini ya vito, pia maombi ya ufungaji wa
madini kwenda nje ya nchi yaliyokuwa yanatozwa shilingi 50,000 nayo
yamepanda hadi kutikia shilingi 320,000.
Sambamba na
ada hizo za madini ya almasi yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini
nayo yamepanda kutoka sh. Milioni moja hadi sh. Milioni 1.2 wakati
leseni za wanunuzi wa madini wa kati maarufu kama ‘mabroka’ nazo
zimepanda kutoka sh. 115,500 hadi sh. 250,000.