Ticker

6/recent/ticker-posts

KISUVITA YAPATA YAMPA TUZO MWENYEKITI WA CCM AMBAYE PIA NI RAIS WA TANZANIA

 


UONGOZI  wa kituo cha sanaa na utamaduni cha viziwi Tanzania (KISUVITA) umempa tuzo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katika kuhakikisha haki na usawa wa fursa kwa watu wenye ulemavu nchini.

Tuzo hiyo imewasilishwa na kupokelewa na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka  jana ofisi ndogo za CCM Lumumba, Dar es Salaam kwa niaba ya Rais Samia.

Akizungumza wakati wa Makabidhiano  hayo,Katibu Mtendaji wa kituo hicho  Habibu Mborobe alisema wanampongeza  Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri unaowashirikisha, kuwajumuisha na kuwathamini watu wenye ulemavu. 

"Kwanza tunamshukuru kwa kuwezesha Safari yetu ya kwenda kushiriki mashindano ya kidunia ya mitindo na urembo nchini Urusi ambako tulifanikiwa kushika nafasi ya kwanza,ushindi huo umetupa heshima ya kuwa waandaaji na wenyeji wa mashindano kama hayo kwa kanda hii ya Afrika yatakayoanza kuanzia Septemba 29  hadi   Oktoba 2, 2021.

Alisema wanamshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa serikali anayoiongoza kutoa fursa ya mikopo isiyo na riba itokanayo na asilimia 2 ya mapato ya ndani ya halmashauri ambayo wao wenye ulemavu wananufaika nayo."Tunamshukuru Rais wetu Samia  kwa kuendelea kuhakikisha vyombo mbalimbali vya habari kuwa na wataalam wa lugha za alama ili nasi tuweze kupata haki yetu ya kupata habari,"alisema Mborobe.

Mbali na pongezi hizo,Mborobe aliiomba CCM kuingilia kati  kwa kupata udhamini kwa mashindano mbalimbali wanayoandaa au kushiriki kwani wao hawana tofauti na watu wenye kusikia katika kutumia bidhaa zote zinazozalishwa na makampuni hayo.

Akizungumza na ujumbe huo Shaka alisema CCM kupitia katiba yake ibara ya 4 (1)&(2) pamoja na ilani yake ya uchaguzi ibara ya 95 imeeleza wazi kuwa binadamu wote ni sawa hivyo wanastahili kuheshimiwa utu wao bila kubaguliwa kwa rangi, jinsia au maumbile yao.

Hivyo CCM itahakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa, wanaheshimiwa, wanathaminiwa na wanajumuishwa katika mipango na programu mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu na serikali.

Aidha alisema  katiba ya Tanzania Ibara ya 12 inawalinda watu wenye ulemavu hivyo serikali itaendelea kuchukua hatua kadhaa za kuhakikisha misingi madhubuti inawekwa katika kupanga na kutekeleza programu za maendeleo zinazolenga kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu ikiwemo kufahamu takwimu za kundi hili muhimu. 

Aidha alisema  bajeti ya serikali ya mwaka 2021/22 imetenga takribani bilioni 1.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa visaidizi kwa watu wenye ulemavu kwenye shule zote nchini kwani serikali imeendelea kuhimiza wataalam wa lugha za alama kuwepo kwenye kila tukio ambalo umma unafuatulia ili kuwapa haki watu wenye ulemavu ya uziwi kupata habari.

Alisema  CCM itaendelea kutoa msukumo kwa serikali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanaonufaika na mikopo isiyo na riba itokanayo na asilimia 2 za halmashauri bila vikwazo vyovyote.

"Katika kujenga jamii yenye usawa na fursa kwa wote CCM itaendelea kutoa rai na msukumo kwa serikali na sekta binafsi kutambua kuwa watu wenye ulemavu wanayo ndoto na malengo makubwa hivyo wakishirikishwa, wakijumuishwa na wakiungwa mkono kwa kuwekewa mazingira mazuri na wezeshi wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa,"alisema.

Shaka amewashukuru KISUVITA kwa kumpa tuzo Rais Samia ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake kwa watu wenye ulemavu nchini.

Post a Comment

0 Comments