Ukatili juu ya wanawake
Tanzania inabaki kuwa changamoto kubwa na kizuizi cha usawa wa kijinsia na
uwezeshaji wa wanawake. Asilimia 40% ya wanawake wenye miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili
wa kimwili Kwa mwaka 2015-2016.
Kiwango
cha ukatili wa kijinsia katika sekta ya uchimbaji madini ni kubwa na hasa
katika unyanyasaji wa kingono na kihisia, hata hivyo takwimu
zilizokusanywa na taasisi ya CSP Foundation Disemba 2022 kwa wanawake
120 kutoka katika kata tatu ambazo ni Naisinyai, Endiamtu na Mererani
zilionyesha kuwa asilimia 90% ya wanawake waishio Mererani walisema kuwa hawapo
katika mazingira salama katika kufanya biashara kwenye eneo la
uchimbaji madini aina ya Tanzanite.
MWANAMKE MCHINBAJI ALONGA
Pili Hussen, mwanamke wa
kwanza kumiliki mgodi katika mji wa Mererani na kuingia ndani ya migodi iliopo Simanjiro
mkoani Manyara, mwanamke huyu anaeleza kupitia vikwazo vingi hadi kufikia hapa
alipo kwani alidiriki kubadili jina na kujiita Mjomba Hussen na akadiriki kuvaa
kaptula na kutembea na panga ili asinyanyaswe na wanaume.
"Kwanza nilikuja Mererani
mwaka 1978 mwezi wa nne, nilipofika kipindi hicho hakukuwa na wanawake wengi
lakini Mimi nilijitosa kuja kufanya kazi ya uchimbaji na wanaume na wakati
nakuja niliambiwa kabisa kama nakuja Mererani sitatoboa, kwa sababu wanawake
walikuwa wananyogwa lakini Mimi niliigiza kama mwanaume lakini sio mwanaume."
Alisema Pili
Pili aliongeza kwa kusema
kuwa, Mafanikio aliyoyapata alianza kupata pesa mara baada ya kusota Kwa muda
mrefu, hela yake ya kwanza aliitumia kwa kuwajengea wazazi wake nyumba Singida
na kuwanunulia nyumba lakini pia aliweza kusomesha watoto wake na wajukuu. Ujasiri
alioupata ni baada ya kuona wanawake wengine wanaendesha magari na ni matajiri
na kumfanya kupambana zaidi ndio katika kazi ya uchimbaji madini na kupata
faida na mafanikio na malengo yake ya kuwa tajiri ameyafikia.
DHANA YA UKATILI WA
KIJINSIA
Ukatili ni hali ya kusababisha
kwa makusudi mateso na kukosesha raha dhidi ya mtu mwingine kimwili,
kisaikolojia au kiuchumi.
UKATILI WA KIJINSIA NI
NINI?
Ni unyanyasaji na
ukiukwaji wa haki za binadamu ambao unaleta madhara kwa mtu Mmoja Mmoja, jamii
na hata taasisi. Ukatili huo hufanywa kwa mtu mwanamke au mwanaume na mara
nyingi hufanywa na mtu mwenye nguvu kiuchumi, kisiasa au kimwili.
AINA ZA UKATILI WA
KIJINSIA
Zipo aina mbalimbali za
ukatili wa kijinsia, ukianza na ukatili wa kimwili; mfano ikiwa ni kupiga,
kuchoma moto na matumizi ya silaha.
-Ukatili wa kisaikolojia;
mfano, kufedheheshwa, kutegwa,kuaibishwa, kuzuiliwa kupata taarifa na kutukanwa.
-Ukatili wa kiuchumi; hii
ni pamoja na kunyimwa haki ya kumiliki urithi, kunyimwa kumiliki ardhi na
rasilimali zingine.
-Ukatili wa kingono;
mfano ubakaji, ulawiti, jaribio la ubakaji, ukahaba wa kulazimishwa na ubakaji
wa ndoa.
ATHARI ZA UKATILI
Kuna athari mbalimbali za
ukatili ikiwemo ulemavu, kifo, magonjwa na kuambukizwa, sonona pamoja na
kushidwa kujihusisha na shughuli za kiuchumi.
Mgodi wa Mererani ni eneo
pekee duniani ambalo madini ya Tanzanite huchimbwa kwa zaidi ya miaka
50 ambapo wanawake wengi wamejiajiri katika
shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kuuza maziwa, kupika chakula, kuuza
matunda, kuchekecha udongo, kuuza nguo na viatu, kununua na kuuza madini ya
Tanzanite pamoja na kutoa huduma mbalimbali.
Kwa mujibu wa
dodoso la awali lililofanywa na taasisi ya CSP Foundation Disemba 2022 Mererani
inaeleza kwamba asilimia 50% tu ya wanawake wafanyabiashara ndogondogo
ndio wana maeneo ya kufanya biashara zao na baada ya ujenzi wa ukuta wa Mererani 65%
ya wanawake wameacha kufanya shughuli za kibiashara ndani ya mgodi ya Mererani kutokana
na gharama za uendeshaji na dodoso hilo lilihusu jumla ya wanawake 120
kutoka katika eneo la Endiamtu, Naisinya na Mererani.
CHANGAMOTO GANI
ZINAWAKUMBA WANAWAKE WANAOFANYA BIASHARA NDANI YA MIGODI YA MERERANI
Mwanaidi Kimu, Mwanamke
anaefanya shughuli zake ndani ya mgodi wa Mererani alieleza baadhi ya
changamoto ambazo zinawakumba wanapokuwa katika migodi hiyo kuwa ni pamoja
na tozo ya shilingi 1000/= kila siku kwa wafanyabiashara wadogo ndani ya
eneo la machimbo.
Gharama za usafiri ndani
ya mgodi wa Mererani, nauli ya kwenda na kurudi ikiwa ni jumla ya Shilingi 4000.
Kutoruhusiwa kurudisha nyumbani baadhi ya bidhaa za biashara zinapokosa
soko au kubaki mfano maziwa, chakula na matunda, kukosa mitaji, ukosefu wa vyoo
na ubovu wa miundombinu ya barabara.
UKATILI GANI WANAWAKE
WANAOFANYIWA KWENYE MGODI WA MERERANI?
Baadhi ya ukatili ambao
wanawake wanaofanya biashara katika mgodi wa Mererani ni pamoja na kukosa haki
ya huduma staha ndani ya migodi, mfano, ukosefu wa vyoo vya kutosha.
Kuvuliwa nguo kwa lengo
la kukagua madini ya Tanzanite kwenye sehemu mbalimbali za mwili wa
mwanamke, Lugha za matusi zinazotumiwa na wanaume dhidi ya wanawake na kuombwa
rushwa ya ngono.
MAPENDEKEZO GANI
WAMEPENDEKEZA ILI KUTATUA CHANGAMOTO HIZO
Wanawake katika migodi
hiyo wameiomba serikali kuwapatia mashine za Kisasa kwa ajili ya kufanya
ukaguzi, kujengewa vyoo vya umma na vyenye kukidhi mahitaji, kuanzishwa kwa
dawati la jinsia ndani ya mgodi wa Mererani.
Kutolewa
elimu ya ukatili wa kijinsia na msaada wa kisheria, kuanzishwa kwa
simu ya bure ya kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia katika eneo hilo, kuboreshwa
kwa miundombinu ya barabara na vyoo ili kupunguza
gharama za uendeshaji wa biashara kwa wajasiriamali wadogo.
Kupunguzwa kwa ushuru kwa
wajasiriamali wadogo wanaouza maziwa, mboga na matunda kulingana na mitaji
yao, kuwepo kwa kituo cha uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi kama vile mikopo,
utengenezwaji wa kituo cha afya.
TAASISI ILIYOFANYA
TAFITI YATOA NENO
Mkurugenzi wa taasisi ya Civil
Social Protection Foundation (CSP), Nemency Iriya, alisema kuwa kwa sasa
wanatekeleza mradi wa mwanamke na uchumi imara wa Tanzanite ambapo
kupitia mradi huo ndio ulipelekea kufanywa kwa utafiti huo, lengo
likiwa ni kuboresha mazingira ya biashara kwa akina mama
kuzunguka nje na ndani ya machimbo ya madini katika mji mdogo wa Mererani.
“Katika tafiti hizo
tuligundua kwamba kuna vitendo vingi vya ukiukwaji wa haki za kibinadamu haswa kwa
kina mama vitendo vya ukatili wa kijinsia vinatokea kutokana na mazingira ya
ufanywaji kazi na biashara ndani na nje ya mgodi na ndio maana tukasena kwakuwa
tuna wasaidizi wa kisheria tuone namna tutakavyopata vitu vitakavyosaidia kutoa
msaada.” Alisema Mkurugenzi.
Mkurugenzi Iriya
aliongeza kwa kusema kuwa watawawezesha akina mama waweze kupata ujuzi na kuwa
majasiri zaidi na pia kuwaunganisha na Taasisi za fedha ili waweze kupata
mikopo itakayowasaidia kuinua biashara zao.
MKUU WA WILAYA
AFUNGUKA
Kwa upande wa Mkuu
wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dkt. Suleiman Serera alisema kuwa
mama akifanya mambo yake vizuri hadi kina baba wananufaika na kuwa waache
kulalamika uwepo wa mfume dume.
"Niwatake tu
akina mama kuendelea kufanya shughuli zao huku Serikali ikiyatafutia ufumbuzi
matatizo yenu. Serikali inaweka miundombinu na niwaambie tu wanitumie
katika kipindi hiKI nilichopo, wakinitumia na kuweza kushirikiana nasi tutaweza
kuvuka zaid. Kama kuna changamoto tukiambiana ina maana ndio kazi baina ya serikali
na wananchi, inaweza kufanya shughuli kwa pamoja na kwa kufanya hivyo
itapunguza hali ya umaskini sababu watu tupo zaidi ya milioni 64 hivyo tunahitajika
kufanya juhudi za pamoja kuhakikisha tunatengeneza ajira" Aliongeza Mkuu
wa Wilaya.
Kwa upande wake Afisa Madini
mkazi (RMO), Menard Msengi, alisema kuwa utaratibu uliopo wa ukaguzi ni
kwa ajili ya usalama Kwa watu ambao sio waaminifu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia