Ugonjwa
wa Saratani hapa nchini Tanzania umeendelea kuwa tatizo linaloongezeka kila
mwaka na kati ya wagonjwa 100 wanaougua ugonjwa wa saratani, asilimia 47 kati
yao ni wanawake wanaougua Saratani ya shingo ya kizazi.
Kwa
upande wa akina Mama, Saratani ambayo inaongoza ni ile ya mlango wa kizazi na
takwimu zilizofanywa na Taasisi ya Ocean Road Kwa mwaka 2022 zinaonyesha
kati ya wagonjwa 100 ambao ni akina Mama, asilimia 47 wanakutwa na Saratani
ya mlango wa kizazi.
Lakini
pia, Saratani nyingine ambayo inafuatia Kwa kusababisha vifo vya akina Mama au
wanawake wengi ni Saratani ya matiti ambayo inachukua nafasi ya pili ikifuatiwa
na saratani ya koo.
Mwandishi
wa habari hizi alifanya mahojiano na Meneja wa huduma ya kinga ya Saratani
kutoka Taasisi ya Ocean road, Dr.Maguha Stephano, ambapo alieleza maana halisi
ya ugonjwa huo wa Saratani na matibabu yake ambapo awali alisema kuwa wamekuwa
na utaratibu wa kutoa huduma za upimaji wa Saratani ya shingo ya kizazi bure na
wamekuwa wakitembea katika hospitali zote za mikoa kwa ajili ya kutoa huduma
hizo.
SARATANI
NI NINI?
Ugonjwa
wa Saratani ni ugonjwa usioambukiza na ni ugonjwa ambao unatokana na mabadiliko
ya chembe hai ambazo zipo katika miili yetu, ambapo pia Saratani zote zina
kinga yake na pia zinafanyiwa uchunguzi.
Kwa
upande wa Saratani ya mlango wa kizazi, takwimu zinaonyesha kisababishi kikubwa
ni kirusi aina ya ‘Human Papilloma Virus’ na kinasambazwa kwa
njia ya kujamiiana, mwanamke anapokutana na mwanaume mwenye maambukizi ya
kirusi hicho ndio anapopata maambukizi na ugonjwa huu unachukua muda mrefu hadi
kugundua ikiwa ni kati ya miaka 10 hadi 15 kulingana na kinga ya Mwanamke.
Pia
kuna vihatarishi ambavyo mwanamke anaweza kuwa navyo vikampelekea kupata Saratani
hii baada ya kuwa na maambukizi ya kirusi cha ‘Human Papilloma Virus’. Kihatarishi
kimoja wapo ni wasichana wanaoanza kufanya ngono katika umri mdogo, kundi
hili lina hatari ya kupata ugonjwa huu.
Sababu
nyingine inayopelekea ni kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wengi na
kupelekea kupata maambukizi ya Kirusi hiko cha Saratani. Matumizi ya Tumbaku, tafiti
zinaonyesha kuwa matumizi ya Tumbaku katika mfumo wowote iwe sigara, Shisha, Ugoro
inamuweka mwanamke kwenye hatari ya kupata saratani ya mlango wa kizazi.
Matumizi
ya pombe pia ni hatari, lakini wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI pia wapo
katika hatari ya kupata maambukizi.
DALILI
ZA UGONJWA HUU
Dalili
za ugonjwa huu zinakuja pale ambapo ugonjwa upo katika hatua kubwa kidogo na
mara nyingi akina Mama wanasisitizwa kupima mapema ili kuepusha kusambaa kwa
ugonjwa huu. Dalili ni kama ifuatavyo:
I.
Dalili kubwa ni
kutokwa na damu ukeni ambayo sio ya hedhi, mwanamke anaweza kutokwa na
damu ukeni baada ya tendo la kujamiiana ama kusikia maumivu wakati wa tendo la
kujamiiana.
II.
Kuumwa na tumbo
chini ya kitovu, kina mama ambao wamekoma hedhi zao wale wenye umri mkubwa
kuanza kuona tena kutokwa kwa damu.
III.
Mabadiliko ya
hedhi, Kwa mfano kuongezekan kwa siku za mzunguko.
IV.
Kutokwa na damu
ukeni isiyokuwa ya kawaidamara nyingi ikiambatana na harufu au maji maji, Kuna
magonjwa mengine yaliyopo kwenye via vya uzazi yanaweza yakaambatana na
hizi dalili lakini Ili kuthibitisha unatakiwa ufike katika vituo vya afya ama
hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa kina.
Uchunguzi
wa Saratani ya mlango wa kizazi unafanyika Kwa mda mfupi, hakuna maumivu
yeyote, na ukionekana una mabadiliko ya awali unapatiwa tiba ya kugandisha
inayozuia chembe chembe hai zisiendelee kubadilika kuwa Saratani. Ugonjwa
huu unatibika kabisa endapo utapata matibabu ya mapema.
MOJA
YA MWANAMKE ALIEAMUA KUPIMA AELEZA
“Kweli
nashukuru nimekuja hapa Mount Meru hospitali kufanya uchunguzi wa Saratani ya
mlango wa kizazi na Saratani ya matiti, nashukuru maana nimepokelewa nimepewa
ushauri na nimehudumiwa. Napenda kuwahasa wanawake wenzangu ambao bado hawapo
tayari kuja kupima Saratani wajitahidi kuja kupima kwa sababu hali ya sasa ni
mbaya ukitegemea na vyakula tunavyokula waje wapime maana ni vyema wakajua afya
zao mapema na kuanza kuchukua hatua mapema.” Leah Mollel alieleza.
MADHARA
YA KIUCHUMI NA KIJAMII YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
i.
Msongo wa mawazo
na hisia, kuwa na hofu na matatizo ya akili.
ii.
Uwezekano mkubwa
wa kutokubeba Ujauzito tena.
iii.
Kunyimwa fursa za
kujikimu na vitendo vya unyanyasi.
TIBA
YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
Matibabu
ya saratani ya shingo ya kizazi hutolewa kulingana na hatua ya ugonjwa. Ugonjwa
ukiwa katika hatua za mwanzo huweza kutibika kabisa (ingawa kuna uwezekano wa
kujirudia).
Hatua
za mwisho za ugonjwa huu huwa haziwezi kupona kabisa ila Kinachofanyika
mara nyingi ni kutoa matibabu yatayotuliza dalili na maumivu na kumuwezesha
mgonjwa kuishi vizuri. Huduma za matibabu hutolewa kwa njia zifuatazo:
1)
Upasuaji katika hatua za mwanzo za ugonjwa.
2)
mionzi.
3)
Dawa za Saratani.
4)
Mionzi pamoja na dawa za Saratani.
MADHARA
YA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
Yafuatayo
ni madhara yanayoweza kutokea endapo mgonjwa mwenye Saratani ya shingo ya
kizazi atashindwa kupata matibabu mapema;
1)
Figo kushindwa kufanya kazi.
2)
Fistula.
3)
Kutokwa na damu kwenye uke.
JINSI
YA KUJIKINGA NA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI
Wanawake
wanashauriwa kufanya mambo yafuatayo ili kujikinga na saratani ya shingo ya
kizazi ambayo ni pamoja na;
1)
Kupata chanjo ya ‘Human papilloma virus’.
2)
Kuepuka ngono katika umri mdogo.
3)
Kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu.
4)
Kutumia kondomu kila mara unapojamiiana.
5)
Epuka kuvuta sigara.
6)
Kufanyiwa uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi angalau mara moja kwa
mwaka.
7)
Tibu kikamilifu magonjwa ya zinaa.
8)
Punguza matumizi ya mafuta mengi kwenye chakula.
KWANINI
CHANJO YA HPV NI MUHIMU?
Saratani
ya shingo ya uzazi huwaathiri zaidi ya wanawake nusu milioni kila mwaka na
husababisha vifo vya wanawake laki mbili na nusu kwa mujibu wa shirika la afya
duniani WHO.
Ni
mojawapo ya saratani inayowakumba wengi lakini pia ni mojawapo ya Saratani
inayoweza kuzuilika.
Chanjo
dhidi ya HPV hulinda usalama dhidi ya maambukizi yanayohusishwa kwa karibu na
saratani hiyo, na ukaguzi wa mapema husaidia kutambua seli kabla hazijageuka
saratani.
WITO
KWA SERIKALI
Serikali
imetoa mchango wake mkubwa na tunaiomba iendelee kutoa mchango
mkubwa wa kuendelea kuelimisha jamii juu ya ugonjwa huu wa Saratani. Waandishi
wa habari pia watumie kalamu na sauti zao kuendelea kuelimisha jamii juu
ya ugonjwa huu wa Saratani.
NINI
KIFANYIKE KUMALIZA KUPUNGUZA UGONJWA HUU?
Saratani
ya shingo ya kizazi inazuilika au kutibika kabisa endapo itagundulika ikiwa
kwenye hatua za awali, hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya yako kwa kadri
utakavyoshauriwa na wataalamu.
Wanawake
wote walio na umri kuanzia miaka 30 na kuendelea wanatakiwa kufanya uchunguzi
wa Saratani ya shingo ya kizazi. Wakati wa uchunguzi wa Saratani ya shingo ya
kizazi ni sasa, usisubiri hadi uone dalili, fika kituo cha huduma za afya kwa
ushauri na mwongozo Zaidi.
habari hii imeandikwa na Woinde shizza wa libeneke la kaskazini blog