KUONDOA DHANA POTOFU :UWEZEKANO WA WANAWAKE KUJIAJIRI KATIKA SEKTA YA UCHOMELE



Flora kweka wa kwanza kushoto mwanamke anayefanya kazi ya uchongaji vyuma katika taasisi ya usanifu na ubunifu mitambo TEMDO akimuelekeza Moja ya mwanafunzi aliekuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika taasisi hiyo namna ya kuchonga vyuma

Na Woinde Shizza, ARUSHA

 

Tatizo la ajira bado ni changamoto kubwa inayowasumbua wanawake wengi hapa nchini, japo kuwa kuna baadhi yao wamediriki hata kusomea fani au kazi zile zinazosemekana na baadhi ya watu kuwa zinapaswa kufanywa na wanaume, wakati huo huo bado serikali ina vipaumbele vichache kwa kuwapa ajira wale ambao wamejitosa kuingia darasani na kusomea fani zinazodaiwa na baadhi ya watu kuwa zinapaswa kufanywa na wanaume.

 

Ripoti mpya ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeeleza kuwa, hakuna mabadiliko makubwa ya mgawanyo wa ajira kisekta kwa kutumia tafsiri ya kitaifa kati ya mwaka 2014 na 2020/21 ingawa ajira katika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zilisinyaa. 

 

Mabadiliko makubwa ya mgawanyo wa ajira yameonekana miongoni mwa watu walioajiriwa katika sekta ya kilimo (66.8% 2014 na 58.4% 2020/2021) na shughuli nyingine binafsi za kiuchumi zisizo za kilimo (mwaka 2014 asilimia 26.6, na mwaka 2020/21 asilimia 22.7).

 

Ripoti hiyo ya Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi ya mwaka 2020/21, imesema kuwa kusinyaa kwa kiwango cha waajiriwa Serikalini kunatoa taswira kamili ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kati ya mwaka 2015 na 2020 ambapo zilitolewa ajira mpya chache. 

 

Hii inaonyesha kwamba zinahitajika juhudi kubwa kuvutia uwekezaji na biashara zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, hasa kwa wanawake ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

 

Frida Munishi ni mwanamke mwenye shahada ya uhandisi mitambo na amekuwa akijitolea kufanya kazi Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa katika taasisi ya ubunifu na usanifu mitambo (TEMDO) anaeleza kilio chake kikubwa alichonacho cha kukosa ajira katika kipindi chote hicho japo amekaa darasani na kusoma lakini tatizo lake kubwa ni kukosa ajira.

 

Anaeleza kuwa kabla hajasoma masomo ya uhandisi, alikuwa anapenda sana maswala ya uhandisi, ndio sababu iliyomfanya kuingia huku na kupambana bila ya kuangalia nani atasema nini au atachukuliwaje na jamii.

 

Anaeleza kuwa nia yake haswa ni kufanya kazi na kujipatia kipato, lakini awali alipokuwa anaanza kazi hii alipitia changamoto mbalimbali ikiwemo mfume dume ambao watu waliokuwa wanampa kazi za kufanya za nje kama uchomeleaji, utengenezaji madirisha na milango walikuwa wanampa kazi kwa shingo upande kwa madai kuwa hataiweza Kwa sababu  yeye ni mwanamke.

 

Frida  Munishi mwanamke mwenye  degree ya usanifu mitambo aliendelea kuendesha mashine ya kudizaini vyuma 

"Mimi apa nilipenda hii kazi mara baada ya kuona mamangu mdogo anafanya kwa iyo nilipomaliza masomo yangu ya sekondari niliamua kujiunga na chuo cha veta Kwa ajili ya kufanya kazi hii ya kuchomelea na kiukweli nilifanikiwa ila tatizo kubwa naloliona ni ajira  ya uhakika sisi wanawake katika fani hii tumekuwa hatuaminiki hivyo mtu mpaka akuletee kazi yake amejitafakari sana" Flora aliongeza.

Anabainisha kuwa amekuwa anajitolea katika taasisi mbalimbali za Serikali Kwa kipindi kirefu, nafasi zimekuwa zinatoka lakini amekuwa anashindwa kuomba Kwa sababu hana vigezo vinavyostahili.

 

WANAPOKUWA KAZINI USHIRIKIANO UPOJE NA WENGINE

 

Anabainisha kwa kutoa shukrani kuwa, tangu waanze kufanya kazi kuanzia ngazi ya chuo mpaka sasa wanapojitolea katika taasisi za Serikali wamekuwa wakipewa ushirikiano mkubwa sana na wanaume ambao wanawakuta katika maeneo yao ya kazi.

 

"Tunachoshukuru wanaume tunaofanyanao kazi wamekuwa wanatupa ushirikiano mkubwa sana haswa tunapokuwa nao katika kazi moja yale ambayo tumekuwa hatuyajui wamekuwa wakituelewesha, wakati mwingine, unakuta wanapata kazi za nje wanatusaidia kwa kutuunganisha na sisi ili tuweze kupata fedha za kujikimu" Alisema Flora.

 

 KAZI HII YA UHANDISI MITAMBO NA UCHOMELEAJI UMEWASAIDIAJE?

 

       i.          Kujipatia kipato cha kuweza kujikimu; tangu kuanza Kwa kazi hii wameweza kujipatia kipato kidogo ambacho kinawasaidia angalau kupata fedha Kwa ajili ya kujiendeleza kimaisha.

 

     ii.          Kuongeza ujuzi waliotoka nao chou; tangu walipoanza kujitolea wamekuwa wakufanya kazi nyingi za ndani na nje, hivyo mafanikio mengine ambayo ameyapata ni pamoja na kuongeza ujuzi wao waliotoka nao shule. 

 

CHANGAMOTO WALIZONAZO NI ZIPI?

 

       i.          Matatizo wanayokumbana nao ni pamoja kukutana na baadhi ya makampuni kuwashusha hadhi na kuwaona kama wakiwaajiri hawawezi kufanya kazi hizo kama wanavyofanya wanaume.

 

     ii.          Malipo madogo kutoka katika Taasisi za Serikali, hivyo 0wamekuwa wakifanya kazi bure hali inayowapelekea kuishi katika mazingira magumu.

 

    iii.          Ukosefu wa mitaji (fedha) Kwa ajili ya kununua vifaa vya kufanyia kazi pindi wanapopata kazi za nje.

 

 

 

 

 

 

 

 


FURSA ZA KIBIASHARA

 

Fursa za kibiashara zipo nyingi, lakini ni pale tu mwanamke atakapokuwa amefanya kazi na ikakubalika na mteja wake, pale anapoaminiwa na mteja basi inakuwa rahisi mteja yule kumletea kazi mbalimbali.

 

Pindi mwanamke anapokuwa mbuninifu wa vitu mbalimbali kama vile mapambo na kadhalika, itamsaidia watu kupenda biashara yake na kuamua kununua. Mfano, kwa sasa kuna fursa ambayo wanawake wengi ambao wanafanya kazi ya uchomeleaji wanafanya ni ile ya kutengeneza stendi za aina tofauti za kuwekewa maua au kuchonga bidhaa mbalimbali Kwa kutumia chuma.

 

Aidha, iwapo mwanamke akiwa amepitia masomo yake vizuri na kupata ujuzi wa kutosha itamsaidia kuweza kujiajiri ikiwemo kufungua eneo lake Kwa ajili ya kufanya kazi.


 

WITO GANI WANAUTOA KWA SERIKALI?

 

       i.          Wameiomba serikali kutoa kipaumbele au kutoa nafasi za upendeleo Kwa wanawake ambao wamesoma masomo ya uhandisi wa aina yoyote, ikiwemo uchomeleaji, uchongaji pamoja na ubunifu.

 

     ii.          Aidha Taasisi hizi za Serikali zitenge fedha angalau kidogo za kuwapa wanawake ambao wanajilea katika Taasisi zao Kwa ajili ya kuwawezesha kuweza kujikimu katika baadhi ya majukumu.

 

    iii.          Wamevitaka vyuo vya ufundi ikiwemo VETA kupunguza masharti ya kutoa ajira na waweze kuwapa ajira kuanzia wanafunzi wenye ngazi ya pili ili waweze kujitafutia ajira wakati wakiwa wanafanya kazi ili kuwasaidia na wale wanaotoka kwenye familia duni.

 

    iv.          Idadi ya wanafunzi wa kike katika fani hiyo bado ni ndogo ikilinganishwa na wanaume, ni dhahiri juhudi na mkakati wa makusudi unahitajika ili kuongeza udahili wa kundi hili hasa katika fani ya uhandisi na uchomeleaji.

 

      v.          Serikali iaangalie namna ya kuwapatia mitaji (mikopo) rahisi isiyokuwa na riba itakayowasaidia kuanza kujiajiri wenyewe Ili waweze kununua vitendea kazi.

 

Afisa uhusiano na masoko kutoka Temdo, Dkt. Sigisbert Mmasi akiongea

AFISA UHUSIANO NA MASOKO KUTOKA TEMDO ALONGA 

 

Kwa upande wake Afisa uhusiano na masoko kutoka Temdo, Dkt. Sigisbert Mmasi, alisema kuwa serikali imekuwa inatoa vipaumbele Kwa wanawake katika swala la ajira lakini shida iliopo ni kwamba wanawake wengi wamekuwa hawana sifa zinazostahili.

 

 

"Shida ya Wanawake inaanzia shuleni unakuta serikali imewapa vipaumbele wasichana wote wanaosoma masomo ya sayansi lakini chakushangaza unakuta wasichana wengi wanakimbilia masomo ya biashara na sanaa na ndio maana unakuta hata kwenye upande wa ajira ni wachache waliopo katika hizi fani za uhandisi na hata ufundi mchundo (uchomeleaji & uchongaji).” Alisema Afisa huyo.

 

Alitolea mfano katika taasisi ya TEMDO, na kusema kuwa tangu mwaka 2006 ni mwanamke mmoja tu aliajiriwa kama fundi mchundo na Kuna wengine wawili ambao wanaojitolea akiwepo wa mwaka mmoja. 


 

WITO KWA WANAWAKE 

 

Alifafanua kuwa, wanawake wengi wanaona kazi za uhandisi na kuchomelea ni ngumu zaidi na wengi wao wanataka kazi nyepesi hivyo aliwataka wanawake kuamka na kuacha kuchagua kazi bali wafanye kazi yeyote itayowaingizia kipato kwani kazi ni kazi, kwani kwasasa kuna vifaa maalumu vinatumika pahala pakazi ili kumlinda mfanyakazi asidhurike wakati anatekeleza majukumu yake.

 

Aidha aliwataka watoto wa kike waliopo mashuleni kusomea masomo ya sayansi kwani serikali imetoa vipaumbele Kwa watoto wa kike wote watakao soma masomo hayo.

 

Tatizo la ajira ni kubwa mno hususani kwa wanawake, ni vyema serikali ikaamua kutoa kipaumbele au kutenga nafasi kwa ajili ya ajira za wanawake, iwapo ikitangaza ajira kumi basi watoe vipaumbele ajira tatu au nne ziwe maalumu kwa wanawake.

 

 

 

 

 

 

 

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post