Na Woinde Shizza, ARUSHA
“Bado ugonjwa wa Fistula ni tishio kwa wanawake wengi
wanaojifungua wengi wao wakiwa ni wale wanaoishi katika maeneo ya nje ya
miji (VIjijini) wamekuwa wanakumbwa na ugonjwa wa Fistula wengi wao wakiwa
hawautambui ugonjwa huo kabisa huku baadhi yao wakiuhusisha ugonjwa huo na
dhana za kishirikina.”
Hospitali ya Maternity Afrika
(kivulini hospital) imekuja na suluhisho kwa ajili ya wanawake wanaopata
ugongwa wa Fistula kwa kutoa huduma za matibabu pamoja na upasuaji kwa
wanawake wote ambao wanapata ugonjwa huo na huduma zao wamekuwa wakizitoa bure
bila ya malipo yoyote.
“Hali ni mbaya sana, sina
takwimu halisi lakini niseme hali ni mbaya mno, mbaya zaidi kumekuwa na
changamoto ya wanawake hawa kutohudhuria hospitali pindi wanapopata ugonjwa huu
wengine wakihofia kupata aibu lakini sisi tumekuwa tukiwafata
wanawake hao huko vijijini tunawapa elimu ya ugonjwa huu kuwa unatibika pia
tunapowakuta wana ugonjwa huu tumekuwa tunawachukuwa kwa gharama zetu na
kuwaleta hapa hospitali na kuwatibu, tena tunawatibu bure bila ya gharama
yeyote ile.“Alibainisha mkunga wa hospitali hiyo Dkt. Musa Laizer.
Kwa mujibu wa takwimu za UNFPA
zinakadiria kwamba takribani wanawake milioni 2 Kusini mwa jangwa
la afrika, Sahara, Asia, ulimwengu wa Kiarabu, Amerika Kusini na Caribbean
wanaishi na Fistula na visa vipya kati ya 50,000 hadi 100,000 hutokea kila
mwaka duniani kote.
Aidha Kituo cha afya cha huduma ya kijamii kisicho
cha serikali kijulikanacho kama CCBRT, kwa mujibu wa takwimu zake
kinaeleza kuwa kila mwaka wanawake 3000 nchini Tanzania hupata Fistula.
Mkunga wa ugonjwa huu wa Fistula ya uzazi kutoka
katika hospitali ya Maternity Afrika (kivulini hospital) inayowasaidia wanawake
wanaopata ugonjwa huu kwa kuwapa huduma ya matibabu bure Dkt. Musa Laizer
anaeleza zaidi kuhusiana na ugonjwa huu ambapo anaeleza kuwa umekuwa ni
changamoto kubwa sana inayokumba wanawake hususa ni wale wa pembezoni na wale
wanaotoka katika familia maskini.
MAANA YA UGONGWA WA FISTULA
Fistula, ni hali inayompata mama pale ambapo anapokuwa
na uchungu mda mrefu au mtoto kukaa njiani kwa mda mrefu na hiyo
husababisha tundu kati ya njia ya uke na kibofu au kibofu na njia ya haja
kubwa ambayo husababisha mama kupata mkojo bila kuzuia au haja kubwa bila
kuweza kuzuia.
mwandishi wa habari hizi akifanyia mahojiano moja ya mgonjwa |
SABABU ZINAZOSABABISHA UGONJWA WA FISTULA YA
UZAZ
Sababu
zinazosababisha ugonjwa huu kwa wanawake ni pamoja na mama kuugua au kukaa
na uchungu kwa muda mrefu kabla ya kujifungua.
Shinikizo la muda mrefu litokanalo na kichwa cha
mtoto kwenye njia ya uzazi ya mama hukata usambazaji wa damu, na kusababisha
mishipa kufa na shimo linalojitokeza linaitwa fistula.
AINA ZA UGONJWA WA FISTULA
Aina ya kwanza ni ile ya kawaida
ni shimo kubwa kati ya njia ya uzazi na kibofu cha mkojo (inayoitwa
vesicovaginal fistula)
Fistula ya Rectovaginal; Shimo
kati ya njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa.
Fistula ya urethrovaginal; Shimo kati ya njia ya
uzazi na mrija wa kupitisha mkojo Urethra ambayo hubeba mkojo kutoka kwenye
kibofu hadi nje ya mwili.
Fistula ya Ureterovaginal; Shimo kati ya mirija
ya uzazi ya kupeleka mkojo kwenye kibofu na njia ya uzazi.
Vesicouterine fistula: Shimo kati ya kibofu
na mfuko wa uzazi au uterasi.
Baadhi ya fistula husababishwa na taratibu za uzazi
kama vile upasuaji na sehemu kutokana na huduma duni za afya na mafunzo au
ujuzi mdogo wa upasuaji, hii huitwa fistula ya iatrogenic.
Lakini pia kuna Fistula ya kiwewe ambayo
husababishwa na ukatili wa kingono haswa katika maeneo yenye migogoro,
uharibifu wa uke unachukuliwa kuwa jeraha la vita.
DALILI ZA UGONJWA HUU
i.
Kutokwa na mkojo au haja kubwa bila kujitambua na
kushidwa kujizuia.
ii.
kutokwa na haja kubwa kama mama amepata fistula
sehemu ya haja kubwa au muda mwingine anaweza kutokwa na vyote viwili kwa
wakati mmoja.
MADHARA YATOKANAYO NA
UGONGWA WA FISTULA KIMWILI NA KISAIKOLOJIA
i.
Maisha ya wanawake walio na hali hiyo yanaelezwa
kuwa ni ya mateso ya muda mrefu ya kimwili na kihisia.
ii.
Tatizo hili linaweza kusababisha maambukizi,
vidonda, magonjwa ya figo, vidonda vyenye maumivu makali, ugumba na kifo.
iii.
Harufu mbaya itokanayo na uvujaji wa mara kwa mara
wa mkojo au kinyesi huwatenga wanawake ambao mara nyingi huaibishwa na
kunyanyapaliwa, kutelekezwa na marafiki na familia zao na kutengwa na jamii
zao.
iv.
Msongo wa mawazo na hisia za kutaka kujiua na
masuala mengine ya afya ya akili.
v.
Wakinyimwa fursa za kujikimu, wanaingizwa zaidi
katika umaskini na mazingira magumu ya hatari.
WASICHANA WADOGO NDIO WAPO
KATIKA HATARI ZAIDI YA KUPATA UGONJWA HUU
Regina Ruchapa, ni mkazi wa
ushirombo Mkoani Geita, anaeleza kuwa amekumbwa na ugonjwa huu wa
fistula mwezi wa Januari, 2023 na alijifungua mtoto wake Januari
14 na mara baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani aliweza kukaa
wiki moja ndipo mkojo ukaanza kutoka.
“Nilikuwa siujui ugonjwa huu na
waliponiruhusu nikaona mkojo unatoka baada ya wiki moja ndio nikarudi tena
hospitali niliojifungulia nipo rudi pale wakaniambia tu nianze tu mazoezi,
nikaanza mazoezi mwili nao ukabadilika ukaanza kuvimba kutokana na mabadiliko
yale.” Alisema Regina.
“Nilikuwa sijui kama ni ugonjwa
na kiukweli niliamini kuwa nimerogwa na wakati nimerudi nyumbani nilitaka
kwenda kwa wataalamu wa jadi wakati najiandaa ndipo nilipopigiwa simu na ile
hospitali ambayo nilijifungulia maana niliacha namba wakaniambia nijiandae kwa
ajili ya kuja huku Arusha kupata matibabu.” Aliongeza.
“Nashukuru kwakweli tangu nifike
apa kivulini nimepona kabisa na nimejua fistula ni ninini na nimejua ugonjwa
huu unatibika niwaambie tu wale wanawake ambao wanapata agonjwa huu hautibika
niwaambie tu fistula inatibika na hapa nilipo kuna mwezangu wa uko kijijini
nilimpigia nikampa ushuhuda na kumwambia huu ni ugonjwa unaotibika na sio
kulogwa nilivyoongea nae amekubali na yupo njiani anakuja na yeye kutibiwa. “Alimalizia
Regina.
MATIBABU YA FISTULA
Inaelezwa kuwa asilimia 95%
ya fistula inaweza kufungwa kwa upasuaji, lakini katika hospitali za kawaida
gharama za matibabu ya ugonjwa huu ni kubwa sana hali ambayo wanawake wengi
walio na Fistula hawawezi kuimudu endapo wanafahamu hata hali halisi ya kiafya
waliyo nayo na kwamba matibabu yapo.
Lakini pia kabla ya kufikia hatua ya matibabu, mkazo
unapaswa kuwa juu ya kuzuia hatua hizo ambazo ni pamoja na: -
i.
Upatikanaji wa huduma za uzazi wa
mpango.
ii.
Wakunga wenye ujuzi na huduma ya dharura ya uzazi.
iii.
Kushughulikia mambo ya kijamii yanayochangia fistula kama
ndoa za utotoni, mimba na elimu ya wasichana.
iv.
Umaskini na ukosefu wa uwezeshaji wa wanawake ambavyo
pia ni sehemu ya Kampeni ya mkakati wa kukomesha Fistula.
Wakunga
ni sehemu muhimu ya suluhisho ili kukomesha fistula ya uzazi, pia kunahitajika
ushirikishwaji kamili wa wakunga katika ngazi ya jamii, kitaifa, kikanda na
kimataifa.Mbali ya ukosefu wa huduma bora za afya, umaskini ni
hatari kubwa ya kijamii kwa sababu unahusishwa na ndoa za mapema na utapiamlo.
Kujifungua mtoto kabla ya viungo vya uzazi kukomaa
kikamilifu pamoja na utapiamlo, kimo kidogo na hali duni za afya kwa ujumla
huchangia sababu za kisaikolojia katika wakati wa uchungu wa kujifungua
unaopelekea kupata Fistula, hata hivyo, wanawake wenye umri mkubwa ambao tayari
wameshapata watoto, wako katika hatari pia.
Kwa nyongeza, sababu ya ukosefu
wa usawa wa kijinsia katika jamii nyingi, wanawake hawana uhuru au uharaka wa
kuamua ni lini waanze kupata watoto au wapi pa kujifungulia.
Njia zifuatazo
zikizingatiwa vyema husaidia kuzuia tatizo la fistula baada ya kujifungua: -
i.
Kuhakikisha kuwa mwanamke anapata ujauzito wa kwanza
akiwa amepevuka vyema.
ii.
Kuacha tamaduni na desturi potofu kama vile kuzaa
watoto wengi kama njia ya kuonyesha ufahari.
iii.
Kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na
kujifungulia hospitali au kituo cha afya.
iv.
Hatua stahiki kuchukuliwa inapotokea dharura kama
vile kupata uchungu muda mrefu wakati wa kujifungua.
MATIBABU
Matibabu ya ugonja huu
ni upasuaji ili kwenda kutatua tatizo. Tatizo la fistula linatibika kabisa
hivyo basi unapopata tatizo hili la fistula usisite kwenda katika kituo cha
afya kilicho karibu nawe uweze kupata maelekezo juu ya utaratibu uliowekwa na
serikali kupitia wizara ya afya ikishirikiana na hospitali ya CCBRT na
hospitali nyingine za Serikali au hospitali ya kivulini kwa ajili ya kupata
matibabu ambayo hutolewa bure kwa sasa.
NINI KIFANYIKE KUMALIZA UGONJWA
HUU
Kutolewa kwa Elimu; Wananchi
wengi hususani wanawake, wale ambao wanakaa vijijini wamekuwa hawana elimu juu
ya ugonjwa huu, hivyo ni wakati wa serikali kuamka na kuanza kutoa elimu kwa
wananchi wote wanaoishi vijijini juu ya ugonjwa huu pamoja na kuwaeleza
umuhimu wa kuhudhuria kliniki katika kipindi cha ujauzito pamoja na kuwaeleza
faida za kujifungulia hopitalini na kuwahi.
Ni wakati wa serikali
kuhakikisha wanawapa elimu wauguzi ambao wako katika vituo vya afya juu ya
namna ya kumsaidia mwanamke ambaye anaviashiria vya ugonjwa wa fistula pindi
wanapofika hospitali kujifungua.
Serikali iendelee kutoa elimu ya kuwataka kina mama waendelee kujifungulia katika vituo vya afya na kuangalia wale ambao wapo mbali na vituo vya afya waweze kujengewa vituo vya afya ambavyo wanaweza kwenda kwa wakati na kusaidika na hayo yakifanyika tatizo la fistula litapungua sana kama sio kumalizika kabisa
“Ugonjwa huu
ukilinganisha mijini na vijijini, sehemu ambapo kuna mkusanyiko
mkubwa wa watu wanaopata ugonjwa huu ni wachache mno tofauti na vijijini
ambao ni wengi, kati ya kina mama kumi ambao wanajifungulia vijijini, watatu
wanakadiriwa kuwa na ugonjwa wa fistula na kushindwa kufika katika kituo cha
afya kwa ajili ya msaada, na wengine wanahofia gharama na kuhisi wamelogwa,
hivyo suluhisho kubwa na la kwanza ni kutolewa kwa elimu ili kutokomeza
ugonjwa huu”