Wadau wa Habari Watakiwa Kusambaza Taarifa Sahihi za Hali ya Hewa kwa Umma

 






Na Mwandishi Wetu,


Dodoma.


Katika Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Tanzania uliofanyika jijini Dodoma, wadau wa sekta ya habari wamesisitizwa umuhimu wa vyombo vya habari kuripoti kwa usahihi na kwa wakati taarifa za utabiri wa hali ya hewa. 


Taarifa za Hali ya Hewa ni muhimu kwa jamii mbalimbali ikiwemo wafuhaji,wakulima na hususan katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo mikusanyiko ya watu inaweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.


Katika hotuba yake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, alihusisha umuhimu wa kuripoti taarifa za hali ya hewa na kaulimbiu ya Siku ya Redio Duniani ya mwaka 2025, isemayo "Redio na Mabadiliko ya Tabianchi." Alisema, "Kaulimbiu hii inatukumbusha wajibu wa vyombo vya habari, hususan redio, katika kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake. Kuripoti kwa usahihi taarifa za hali ya hewa ni sehemu muhimu ya jukumu hilo."



Prof. Kabudi aliongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kusaidia jamii kuelewa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu utabiri wa hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika.




Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekuwa ikitoa utabiri wa hali ya hewa wa saa 24, siku tano, kumi, mwezi, na msimu, pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa. Hata hivyo, usambazaji wa taarifa hizi unategemea sana vyombo vya habari ili kuwafikia wananchi kwa wakati. Kwa mfano, TMA imekuwa ikitoa tahadhari kuhusu mvua kubwa, upepo mkali, na mawimbi makubwa, ambazo ni muhimu kwa sekta mbalimbali kama kilimo, uvuvi, usafiri, na afya.




Kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu, ni wazi kwamba vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kuchukua hatua stahiki.




Katika mkutano huo, wadau pia walisisitiza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinafikishwa kwa wananchi kwa usahihi na kwa wakati, ili kuwawezesha kuchukua tahadhari zinazofaa na kufanya maamuzi sahihi katika shughuli zao za kila siku.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi kama TMA ili kuhakikisha taarifa muhimu kama za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa usahihi.

Kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za hali ya hewa katika maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi, ni wazi kwamba vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuhakikisha taarifa hizi zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.



Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post