BREAKING NEWS

Wednesday, October 5, 2011

WAAJIRI WATAKIWA KUWADHAMINI WAFANYAKAZI WAO

WAAJIRI kutoka sekta mbalimbali nchini wametakiwa kudhamini na kuheshimu uwepo wa vijana hususani wale walioko kwenye ajira zisizo rasmi huku kipaumbele kikilenga zaidi wanawake katika kuhakikisha wanapatiwa haki zao zote za msingi pamoja na kuingizwa katika ajira iliyo rasmi na kupatiwa haki zote za msingi.

Vijana wengi hususani wale walioko kwenye ajira zisizo rasmi wamesahaulika sana katika jamii huku wakikosa haki zao za msingi na kuendelea kuteseka katika maisha huku ikilinganishwa kuwa waathirika wakuu ni wanawake,hali inayochangia kuzidi kuongezeka kwa changamoto ya ajira hapa nchini.

Hayo yalisemwa jana na Afisa Maendeleo ya jamii wa mkoa wa Arusha, Blandina Nkini wakati akifungua mkutano wa waajiri kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Tanga,na Arusha uliolenga kujadili changamoto mbalimbali za ajira zilizopo katika sekta zisizo rasmi ulioandaliwa na shirika la kijerumani la idadi ya watu (DSW).

Alisema kuwa, wadau mbalimbali wakiwemo waajiri wanapaswa kudhamini na kulinda ajira za watanzania huku kipaumbele kikilenga zaidi katika sekta za ajira zisizo rasmi kwani wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana huku wakikosa sehemu ya kupeleka kilio chao.

Nkini alisema kuwa,tatizo la ajira linaongoza kwa kiasi kikubwa sana katika nchi yetu huku wanaoadhirika zaidi wakiwa ni vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa letu, hivyo umefika wakati sasa kwa waajiri kuelekeza nguvu zao na kuweka kipaumbele katika kuwasaidia vijana kuondokana na changamoto hizo.

‘Unajua changamoto hii ya ajira kwa vijana ni tatizo sugu kwa taifa letu hususan wale walioko katika sekta zisizo rasmi ambao walengwa zaidi ni wanawake , jamani serikali yenyewe haiwezi kutatua changamoto hizo bila ya kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na watu wenye moyo wa kutatua changamoto zinazowakabili, hivyo naomba taasisi mbalimbali ziendelee kujitokeza ili kuondokana na changamoto hiyo,alisema Nkini.

Afisa programu wa shirika hilo,Christina Sudi alisema kuwa, mkutano huo unalenga zaidi kujadili changamoto zinazowakabili vijana walioko kwenye sekta zisizo rasmi hususani wasichana ambao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana katika maisha bila kuwa msimamo wa maisha.

Alisema kuwa,shirika hilo hadi sasa hivi limeweza kuwapatia vijana hao kutoka mikoa ya Arusha, Tanga na Kilimanjaro elimu juu ya ujasiriamali, na Afya ya uzazi kwa vijana wapatao 270 ambapo wamefanikiwa kutoka kwenye ajira zisizo rasmi na kuingia kwenye ajira rasmi huku wengine wakijiajiri wenyewe.

Sudi alisema kuwa,pia wameweza kusaidia jumla ya klabu 42 za vijana katika kuwapatia mitaji mbalimbali ya biashara na kuweza kuondokana na hali ngumu ya kimaisha waliyokuwa nayo .

‘Unajua lengo la shirika hili ni kuhakikisha kijana yeyote aliyeko katika ajira isiyo rasmi hususani wasichana wameweza kuondokana na ajira hiyo na kuweza kujiunga na sekta zilizo rasmi, pia katika kufanikisha hilo tumekuwa tukitoa mafunzo juu ya Afya ya uzazi na ujasiriamali ili kutokana na wengi wao kutokuwa na elimu hiyo na kupitia mradi huo tumeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana’alisema Sudi.

Alisema kuwa, kupitia mradi huo wameweza pia kusaidia jumla ya hospitali tisa , katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kwa kuwapatia zana mbalimbali za uzazi wa mpango lengo likiwa ni kuwafikia walengwa ambao ni vijana walioko katika maeneo hayo.

Pia wameweza kukarabati hospitali mbili ya Kaloleni mkoani Arusha na St. Raphael Korogwe kwa lengo la kuwezesha vijana kupatiwa huduma rafiki kwa vijana katika hospitali hizo.

Naye Mchumi kutoka Wizara ya Kazi na Ajira, Joseph Nganga akichangia mada katika mkutano huo alisema kuwa, vijana ni watu ambao wanapaswa kuangaliwa kwa karibu sana kwani ,asilimia 11.7 ya watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira, huku asilimia 14.5 ya vijana hawana ajira kwa nchi nzima.

Alisema kuwa, hali hii inaonyesha wazi pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali za kumsaidia kijana lakini bado juhudi za lazima kutoka kwa wadau binafsi wanapaswa kulitupia macho swala hili ili kuweza kuliokoa taifa la kesho ambalo ni vijana walio wengi ambao hawana kazi za kufanya na hii ni hatari sana kwa nchi yetu.

Nganga alisema kuwa, tatizo la ajira lipo zaidi mijini kutokana na kuwa asilimia kubwa ya vijana wanakimbilia mijini kufuata ajira badala ya kubaki vijijini na hii ni kutokana na kutoboreshwa kwa miundombinu katika maeneo ya vijijini hali inayowalazimu wengi wao kushindwa kubaki vijijini.

Hivyo kuna haja ya kuboreshwa kwa mazingira ya vijijini kwanza ili kumwezesha vijana kutokimbilia mijini ambapo wanasababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiokuwa na ajira na kuwa ni changamoto kubwa zaidi.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates