Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu ya
kesi inayomhusi Waziri wa zamani wa Vijana wa Rwanda, Callixte Nzabonimana Mei
31, 2012.
Nzabonimana
anakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji
hayo, uchochezi, kuteketeza kizazi na mauaji kama uhalifu dhidi ya
binadamu.
Pande zote
mbili katika kesi hiyo ziliwasilisha hoja zao za mwisho Oktoba 20 na 21, 2011
huku upande wa mwendesha mashitaka ukitaka impatie adhabu ya kifungo cha maisha
jela iwapo mshitakiwa atatiwa hatiani, kwa kuhusika kwake katika mauaji ya
kimbari ya mwaka 1994.
Kwa mujibu wa
mwendesha mashitaka, Nzabonimana alikuwa mchochezi mkuu wa mauaji hayo mkoani
kwake alikozaliwa, Gitarama, katikati ya Rwanda. ‘’Nzabonimana hakuwa Waziri
nchini Norway au Sweden bali Waziri nchini Rwanda.Alikuwa kama simba mkoani
Gitarama mwaka 1994.Aliweza kusimama na kutoa wito kwa wananchi kuanza kuwaua
Watutsi na amri zake zilikuwa zinazingatiwa na kutekelezwa.’’Mwendesha
mashitaka, Paul Ng’arua alieleza.
Upande wa
utetezi umeiomba mahakama kumwachia huru mteja wao katika mashitaka yote
yanayomkabili wakidai kwamba mashitaka hayo ‘’yalitungwa’’ na ‘’yamejaa
uongo.’’
Philippe
Larochelle, Wakili Msaidizi wa Nzabonimana alidai kwamba mashahidi walioletwa
kutoka magerezani nchini Rwanda walikiri kuwa walishawishiwa kuwatuhumu viongozi
waliokuwa madarakani wakati wa mauaji ya kimbari ili kupunguziwa adhabu katika
hukumu za kesi zao.
Waziri huyo
alitiwa mbaroni nchini Tanzania Februari 18, 2008 na kesi yake ilianza Novemba
9, 2009 na kuhitimishwa Septemba 12,2011. Mwendesha mashitaka aliita mashahidi
20 wakati upande wa utetezi uliita mashahidi 38.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia