MBUNGE wa jimbo la Arumeru mashariki Joshua Nasari (chadema) amewasihi vijana,kujifunza uwajibikaji na kuachana na starehe zisizo za msingi hususani unywaji wa pombe wa kupindukia aina ya viroba,hatua ambayo itawasaidia kuwa na maono yenye tija katika kujiletea maendeleo wenyewe na kuondoa dhana tegemezi.
Nasari ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha watoto yatima cha African Orphanage kilichopo Sakila ,uzinduzi huo ulienda sanjari na sherehe za kumuaga mwinjilishaji na mwasisi wa makanisa ya Pentekoste wilayani Arumeru,Askofu Nickson Issangya anayeenda kuhubili injili nje ya nchi katika nchi za Afrika na balani Ulaya.
Aidha alisisitiza kwa kuwataka wananchi katika jimbo hilo kushikamana kwa pamoja na kusahau itikadi zao za kisiasa kwani muda wa kampeni umeisha na mbunge amepatikana.
Alisema wakazi wa jimbo hilo wengi wao wamekuwa wakijengeana chuki zinazosababishwa na tofauti za kisiasa hadi makanisani bila kutambua kuwa uchaguzi sasa umeisha na kinachotakiwa ni kuwajibika kwa kufanyakazi za kuleta maendeleo katika jimbo hilo na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine mbunge huyo alitoa ushuhuda wa maisha yake na kudai kuwa wakati akisoma shule ya msingi alikuwa akiuza kwa kutembeza minadani mifuko aina ya plasitiki maarufu kwa jina la Marliboro, kwani wazazi wake hawakuwa na uwezo wa kumlipia ada.
Alisema kuwa wakati akisoma alipandikizwa maono ya ubunge na mwenyezi mungu ,hivyo katika kipindi chote cha masomo yake kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu,ndoto zilizokuwa zikimjia usingizini ni kuhusiana yeye kuwa mbunge .
Aliwataka wananchi katika jimbo hilo kushikana katika kuliletea maendeleo jimbo la Arumeru mashariki,lenye changamoto nyingi ikiwemo ya uhaba wa Ardhi,na kudai kuwa atafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha analeta mabadiliko na kwamba wakazi wa jimbo hilo hawatajuta kumchagua .
Kwa upande wa Askofu Nickson Issangya aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kuacha kubaguana kwa itikadi za kisiasa hadi makanisani na kuwataka kupigania maendeleo yao wenyewe wakimtumaini mwenyezi mungu kwa kuwa kampeni za uchaguzi zimeisha na mbunge amepatikana.
Katika sherehe hiyo mbunge Nasari aliahidi kusaidia vituo vya watoto yatima vilivyomo katika jimbo hilo na kuwataka wananchi kujikita zaidi kutoa msaada kwenye makundi yasiyojiweza hususani watoto yatima wajane na akinamama wazee,kwani kabla ya kuwa mbunge aliwahi kufanyakazi kwenye kituo cha watoto yatima wapatao 86 .
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia