WAKILI WA RYANDIKAYO APEWA HADI JUNI 15, KUJIBU MAOMBI YA MWENDESHA MASHITAKA

Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imetoa hadi Juni 15, mwaka huu kwa wakili wa zamu wa mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ambaye bado anasakwa, Charles Ryandikayo kujibu maombi ya mwendesha mashitaka ya kutaka kuihamishia kesi hiyo kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.
‘’Mahakama inamwamuru wakili wa zamu kujibu maombi ya mwendesha mashitaka ifikapo Juni 15, 2012,’’ inaeleza sehemu ya uamuzi huo wauliotolewa Mei 24, 2012.
Mwendesha mashitaka Mei 9, mwaka huu aliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kutaka kuihamishia nchini Rwanda, kesi ya Ryandikayo, meneja wa zamani wa mgahawa mmoja katika wilaya ya Gishyita pamoja na kesi nyingine inayomkabili aliyekuwa Meya wa wilaya Gisovu, Aloys Ndimbati. Wilaya zote zipo katika mkoa wa Kibuye.
Katika maombi yake,wakili wa zamu wa mtuhumiwa Ryandikayo, Nelson Merinyo wa Tanzania,aliomba muda wa wa miezi mitano ili kujibu hoja za mwendesha mashitaka na kwamba alipokea nakala ya maombi hayo Mei 18, 2012.
Alifafanua kuwa anataka kujibu hoja hizo kwa ‘’ upana na kwa kina’’ hivyo kuhitaji muda zaidi kutimiza adhama hiyo.
Ryandikayo anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa ushiriki wao katika mauaji ya kimbari ya 1994. 
Kwa mujibu wa hati hiyo ya mashitaka Ryandikayo alishiriki katika mauaji ya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto waliokusanyika ndani ya kanisa la Mubuga na kuwaelekeza wanamgambo na polisi kulishambulia kanisa hilo kwa risasi, mabomu ya mkono na silaha nyingine.
Maombi hayo yamekuja baada ya maamuzi ya Mahakama Mei 8, 2012 kuhamishia nchini Rwanda, kesi ya mtuhumiwa ambaye bado anatafutwa, Ladislas Ntaganzwa.
Maombi mengine matatu ya aina hiyo yameshatolewa uamuzi na ICTR ambayo yanawahusu, Mchungaji Jean Uwinkindi na watuhumiwa wawili ambao nao bado wanasakwa ikiwa ni pamoja na Fulgence Kayishema na Charles Sikubwabo.
Uamuzi mwingine bado unasubiriwa juu ya mshitakiwa Bernard Munyagishari anayesadikiwa kuwa kiongozi wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi, Kaskazini ya Rwanda.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia