Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya
Rwanda (ICTR) imeruhusu mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo kwa mara ya
pili kuleta ushahidi mwingine wa ziada kupinga utetezi wa kutokuwepo
eneo la uhalifu katika kesi ya aliyekuwa Wazri wa Mipango wa Rwanda,
Augustin Ngirabatware.
Wakati
mwendesha mashitaka akiruhusiwa kumwita shahidi mmoja zaidi kupingana
na utetezi wa mshitakiwa, Mahakama hiyo iliyokuwa inaongozwaa na Jaji
William Sekule imekataa ombi la upande wa utetezi kuleta mashahidi wake
watano wa ziada kupinga ushahidi wa mwendesha mashitaka.
Katika
uamuzi wake wa Mei 18, 2012, mahakama ilibaini kwamba ‘’ kigezo cha
kufungua upya kesi ya mwendesha mashitaka kwa mashahidi wa ziada
kimetimizwa na itakuwa ni kwa masilahi ya haki kumsikiliza shahidi
(aliyehifadhiwa jina) PRWIII.’’
‘’Mahakama
imeamuru kwamba shahidi huyu wa utetezi aletwe kutoa ushahidi haraka
iwezekanavyo na isiwe zaidi ya Juni 6, 2012,’’ inasomeka sehemu ya
uamuzi huo. Mahakama hiyo imepanga kukutana Juni 18, kwa ajili ya kupata
majumuisho ya mwisho toka kwa pande mbili husika katika kesi hiyo.
Mahakama
imeeleza kwamba ushahidi wa PRWIII, ambaye ni mwana diplomasia wa
Nigeria una umuhimu katika kutoa changamoto kwenye utetezi wa mshitakiwa
kwamba hakuwepo eneo la uhalifu, kati ya Aprili 23 na Mei 23, 1994.
Katika kipindi hicho mshitakiwa alidai hakuwepo nchini Rwanda bali nje
katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Senegal, France, Swaziland,
Togo na nyinginezo.
Mashahidi
sita wa ziada wa mwendesha mashitaka walitoa ushahidi wao ulioanza
kupokelewa tangu Machi 6, 2012 na shahidi PRWIII naye alitarajiwa
kufanya hivyo pia. Lakini hadi Aprili 2, wakati mwendesha mashitaka
anafunga kesi yake, shahidi huyo alishindwa kufika mahakamani kwa sababu
serikali ya nchi yake ilikuwa haijatoa ruhusa kwake.
Ikiyatupa
maombi ya utetezi ya kuita mashahidi wake wa ziada, Mahakama ilieleza
katika uamuzi tofauti ambao nao ulitolewa Mei 18, kwamba hakuna hata
mmoja wa mashahidi waliopendekezwa aliyefikia sifa za kuwa shahidi wa
ziada.
‘’Lengo
la kuita mashahidi wa ziada ni kutoa nafasi kwa utetezi kukana jambo
jipya linalotokana moja kwa moja na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa
ziada wa mwendesha mashitaka, na kama jambo hilo jipya ni muhimu katika
kesi husika na ambalo pia lingeweza kutarajiwa na upande wa utetezi,’’
mahakama ilifafanua.
Hivi
sasa Mahakama hiyo pamoja na pande mbili katika kesi hiyo za mwendesha
mashitaka na utetezi zipo nchini Rwanda kutembelea maeneo kunakosadikiwa
kuwa uhaliofu ulitendeka. Maeneo hayo ni pamoja na mjini Kigali na
maeneo yanayozunguka, Gitarama (Rwanda kati) na Gisenyi (Kaskazini
Magaribi).
Waziri
huyo wa zamani anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji ya
kimbari, mauaji ya kimbari au kushiriki mauaji hayo, uchochezi,
kuteketeza kizazi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia