TRA TATAKIWA KUFUNGUA OFISI MANYARA
MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) Mkoa
wa Manyara imetakiwa kufungua ofisi yake Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya
Simanjiro ili kuwawezesha madereva wa pikipiki za kubebea abiria (bodaboda)
kukata leseni zao.
Hayo yameelezwa na Mkuu mpya wa
kituo cha polisi Mirerani,Mrakibu msaidizi wa polisi Mohamed Mkalipa wakati
akizungumza na madereva wa pikipiki wanaotoa huduma ya usafiri wa abiria kwenye
mji huo.
Mkalipa alisema kutokana na umbali wa
ofisi za TRA ulipo kati ya Babati na Mirerani unawafanya madereva wengi
kushindwa kukata leseni,hivyo ni vema mamlaka hiyo ikaanzisha ofisi zao
Mirerani ili madereva wapate huduma hiyo.
“Kutokuwepo ofisi za TRA wilaya hapa
na pia kwenye mji mdogo wa Mirerani kunakwamisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji
wa leseni za madereva hivyo viongozi wa mamlaka hiyo wanapaswa walibebe kwa
uzito,” alisema Mkalipa.
Pia aliwataka madereva hao kutii
sheria za usalama barabarani na kutoa ushirikiano kwa askari wa usalama
barabarani kupitia dhana ya polisi jamii kuliko kukimbia kila wakati wanapokuwa
na makosa ya barabarani.
Alisema madereva wa pikipiki
wanatakiwa kutii sheria bila shuruti kwa kutimiza masharti yote ya usafirishaji
wa abiria ikiwemo kuvaa kofia ngumu wanapoendesha pikipiki kwa ajili ya usalama
wao endapo wakipata ajali.
Hata hivyo,waendesha pikipiki hao
waliunga mkono tamko la mkuu huyo la TRA kufungua ofisi zao kwenye mji huo
kuliko kufika mara chache na kuwavizia kipindi ambacho hawana fedha za kulipia
leseni.
“Kitendo cha TRA kutokuwa na ofisi za
kudumu kwenye wilaya hii kinatukwaza sana,kwani sisi wenyewe tungekuwa
tunakwenda peke yetu na kulipa fedha siyo kama sasa wanapokuja mara moja moja
kwa kutuvizia,” walisema.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia