Wakati
Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne
imehitimisha kupokea ushahidi maalum katika kesi inayomhusu mtuhumiwa wa
mauaji ya kimbari anayesakwa vikali na mahakama hiyo, Felicien Kabuga,
kesi kama hiyo pia dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Rwanda,
Augustin Bizimana aliahirishwa hadi Juni 25, 2012.
‘’Upokeaji
wa ushahidi maalum katika kesi ya Kabuga ulimalizika jana (Jumanne) na
jumla ya mashahidi sita walijitokeza kumtetea mtuhumiwa,’’ Msemaji wa
ICTR, Roland Amoussouga aliliambia libeneke la kaskazini Jumatano.
Wakili
wa zamu anayemwakilisha Kabuga katika kesi hiyo, Bahame Nyanduga
alianza kuwasilisha mashahidi wa utetezi wa mteja wake Aprili 23, 2012.
Mwendesha mashitaka kwa upande wake alianza kuita mashahidi Mei 23,2011
na kuhitimisha Oktoba 28, 2011.
Kabuga
anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo,
au kushiriki mauaji hayo, kujaribu kufanya mauaji ya kimbari, uchochezi
na ukatili dhidi ya binadamu hususan ni utesaji na kuteketeza kizazi.
Amossouga pia alisema kwamba ICTR imeahirisha usikilizaji wa ushahidi
maalum wa upande wa utetezi katika kesi ya Bizimana hadi Juni 25.
‘’Kuhusu Bizimana, usikilizaji wa ushahidi umeahirishwa hadi Juni 25,
2012 kwa kuwa shahidi wa tatu wa utetezi alisema hataweza kupatikana
kabla ya Juni 20,’’ Msemaji alifafanua.
Usikilizaji
maalum wa ushahidi wa kesi hufanyika kwa lengo la kukusanya na
kuhifadhi ushahidi husika ili kuweza kutumika baadaye iwapo watuhumiwa
husika watatiwa hatiani.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia