WANANCHI WA KATA SOKON ONE WAPANGA KUANDAMANA

WANANCHI  wa kata ya Sokon 1mtaa wa Muriet katika manispaa ya Arusha wamepanga kuandamana kumwona waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Anna Tibaijuka endapo hawatashughulikiwa mgogoro wao wa muda mrefu  kati yao na manispaa ya jiji la Arusha.

Aidha wananchi hao wanailalamikia manispaa ya Arusha kwa kushindwa kuwalipa fidia wakazi 115 wa eneo hilo, licha ya kuwataka wapishe  kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa dampo la kisasa.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake  , Mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao , Jackson Japhet alisema kuwa, wamehangaika kwa kipindi kirefu sana kutafuta haki yao ya msingi lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, hivyo kwa sasa wamelazimika kuandamana kumwona waziri mwenye dhamana ili kumfikishia kilio chao.

‘’sisi wananchi  kwa pamoja tumekubalina kuandaa maandamano makubwa kwenda kumuona  waziri  Tibaijuka  tuweze kupatiwa haki zetu za msingi ,hivi sasa tunakamilisha taratibu za usafiri na maladhi ‘’alisema Japhet.

Aliongeza kuwa, swala la kupisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa dampo la kisasa wao hawalipingi wala hawataki kupingana na serikali ila tatizo lililopo ni kutokana na fidia ndogo iliyotangazwa na manispaa hiyo ambapo ,manipaa imepanga kuwalipa kiasia cha shilingi milioni 1 hadi 2 ,kiasi ambacho wamedai ni kidogo na hakitoshelezi.

'kwa mfano pale kuna wananchi wana nyumba kubwa za kisasa zenye zaidi ya thamani ya  milioni 9, wana  viwanja vingine pembeni halafu wamejenga makaburi ya watoto wao pale, sasa wanakuja kutuambia tuondoke halafu wanatulipa milioni 2 tupeleke wapi wakati hiyo hela haifiki hata robo ya thamani za mali zetu'alisema Mwenyekiti huyo.

Alifafanua zaidi kuwa, wanachotaka wananchi hao ni kulipwa fidia kulingana na mali zao, kwani vinginevyo inakuwa ni hasara kubwa sana kwani imefikia mahali manispaa wanakupa hundi kidogo huku wakidai tuchukue halafu tuandike barua ya kuomba kulipwa fedha nyingine ,huo ni udanganyifu mkubwa sana wa wananchi.

Jackson aliongeza kuwa,kwa sasa hivi kuna jumla ya wananchi 25 ambao tayari wamerubuniwa na kukubali kusaini kifuta jasho hicho kwa fedha tofauti huku wakitakiwa kuandika barua ya kuomba hela tena lakini hao waliofanya hivyo kwa sasa  wanalalamika kwani walishaandika barua na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Jackson   alisema kuwa, wao walikuwa wakiishi katika eneo hilo kabla hata ya kuwepo kwa  dampo  hilo ambapo wao waliwapatia manispaa eneo la heka 10 na kuweza kuweka dampo hilo ambapo waliomba tena kuongezewa heka  79 na wananchi hao wakakubali.

Aliongeza kuwa, mgogoro huo umejitokeza baada ya manispaa kutaka  tena kuongezewa mita 100 kutoka zile heka 79 hali ambayo imekuwa ni kilio katika wananchi  hao  kwani huo ni uonevu mkubwa sana unaofanywa na jiji hilo.

Alisema kuwa, kinachosikitisha zaidi wananchi hao hawajapewa muda wa kutoa maoni yao kuhusiana na mradi huo wa dampo unaotakiwa kuwekwa katika maeneo hayo badala yake uongozi wa manispaa walifika katika maeneo hayo na kuwaelezea lakini hawakupewa nafasi ya wao kutoa maoni yao na kuelezwa kuwa kwa wale watakaoathirika kwenye hizo mita 100 watapewa fidia lakini hakuna kitu.

‘Jamani kinachotushangaza ni kuwa , kama kweli tunalipwa fidia ya maeneo yetu na viwanja pia inakuwaje baadhi ya watu wanapewa  16,000 , wengine 20,000 huku wengine wakipewa 60,000 na wengine 6,000,000 , na wengine wakipewa hata 20,000 sasa hapa jamani mtu unapewa kweli milioni 6 utajenga au utanunua kiwanja wakati hayo yalikuwa ni maeneo yetu na tulishajenga nyumba za kudumu ’alisema Japhet.

Alifafanua zaidi kuwa, hicho wanacholipwa wao sio fidia bali hicho ni kifuta jasho tu kwani haiwezekani mtu ana ardhi yake na pia anamiliki nyumba ya gharama kubwa sana lakini hela anayopewa haitoshi kitu chochote ina maana hiyo hela tunayopewa basi watupe na viwanja vya kujengea basi vinginevyo hatuondoki katika maeneo hayo.

Aliongeza kuwa, kama kweli serikali inataka kujenga mradi katika eneo hilo lazima wawatendee wananchi wa eneo hilo haki,ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia kwa kufuata sheria na kanuni na maeneo ya kujenga wapewe sio kulipwa fedha kidogo wakati maeneo ya kujenga hawana.

Hata hivyo wananchi hao tayari wameshaandika barua ya malalamiko hayo kwa viongozi mbalimbali wa mkoa wa Arusha na kutuma nakala  kwa Mkurugenzi wa manispaa ya jiji la Arusha, Mkuu wa wilaya ya Arusha, na  Mkuu wa mkoa wa Arusha lakini hadi sasa hivi hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Estomih Chang'ah alipotafutwa kuzungumzia swala hilo hakuweza kupatikana nan juhudi zaidi zinaendelea.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post