WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Magara Wilaya ya Babati Mkoani
Manyara ambao tangu mwaka 2007 walikuwa wanakabiliwa na tatizo la maji ya
kunywa na kutumia hatimaye wamepatiwa ufumbuzi baada ya kuchimbiwa kisima.
Akizindua kisima hicho kilichojengwa kwa msaada wa Mkurugenzi wa
Rift Wall,Jiwa Sisodiya,Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini Vrajilal JituSon
alimshukuru Sisodiya kwa msaada huo na kuwasihi walimu na wanafunzi kutunza
mradi huo.
JituSon aliitaka jamii ya eneo hilo kuishi vizuri na wawekezaji
ili waweze kusaidiana kusukuma gurudumu la maendeleo kwani Tarafa ya Mbugwe ina
utajiri wa kutosha lakini jamii inakabiliwa na umasikini mkubwa.
“Hawa wawekezaji wetu wa bonde la Kiru wametoa misaada mingi kwa
jamii hivyo inatubidi sisi kama jamii ya sehemu husika tuwape ushirikiano kwani
bila ushirikiano mafanikio hayatakuwepo ,” alisema JituSon.
Naye,Mkuu wa shule hiyo ya Magara Silvester Umbayda alisema hadi
kukamilika kwa mradi huo ulioanza kujengwa Januari 28 mwaka huu umegharimu sh6
milioni zilizotolewa na Sisodiya na familia yake.
Umbayda alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ilikuwa
inakabiliwa na changamoto kubwa ya matumizi ya maji ya kunywa na kutumia lakini
baada ya kuchimbwa kwa kisima hicho cha futi 105 tatizo hilo limekwisha.
Kwa upande wake,Sisodya alisema aliamua kuchimba kisima hicho
baada ya kupata malalamiko ya wanafunzi wa shule hiyo kuwa wanaharisha kila
mara baada ya kunywa maji ya mto Magara ambayo maji yake siyo masafi.
“Mimi na familia yangu tuliamua kugharamikia kuchimba kisima hiki
ili wanafunzi hawa wasipate adha ya kuugua mara kwa mara ugonjwa wa tumbo baada
ya kunywa maji machafu ya mto,” alisema Sisodya.
Alisema zaidi ya mradi huo alishasaidia miradi mingi ikiwemo sh12
milioni za ujenzi wa barabara,alitoa vyandarua 4,000 vya kujikinga na
mbu,miwani 100 ya macho ya wazee na alijitolea magunia 500 ya mahindi wakati wa
njaa.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia