Mahakama ya
Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itatoa hukumu ya kesi
inayomkabili afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Kapteni Idelphonse Nizeyimana
Juni 19, 2012, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mahakama hiyo
Ijumaa.
Nizeyimana anakabiliwa na
mashitaka ya mauaji ya kimbari, kuteketeza kizazi, mauaji na ubakaji.
Mwendesha mashitaka pamoja na
mambo mengine anadai kwamba mshitakiwa alikuwa mtu wa pili kimadaraka aliyekuwa
anashughulikia Usalama na Operesheni za Kijeshi katika Chuo cha Maafisa wa Jeshi
Wasiokuwa na Kamisheni (ESO), mkoani Butare, Kusini ya Rwanda.
Nizeyimana anadaiwa kuamuru,
kusimamia na kupanga mauaji dhidi ya Watutsi katika maeneo mbalimbali mkoani
humo ikiwa ni pamoja na mauaji dhidi ya Malkia wa Kitutsi, Rosalie Gicanda
Aprili 21, 1994.
Katika kuwasilisha hoja za
mwisho Desemba 7, 2011, mwendesha mashitaka aliiomba mahakama iliyokuwa
inaongozwa na Jaji Lee Muthoga, kumpatia adhabu ya juu kabisa inayoweza kutolewa
na mahakama hiyo ya kifungo cha maisha jela iwapo atatiwa hatiani.
‘’Adhabu pekee muafaka kwa
mujibu wa mwendesha mashitaka ni kumpatia kifungo cha maisha jela ,’’
alipendekeza Mwendesha Mashitaka, Drew White.
White pia hakulifumbia macho
suala la madai ya kuhusika kwa mshitakiwa katika mauaji dhidi Malkia wa Kitutsi,
Rosalie Gicanda kwa kueleza kwamba, mashahidi wawili wa kuaminika wa upande wa
mwendesha mashitaka walitoa ushahidi wao akiwemo mjukuu wake na
mpishi.
Hata hivyo, John Philpot,
Wakili Kiongozi wa Nizeyimana alipangua hoja za mwendesha mashitaka kwa kusema
kuwa ameshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mteja wake pasipo mashaka.
Alisema kwamba mteja wake alichukua hatua sahihi zilizopaswa kuchukuchukiwa na
askari nyakati za vita.
‘’Mteja wangu hakuwa kiongozi
wa ESO, hakuwa na mamlaka kamili na hakuwa na mamlaka ya kisheria juu ya askari
waliodaiwa kuwa chini ya himaya yake,’’ alisema wakili huyo.
Pia wakili huyo aliwasilisha
ushahidi wa kuwa mteja wake wakati fulani hakuwepo katika maeneo yalikofanyika
uhalifu kwenye miezi ya Aprili na Mei, 1994 bali muda huo alikuwa katika kiwanda
cha Chai cha Mata, mkoani Gikongoro akiendesha mafunzo ya kijeshi kwa askari
wapya.
‘’Kesi hii sasa iko mikononi
mwenu. Tunawaomba kusimama katika ukweli na haki kumwachia huru Nizeyimana,’’
Nizeyimana aliwaomba majaji alipokuwa anakamilisha kuwasilisha hoja zake za
mwisho.
Nizeyimana alitiwa mbaroni
nchini Uganda, Oktoba 5, 2009 na kuhamishiwa katika gereza la Mahakama ya Umoja
wa Mataifa Arusha, Tanzania, siku iliyofuata. Alikana mashitaka dhidi yake
alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 14, 2009.
Kesi yake ilianza kusikilizwa
Januari 17, 2011 ambapo mwendesha mashitaka aliita mashahidi 38 na upande wa
utetezi pia uliita idadi sawa na hiyo na kufunga kesi yake Februari 25, 2011.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia