Mwendesha
Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR),Hassan Bubacar Jallow amewasilisha maombi mengine mawili ya
kutaka kesi za watuhumiwa wawili wa mauaji ya kimbari ambao bado
wanasakwa na mahakama hiyo zikasikilizwe nchini Rwanda.
Maombi
yaliyowasilishwa yanawahusu Aloys Ndimbati, Meya wa zamani wa Gisovu na
Charles Ryandikayo aliyekuwa meneja wa mgahawa mmoja katika wilaya ya
Gishyita, zote mbili zipo katika mkoa wa Kibuye. Watu hao wanashitakiwa
kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, uhalifu dhidi
ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa ushiriki wao katika mauaji ya
kimbari ya 1994.
‘’Mwendesha
mashitaka aliwasilisha maombi hayo wiki iliyopita Mei 9. Tumemwomba
Rais wa Mahakama kupangia majaji wa kusikiliza maombi hayo na kuyatolea
uamuzi wa uhamisho,’’ Mkuu wa Kitengo cha Rufaa na Ushauri wa Kisheria
katika Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, James Arguin aliliambia Shirika la
Habari la Hirondelle, Jumatatu.
Hati
ya mashitaka inadai kwamba Ndimbati binafsi aliwashambulia raia wa
Kitutsi na kuwapeleka wanamgambo na wachochezi wengine wa ghasia katika
eneo la Bisesero ambako maelefu ya wanaume, wanawake na watoto walikuwa
wanapata hifadhi kufuatia mashambulizi yaliyofanywa dhidi yao kabla,
katika mkoa huo wa Kibuye.
Kwa
mujibu wa hati hiyo ya mashitaka pia, Ryandikayo alishiriki katika
mauaji ya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto waliokusanyika ndani ya
kanisa la Mubuga na kuwaelekeza wanamgambo na polisi kulishambulia
kanisa hilo kwa risasi, mabomu ya mkono na silaha nyingine.
Maombi
hayo yamekuja baada ya maamuzi ya Mahakama Mei 8, 2012 kuhamishia
nchini Rwanda, kesi ya mtuhumiwa ambaye bado anatafutwa, Ladislas
Ntaganzwa.
Maombi
mengine matatu ya aina hiyo yameshatolewa uamuzi na ICTR ambayo
yanawahusu, Mchungaji Jean Uwinkindi na watuhumiwa wawili ambao nao bado
wanasakwa ikiwa ni pamoja na Fulgence Kayishema na Charles Sikubwabo.
Uamuzi
mwingine bado unasubiriwa juu ya mshitakiwa Bernard Munyagishari
anayesadikiwa kuwa kiongozi wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi,
Kaskazini ya Rwanda.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia