BREAKING NEWS

Saturday, May 5, 2012

VIONGOZI WATUHUMIWA KUDAI RUSHWA

MGORORO wa uuzaji wa maeneo ya wazi katika kata ya baraa jijini Arusha,umechukua sura mpya baada ya wananchi kuwatuhumu hadharani viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani kuwa, waliomba kiasi cha shilingi 800,000 kwa mmiliki wa chuo cha ualimu cha Silla ili kubariki ujenzi wa chuo chake ndani ya eneo la wazi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi ya kata hiyo, walidai kuwa viongozi hao walitaka mmiliki wa chuo hicho,Adamu Shayo awapoze kwa kiasi hicho cha fedha ili aendelee na ujenzi kwenye eneo la wazi katika kata hiyo.
Tuhuma hizo ziliwalazimu viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani wa kata hiyo Paul Lotti Laizer pamoja na wanachi kwenda kupitia upya mipaka yote ya eneo la wazi la kata hiyo sanjari na kukakua bikoni za mipaka ya asili iliyokuwepo hapo awali inayosadikiwa kung’olewa na baadhi ya watu waliovamia na kujenga makazi ya kudumu kinyume cha sheria.
Kabla ya kuanza zoezi la uhakiki wa mipaka diwani Laizer alikanusha vikali tuhuma hizo na kuapa kuwa yeye hakuwahi kuomba wala kupokea rushwa katika kipindi chote cha uongozi wake na kuwataka wananchi waliomwangushia tuhuma hizo nzito,kuzithibitisha katika mkutano huo wa hadhara.
‘’mimi nimekuwa kiongozi wa kata hii miaka mingi na mpaka na kuwa meya siku wahi kuomba rushwa kwa mwanachi yoyote natambua sana mipaka ya kata hii tangu nikiwa mdogo mwaka 1962 nachunga mifugo wakati tukiiba mahindi tukiwa watoto,sasa leo iweje nisahau mipaka kwenye kata yangu’’alisema diwani huyo kwa uchungu huku akitishia kumwaga laana kwa wanaomtuhumu.
Hata hivyo wananchi hao walishindwa kuthibitisha tuhuma hizo na kuzua malumbano huku wakitetea hoja yao kwa kushinikiza kimabavu kuwa viongozi hao waliomba fedha hiyo,hali iliyomlazimu mzee mmoja kusimama na kujitambulisha kuwa yeye ni mkazi wa muda mrefu katika kata hiyo na ndiye aliyeuza eneo ambalo chuo cha ualimu cha Silla kimejengwa.
Katika Hatua nyingine mkurugenzi wa chuo cha ualimu cha Silla,Shayo aliwajia juu wananchi hao na kuwataka wathibitishe madai yao kabla ya kuwafikisha mahakamani na kuwaonya waache kutangaza kuwa chuo hicho kinampango wa kubomolewa wakidai kimejengwa kwenye eneo la wazi la kata hiyo.
Akiongea katika mkutano huo alidai kuwa, chuo chake kimejengwa kihalali kwa kufuata taratibu zote za sheria ya Ardhi, ikiwemo kuwa na hati halali ya umiliki wa kiwanja hicho (Title D. namba 34614 )Plot no, 288 eneo la baraa block GG iliyotolewa Desemba 20 mwaka 2011 na ofisi ya Ardhi kanda ya kaskazini.
Awali wananchi hao walitangaza kubomoa nyumba zote wanazodai kujengwa ndani ya eneo la wazi kikiwemo chuo hicho cha Silla ,hata hivyo uongozi wa kata hiyo uliwataka wananchi hao kuacha majungu na jazba zisizofaa kwani, taratibu za kuvunja nyumba ya mtu zinafanyika pale ambapo uongozi utaridhika na madai hayo kwa kufuata sheria.
Mwenyekiti wa kijiji cha Baraa Jacob Meja alieleza kusikitishwa na hatua ya wananchi hao kutangaza kujichukulia sheria mkononi kwa kuanza kubomoa nyumba za watu zinazodaiwa kujengwa kinyume cha sheria, na kuwaomba wawe wavumilivu ,kwani baada ya zoezi la uhakiki wa mipaka kukamilika,hatua zaidi zitafuata.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates