MAHAKAMA YA RUFAA YATHIBITISHA ADHABU ZA WAWILI NA KUMPUNGUZIA MMOJA


Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumanne, imethitisha adhabu za warufani wawili na kumpunguzia mwingine mmoja adhabu ya kifungo cha maisha jela hadi miaka 35.

Afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda Luteni Idelphonse Hategekimana ataendelea kutumikia adhabu yake ya kifungo cha maisha jela ambapo mfanyabiashara Gaspard Kanyarukiga naye ataendela kubaki kifungoni akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 aliyopewa na mahakama ya awali.

Aliyekuwa na bahati ya pekee katika rufaa yake ni Meja Aloys Ntabakuze ambaye amepunguziwa adhabu kutoka kifungo cha maisha jela hadi miaka 35.

Ntabakuze, ambaye alikuwa Kamanda wa Bataliani ya Makomando alitiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari,uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita Desemba 18, 2008 kwa sababu ya askari waliokuwa chini ya mamlaka yake kushiriki kwenye mauaji katika maeneo mbalimbali mjini Kigali.

Naye Luteni Hategekimana, aliyekuwa Kamanda wa kambi ndogo ya kijeshi ya Goma, mkoani Butare, Kusini mwa Rwanda,alipatikana na hatiani Desemba 6, 2010 kwa makosa ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu kutokana na mchango wake katika mauaji ya baadhi ya watu na kuamuru mauaji dhidi ya wakimbizi wa Kitutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika kanisa la Ngoma.

Kwa upande wake mfanyabiashara Kanyarukiga alitiwa hatiani Novemba 1, 2010 kwa makosa ya mauaji ya kimbari na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu kwa kupanga kwa kushirikiana na wengine, kubomoa kanisa lilokuwa Magharibi ya Rwanda, Aprili 16, 1994.

Watutsi wapatao 2000 waliokuwa wanapata hifadhi ya usalama wao katika kanisa hilo la Nyange, wilaya ya Kivumu katika mkoa wa Kibuye, waliuawa.

Hii ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mahakama hii miaka 17 iliyopita Mahakama yake ya Rufaa kutoa hukumu tatu katika siku moja.




Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post