WAZIRI MAKONDA: STENDI KUU ARUSHA KUWA NGUZO YA UCHUMI NA MAANDALIZI YA AFCON 2027


Na Woinde Shizza, Arusha

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini,  Paul Makonda, amesema ujenzi wa stendi kuu ya mabasi jijini Arusha ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa wananchi na maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 yanayotarajiwa kufanyika nchini.

Akizungumza jijini Arusha wakati alipofanya ziara ya kutembelea  baadhi ya miradi inayosimamiwa na halmashauri ya jiji hilo, Waziri Makonda alisema wananchi wa Arusha wamekuwa na kiu ya muda mrefu kuona stendi hiyo ikijengwa, na sasa serikali imeanza utekelezaji rasmi wa mradi huo chini ya usimamizi makini wa mamlaka husika.

“Leo tunasema kwa uwazi na kwa furaha, stendi inajengwa sasa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha mradi huu unakamilika kabla ya mashindano ya AFCON ,huu ni mradi wa kimkakati unaolenga kuchochea maendeleo ya wananchi,” alisema Makonda.

Amesema miradi ya maendeleo kama hiyo ina gharama kubwa za fedha, muda na nguvu kazi, hivyo ni jukumu la wananchi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kulipa kodi ili fedha hizo zirudi kwao kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi.

Waziri huyo alibainisha kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni mzawa mwenye historia ya kufanya kazi kwa uadilifu na uwajibikaji, huku serikali ikihakikisha atalipwa vyeti vyake vya kazi kwa wakati

 “Hata kama malipo yatachelewa kidogo, mkandarasi huyu ameonyesha moyo wa kizalendo, Tunamheshimu kwa kuzingatia falsafa ya kazi na utu,” alisema Makonda.

Ameongeza kuwa ujenzi wa stendi hiyo utazalisha fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi, ikiwemo biashara ndogondogo, huduma za malazi, usafirishaji na uwekezaji wa miundombinu ya kibiashara ambapo alitoa wito kwa wakazi wa Arusha kutumia fursa hiyo kujiandaa mapema ili wawe miongoni mwa wanufaika wakubwa wa mradi huo.

“Serikali ya Dkt. Samia haitaleta fedha za biashara nyumbani kwako, bali inatengeneza mazingira ya fursa karibu yako, Ni jukumu lako kuzitumia ipasavyo,” alisisitiza Waziri Makonda, akiwataka wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani kushirikiana na kamati ya mipango miji kupanga matumizi bora ya maeneo jirani na stendi hiyo.

Aidha, alisema serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imekubaliana kujenga na kuhuisha reli ya kisasa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi eneo la uwanja wa AFCON jijini Arusha, hatua itakayoongeza tija katika usafiri, biashara na utalii kwa wananchi wa Arusha na mikoa jirani.

Mbali na mradi huo wa standi kuu ya mabasi pia aliweza kutembelelea mradi wa soko kuu la kilombero ,pamoja na mradi wa jengo kuu la utawala  la halmashauri ya jiji la Arusha ambapo aliwasisitiza viongozi,madiwani na mstaiki meya wa jiji hilo kusimamia vyema miradi hiyo huku akiwapa onyo la kutoanzisha mgogoro ya aina yoyote katika kutekeleza miradi hiyo na iwapo atatokea wa kuleta mgogoro  atamchukulia hatua kali ya kisheria.


 

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia