SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA MIFUMO ISIYO RASMI KAZINI


Na Woinde Shizza, Arusha


Serikali imewataka watumishi wa umma kuacha kutumia mifumo isiyo rasmi katika mawasiliano na utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi, ikisisitiza umuhimu wa kutumia mifumo rasmi ya Serikali Mtandao ili kulinda usalama wa taarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.


Kauli hiyo imetolewa Februari 19, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, wakati akihitimisha kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao (eGA) kilichofanyika kwa siku tatu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), kikihusisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka sekta za umma na binafsi.


Waziri Kikwete alisisitiza nidhamu ya kidijitali, akionya watumishi wanaotumia barua pepe binafsi kama Gmail, Yahoo na Hotmail kwa shughuli za kikazi, akieleza kuwa njia hizo hazina viwango vya usalama vinavyohitajika kulinda nyaraka na taarifa nyeti za serikali.


Aidha, alisema bado baadhi ya watumishi wanatumia njia zisizo rasmi katika miamala ya kifedha na mikopo, jambo linaloweza kuleta hatari za kiutumishi na kifedha licha ya serikali kuweka mifumo salama ya ndani.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Benedict Ndomba, alisema maazimio ya kikao hicho yanalenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora wa huduma za umma kupitia ushirikiano wa wadau wote. Alibainisha kuwa mkutano huo ulijadili mada 14 kuhusu utekelezaji wa miradi ya TEHAMA, ukiweka mkazo katika kuunganisha mifumo ya taasisi za umma, kuimarisha ulinzi dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, na kuharakisha utoaji huduma kupitia majukwaa ya kidijitali.


Ndomba aliongeza kuwa serikali mtandao ni kichocheo cha uchumi wa kidijitali kinachopunguza urasimu na kuongeza kasi ya utoaji huduma kama malipo ya serikali na usimamizi wa rasilimali watu.


Katika hafla hiyo, eGA ilitoa tuzo kwa taasisi zilizotekeleza miradi ya TEHAMA kwa kuzingatia sheria, kanuni na viwango vilivyowekwa.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, alisema matumizi ya mifumo ya serikali mtandao yamepunguza gharama za uendeshaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, akitoa mfano wa Bunge kuondoa matumizi ya karatasi na kutumia mifumo ya kielektroniki.


Ndumbaro alisisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya serikali ili kurahisisha huduma kwa wananchi kwa kutumia namba moja ya utambulisho wa taifa, huku akiahidi kuwa Bunge litaendelea kusaidia marekebisho ya sheria na bajeti ili kuharakisha mchakato huo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvila, alisema uamuzi wa kufanyika kwa mikutano ya serikali mtandao mkoani humo ni ishara ya imani ya taifa kwa mchango wa Arusha katika mageuzi ya kidijitali.


Serikali pia imeagiza waajiri katika taasisi za umma kuwekeza zaidi kwenye mafunzo ya wataalamu wa TEHAMA ndani na nje ya nchi ili kuhimili mabadiliko ya kasi ya teknolojia na kukabiliana na vitisho vya kimtandao.


Katika kumalizia, viongozi wa mkutano huo walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuendeleza mageuzi ya kidijitali yaliyosaidia kuongeza kasi ya utoaji huduma na uwajibikaji serikalini.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia