MAKONDA: KAMBI YA MATIBABU YAKUZA UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA MAPEMA

 



Na Woinde Shizza, Arusha

Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema kambi ya matibabu bila malipo inayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha inalenga kujenga utamaduni wa wananchi kupima afya mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema na kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika kambi hiyo Julai 14, 2026, Makonda alisema huduma zinazotolewa zimejengwa katika misingi ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, huku zikitoa fursa ya uchunguzi wa afya, ushauri wa kitaalamu na matibabu bila malipo.

Alisema kambi hiyo imebeba mafunzo muhimu kwa jamii, ikiwemo kuthamini utumishi unaogusa maisha ya watu, kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kusaidia wananchi kugundua changamoto za kiafya katika hatua za awali kabla hazijawa kubwa.

Makonda alieleza kuwa uchunguzi wa mapema huwasaidia wananchi kupata rekodi za afya zao, kupunguza matumizi holela ya dawa bila ushauri wa wataalamu wa afya na kuongeza uwezekano wa kupata matibabu sahihi kwa wakati.

Aidha, aliwataka wananchi wanaonufaika na huduma hizo kufuata maelekezo ya madaktari kuhusu matumizi ya dawa, kuhudhuria kliniki za ufuatiliaji pale inapohitajika na kutunza vifaa vya tiba wanavyopatiwa, ikiwemo miwani, ili kuhakikisha matokeo bora ya matibabu.

Alisisitiza kuwa ingawa wananchi wanapata huduma hizo bila kulipia, utekelezaji wa kambi hiyo umegharimu rasilimali kubwa kupitia Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, taasisi za afya, hospitali za Serikali na binafsi pamoja na wadau mbalimbali waliojitolea kuokoa maisha ya Watanzania.

Makonda alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya, pamoja na kuwapongeza madaktari, wauguzi na wataalamu wote wa afya wanaoshiriki kutoa huduma katika kambi hiyo.



Kambi ya matibabu bila malipo inaendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, ambapo mamia ya wananchi wanaendelea kupata huduma mbalimbali za uchunguzi, ushauri na matibabu kwa lengo la kuboresha afya na kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara






















About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia