MWENGE WA UHURU WATUA JIJINI ARUSHA KWA KISHINDO MIRADI YA SH. BILIONI 3.9 KUTEMBELEWA
Na Woinde Shizza, Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, leo Julai 9, 2026 amepokea Mwenge wa Uhuru 2026 kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloriana Julias Kimath, katika hafla iliyofanyika viwanja vya Magereza Kisongo, huku ukitarajiwa kutembelea miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh3.9 bilioni.
Akizungumza baada ya kuupokea Mwenge huo, Mkude alisema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilometa 89.2 katika Wilaya ya Arusha na kukagua, kuzindua pamoja na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa sekta za elimu, afya, maji, mazingira, uwekezaji na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Alisema Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Ng'onda, atazindua mradi wa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 katika Kata ya Olasit, Kimindorosi, wenye thamani ya Sh93 milioni, pamoja na mradi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Arusha wenye thamani ya Sh12 milioni.
Mbali na uzinduzi huo, Ng'onda ataweka mawe ya msingi katika miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Muriet (Bondeni City) unaogharimu Sh1.3 bilioni, jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Moivaro lenye thamani ya Sh376.7 milioni na ujenzi wa Barabara ya Ugiriki yenye urefu wa kilometa 1.1 kwa kiwango cha zege unaogharimu Sh1.79 bilioni.
Mwenge wa Uhuru pia utatembelea mradi wa uwezeshaji wananchi kiuchumi wa Kikundi cha Vijana cha Mclives Limited wenye thamani ya Sh76.7 milioni pamoja na mradi wa uwekezaji wa ufugaji wa kuku wa Devi uliopo Kata ya Osunyai wenye thamani ya Sh200 milioni.
Mkude alisema mbali na kukagua miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru atafanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa elimu kuhusu lishe, mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya, malaria na VVU/UKIMWI sambamba na kuwasilisha jumbe za kudumu za Mwenge wa Uhuru kwa wananchi.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026 ni, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo," ikihamasisha ushiriki wa wananchi katika kulinda amani, uwajibikaji na kuchochea maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya kijamii na kiuchumi.
![]() |
![]() |






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia