VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA FURSA ZA ZABUNI ZA SERIKALI
![]() |
Na Woinde Shizza, Arusha
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwang'onda, amewahimiza vijana nchini kutumia kikamilifu fursa za zabuni zinazotolewa na Serikali kupitia taasisi za umma kwa kusajili vikundi vyao katika mfumo wa manunuzi ya umma ili waweze kushiriki kwenye zabuni zinazotengwa kwa makundi maalumu.
Mwang'onda alitoa wito huo wakati wa ziara ya Mbio za Mwenge wa Uhuru katika Kijiji cha Magadini, Kata ya Mto wa Mbu, wilayani Monduli, baada ya kutembelea na kukagua mradi wa kikundi cha vijana cha Hakuna Matata Art, unaolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Alisema mradi huo una thamani ya Sh milioni 60, ambapo Sh milioni 40 ni mkopo usio na riba uliotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, huku Sh milioni 20 zikiwa ni mtaji uliowekezwa na wanakikundi wenyewe.
Mwang'onda alisema kikundi hicho ni mfano wa namna mikopo ya asilimia 10 inavyoweza kuwainua vijana kiuchumi, huku akisisitiza kuwa Serikali imeendelea kupanua fursa kwa kuwawezesha vijana kushiriki pia katika zabuni za taasisi za umma.
Alifafanua kuwa kila taasisi ya umma imeelekezwa kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya manunuzi kwa ajili ya makundi maalumu, yakiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo vijana wanatengwa asilimia 10 ya fursa hizo.
"Ni muhimu vijana wajisajili kwenye mfumo wa manunuzi ya umma ili waweze kushindania zabuni zinazotolewa na Serikali. Fursa hizi zimeanzishwa mahsusi kuwawezesha kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo," alisema Mwang'onda.
Aidha, aliwataka vijana kutumia ipasavyo mikopo na fursa zinazotolewa na Serikali kwa kuanzisha na kuendeleza miradi yenye tija, badala ya kusubiri ajira rasmi, akieleza kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira nchini.






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia