MAKONDA: ZAIDI YA WAGONJWA 20,000 WAHUDUMIWA KAMBI YA MATIBABU ARUSHA, 258 WAPEWA RUFAA
Na Woinde Shizza, Arusha
JUMLA ya wagonjwa 24,871 wamehudumiwa katika Kambi ya Matibabu ya Kibingwa na Ubingwa Bobezi iliyofanyika jijini Arusha, huku wagonjwa 258 wakibainika kuhitaji matibabu ya kibingwa zaidi na kupewa rufaa kwenda hospitali za juu kwa ajili ya upasuaji na matibabu maalumu.
Hayo yalisemwa leo na Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya kambi hiyo, akieleza kuwa huduma zilizotolewa zilijumuisha matibabu ya magonjwa ya moyo, damu, watoto, afya ya uzazi, macho, mifupa, afya ya kinywa na meno, ngozi, figo na mfumo wa mkojo, masikio, pua na koo (ENT), tiba mazoezi, lishe, afya ya akili pamoja na uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa wanawake.
Makonda alisema mbali na huduma za matibabu, wananchi walipatiwa elimu ya afya kuhusu kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Ebola, kifua kikuu, Virusi vya UKIMWI, sambamba na huduma za maabara, dawa na uchangiaji wa damu.
Alisema huduma hizo zilitolewa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali za afya nchini zikiwemo Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Kibong'oto, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, Hospitali ya Selian pamoja na hospitali zote za halmashauri za Arusha, Arumeru, Monduli, Longido, Ngorongoro na Karatu.
Kwa mujibu wa Makonda, zaidi ya wataalamu wa afya 720, wakiwemo madaktari bingwa, wauguzi na watumishi wa kada mbalimbali walishiriki katika utoaji wa huduma hizo, huku wastani wa wagonjwa 3,553 wakihudumiwa kwa siku, idadi iliyozidi lengo la kuhudumia wagonjwa 2,000 kila siku.
Alisema kati ya wagonjwa waliopatiwa huduma, 258 walibainika kuhitaji upasuaji wa haraka na matibabu ya kibingwa zaidi, ambapo baadhi walifanyiwa upasuaji ndani ya kambi huku wengine wakipewa rufaa na kuanza kufuatiliwa ili waweze kupata matibabu katika hospitali za juu bila kukwamishwa na gharama.
Makonda alitaja miongoni mwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa haraka kuwa ni mtoto wa mwaka mmoja kutoka Kisongo aliyebainika kuwa na uvimbe kwenye moyo unaohitaji matibabu yenye gharama ya takribani Sh milioni 27, mama mwenye saratani ya utumbo aliyeshindwa kufanyiwa upasuaji kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na ukosefu wa fedha pamoja na mgonjwa mwingine mwenye uvimbe kwenye ubongo unaohitaji matibabu ya zaidi ya Sh milioni 15.
Alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya inaendelea kuweka utaratibu wa kuhakikisha wagonjwa hao wanapata matibabu ya kibingwa kwa wakati, akisisitiza kuwa lengo la kambi hiyo halikuwa kutoa huduma za matibabu pekee bali kuhakikisha wananchi wanaohitaji matibabu ya juu wanafikishwa kwenye huduma stahiki na kuendelea kufuatiliwa hadi watakapopona.











0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia