ARUSHA KUNG'ARA KUPITIA TAMASHA KUBWA LA SANAA, KUVUTIA WAGENI WA KIMATAIFA

 



Na  Woinde Shizza , Arusha

Jiji la Arusha linatarajia kuwa kitovu cha sanaa, utalii na ubunifu mwezi Oktoba 2026 kupitia Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Kazi za Ufundi, linalotarajiwa kuwakutanisha maelfu ya wasanii, wabunifu, wawekezaji na wanunuzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Tamasha hilo linaandaliwa na Tanzania International Tourism Festival (TITF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TASFA), likiwa na lengo la kuimarisha sekta ya sanaa na utalii, kuongeza thamani ya kazi za ubunifu na kufungua masoko mapya kwa wasanii wa Kitanzania.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi wa TITF, Ibrahim Jamal, alisema tamasha hilo litakuwa jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania kupitia sanaa, huku likiwapa wasanii fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kuunganishwa na masoko ya kimataifa.

Alisema tamasha hilo litawakutanisha wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mavazi, watengenezaji wa vito, wafinyanzi na wasanii wa kazi za mikono kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kubadilishana uzoefu na kuendeleza ubunifu.

Jamal alisema pamoja na maonesho ya kazi za sanaa, washiriki watapatiwa mafunzo kuhusu uongezaji thamani wa bidhaa, ulinzi wa haki miliki za kazi za ubunifu pamoja na mbinu za kuingia katika masoko ya ndani na kimataifa.

Aliongeza kuwa tamasha hilo litakuwa na maonesho ya moja kwa moja ya utengenezaji wa kazi za sanaa (live demonstrations) pamoja na mikutano ya kibiashara (B2B), itakayowaunganisha wasanii na wanunuzi wakubwa pamoja na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.



Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TASFA), Rukia Walele, alisema tamasha hilo linafungua ukurasa mpya kwa sekta ya sanaa za ufundi ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa ubunifu na uhifadhi wa utamaduni wa Mtanzania.

Alisema kupitia zaidi ya vyama 20 vinavyounda shirikisho hilo, maelfu ya wasanii watanufaika kwa kupata fursa za kujifunza mbinu za kisasa za biashara, kujenga mitandao ya kibiashara na kutangaza bidhaa zao katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Walele alisema tamasha hilo linatarajiwa kuongeza kipato cha wasanii, kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii na kuiimarisha Tanzania kama kitovu cha sanaa za ubunifu barani Afrika.



Waandaaji wameeleza kuwa tamasha hilo linatarajiwa kuvutia maelfu ya wageni na washiriki kutoka mataifa mbalimbali, hatua inayotarajiwa kuimarisha uchumi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kupitia sekta za sanaa, utamaduni na utalii.








About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia