UZINDUZI WA MATOKEO YA SENSA YA KITAIFA YA WANYAMA PORI WAFANYIKA ,SWALA TWIGA WAHOFIWA KUTOWEKA ,KIJAJI ATAKA UCHUNGUZI WA HARAKA
Na Woinde Shizza,Arusha
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) pamoja na wadau wa uhifadhi kutumia matokeo ya Sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori kufanya tathmini ya kina kuhusu hali ya swala twiga ili kubaini sababu za kupungua kwa idadi ya mnyama huyo wa taifa.
Dk Kijaji alitoa kauli hiyo leo Juni 17, 2026 jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Kitaifa ya Wanyamapori uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo jengo la PAPU Tower kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema matokeo ya sensa hiyo yanapaswa kutumika kama msingi wa tafiti na hatua mahsusi za uhifadhi ili kubaini sababu za kupungua kwa swala twiga, ikiwamo uwezekano wa uwindaji haramu, mabadiliko ya tabianchi au changamoto nyingine zinazohusiana na makazi yake.
“Matokeo haya yatumike kujua swala twiga wanapotelea wapi, nani anawavuna na kama mabadiliko ya tabianchi yana mchango katika kupungua kwao. Lazima tuchukue hatua za haraka kunusuru spishi hii muhimu kwa taifa letu,” alisema.
Waziri huyo pia aliitaka TAWA kuendelea kusimamia uoto wa asili, hususani miti na mimea inayotegemewa na wanyamapori hao kwa chakula, ili kuhakikisha mazingira yao yanaendelea kuwa salama na rafiki kwa ustawi wao.
Akiwasilisha matokeo ya sensa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. Eblate Mjingo , alisema sensa ya mwaka 2024/2025 imeonyesha mafanikio katika uhifadhi wa baadhi ya spishi muhimu huku nyingine zikikabiliwa na changamoto zinazotokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu karibu na maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema idadi ya tembo imeongezeka kutoka 46,408 mwaka 2014 hadi 66,714 mwaka 2025, nyati kutoka 242,946 hadi 328,437 na faru kutoka 142 hadi 285 katika kipindi hicho.
Spishi nyingine zilizoonyesha ongezeko ni tandala walioongezeka kutoka 3,877 hadi 6,417, pala hala kutoka 12,586 hadi 20,983, pofu kutoka 52,558 hadi 102,591 na korongo kutoka 3,488 hadi 6,904.
Hata hivyo, alisema sensa hiyo imebaini kuwa swala twiga limepungua kwa kiwango kikubwa, hali inayohusishwa na kuongezeka kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi ya binadamu katika maeneo jirani na hifadhi za wanyamapori.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, simba wameongezeka kutoka 16,800 hadi 17,200, twiga kutoka 27,478 hadi 29,185, chororo kutoka 1,079 hadi 1,320 na nyumbu kutoka 1,501,108 hadi 1,598,290.
Licha ya mafanikio hayo, wataalamu wameeleza kuwa idadi ya tembo waliopo sasa ni asilimia 53 pekee ya waliokuwapo mwaka 2005/2006, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mikakati ya uhifadhi na kukabiliana na migongano kati ya binadamu na wanyamapori ili kulinda bioanuwai ya Tanzania.












































0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia